ICTR YAHITIMISHA KUPOKEA USHAHIDI DHIDI YA WAZIRI WA ZAMANI WA RWANDA
Posted on
Jun 26, 2012
|
No Comments
Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) ilihitimisha upokeaji wa ushahidi maalum katika kesi inayomkabili mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari ambaye bado anasakwa na mahakama hiyo, Augustin Bizimana, Waziri wa zamani wa Ulinzi wa Rwanda.
‘’Naomba niwajulishe kwamba upokeaji wa ushahidi maalum katika kesi ya Bizimana umeendelea kwa kupata ushahidi kutoka kwa shahidi wa mwisho ambaye pia amehitimisha ushahidi wake leo.Hivyo basi kufuatia hatua hiyo, upokeaji ushahidi huo umehitimishwa,’’ alieleza Msemaji wa ICTR, Roland Amossouga.
Bizimana anashitakiwa kwa makosa ya mauaji ya kimbari, kula njama kutenda makosa hayo, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.
Kesi nyingine mbili za aina hiyo ambazo ushahidi wake umeshapokelewa ni pamoja na ile ya mtuhumiwa anayesakwa vikali na anayesadikiwa kuwa ndiyo mfadhili wa mauaji ya kimbari, Felicien Kabuga na Protais Mpiranya, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Walinzi wa Rais.
Utaratibu wa kupokea ushahidi katika kesi ya mshitakiwa ambaye bado hajakamatwa umewekwa ili kuhifadhi ushahidi husika uweze kutumika pindi mshitakiwa akitiwa mbaroni hapo baadaye.
Wakili wa Zamu wa Bizimana, Yitiha Simbeye aliita jumla ya mashahidi watatu kwa ajili ya utetezi wa mteja wake. Utetezi katika kesi ya Biziamana ulianza Mei 14, 2012.

