photo NAAZ_zpsd0bbd510copy_zps37715af5.jpg
 photo NAAZ_zpsd0bbd510.jpg
Nafasi Ya Matangazo
> | > LISSU AYATAJA MAJINA YA WABUNGE WATUHUMIWA WA HONGO; BAADHI YAO WAZUNGUMZA.

LISSU AYATAJA MAJINA YA WABUNGE WATUHUMIWA WA HONGO; BAADHI YAO WAZUNGUMZA.

Posted on Jul 31, 2012 | No Comments

Mnadhimu Mkuu wa kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu (Pichani) amewataja wabunge wa CCM ambao watuhumiwa wa hongo inayolihusisha na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO). 
Akizungumza na waandishi wa habari  mjini Dodoma jana, Lissu aliwataja pia wabunge wengine ambao ni wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini wenye mgongano wa kimaslahi na TANESCO na kampuni za kuuza mafuta .
Alisema wabunge hao,  wakiwa kama wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, hawajawahi kutangza mgongano wa maslahi kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Utumishi wa Umma ya mwaka 1995, “Wabunge wanaoguswa moja kwa moja na tuhuma hizi ni Mbunge wa Viti Maalum, Sara Msafiri na Munde Tambwe Abdallah (CCM). Wabunge hawa wawili wanafanya biashara na TANESCO ya kuiuzia matairi na hawajawahi kutangaza mgongano wa kimaslahi. Mbunge mwingine ni wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM) na yeye ni Mtaalamu Mwelekezi wa Kampuni ya Kuuza Mafuta ya Puma Energy na  Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini. Mwingine ambaye yupo kwenye kamati hii na ana mgongano wa kimaslahi ni Mbunge wa Korogwe Mjini, Yusuph Abdallah Nassir (CCM). Huyu ni mmiliki wa vituo vya mafuta na mwingine ni Mbunge wa Viti Maalum, Mariam Kisangi (CCM) ambaye naye anamiliki vituo vya mafuta,” alisema.
Alisema mjumbe mwingine, aliye katika Kamati hiyo anayetuhumiwa ni Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka, “Huyu hana mgongano wa maslahi wa moja kwa moja, lakini amekuwa mtetezi mkubwa wa makampuni yaliyonyimwa zabuni ya kuuza mafuta ya Oryx na Camel Oil,” alisema.
Pia alimtaja mbunge mwingine ambaye yupo katika kamati hiyo na ana mgongano wa maslahi kuwa ni Mbunge wa Viti Maalum, Vick Kamata (CCM). Hata hivyo hakuutaja mgongano huo wa kimaslahi.
Kuhusu wabunge wa Chadema walio katika Kamati ya Nishati na Madini, alisema wapo watatu lakini hawajaguswa na tuhuma zozote, “Wabunge wetu waliopo kwenye Kamati ni Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde na Mbunge wa Viti Maalum, Mrisho Taratibu Abama. Wabunge wetu hawajashiriki kwa namna yoyote katika vitendo vinavyotuhumiwa ila wameathirika kwa wao kuwa wajumbe wa kamati hiyo, lakini mwenye ushahidi wowote aulete tutaupokea,” alisema Lissu.
Kuhusu kuhusishwa na tuhuma hizo kwa Mbunge wa Kigoma Kaskani, Zitto Kabwe (CHADEMA ), alisema chama chake kinataka achunguzwe ili ukweli ujulikane, “Sisi kwa muda wa wiki nzima tangu tuhuma hizi zianze kutolewa, chama hakijapta nafasi ya kukaa naye na kupata maelezo yake. Lakini, tunataka na tuhuma zake zichunguzwe, hatuna maslahi yoyote katika jambo hili kwani kambi yetu haiwezi kuficha watu wachafu, chochote kinachosemwa juu yake kichunguzwe, majibu yatolewe hadharani ili na sisi tupate msingi wa kuanzia,” alisema
Alisema Kambi ya Upinzani, inamtaka Spika wa Bunge Anne Makinda kuvunja na Kamati nyingine zilizowahi kutuhumiwa kwa vitendo vya rushwa katika siku za hivi karibuni na kuziunda upya.
Alizitaja kamati hizo, kuwa ni Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa na Kamati ya Hesabu za Mshirika ya Umma, “Vilevile iwachukulie hatua wabunge wote waliotajwa kuhusika na vitendo vya rushwa, kwa kawaida bunge ni chombo cha kuisimamia Serikali sasa iweje wabunge wenyewe ndio watuhumiwe kwa makosa ambayo walipaswa kuisimamia Serikali,” alisema.
MAJIBU YA WATUHUMIWA


Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo, Kisangi alikiri kumiliki kituo cha mafuta lakini akasema sheria haimzuii mtu kama mambo yake anayafanya kwa uwazi, “Nimekuja bungeni nikitokea kwenye ualimu, nilikuwa nafundisha Shule ya Msingi ya Mianzini na biashara hii ni ya familia. Inaendeshwa kwa uwazi na mwanangu wa kwanza ndiye anayeisimamia. Kutokana na uwazi katika shughuli zangu, mwaka jana Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilinipongeza. Mimi ni msafi na siko huko wanakofikiri wao (CHADEMA).”
Alipozungumza na gazeti la MTANZANIA kwa simu, alisema hafanyi biashara na TANESCO ingawa anafanya biashara ya kuuza mafuta, “Kwanza kabisa sifanyi biashara ya mafuta na TANESCO, mimi nina biashara yangu ya kuuza mafuta kwa miaka mingi na pia kuna eneo langu moja pale Mbagala Rangi Tatu, Dar es Salaam ambalo lilichukuliwa na Kampuni ya Mafuta cha Kobil. Lakini hao, wanaolalamikia mimi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Nishati, wajue biashara ya mafuta nimeianza kwa zaidi ya miaka 20. Kwa hiyo, kitendo cha mimi kuingia katika kamati hiyo siyo kosa kwa sababu wabunge tunaingia kwenye kamati kutokana na uzoefu tulionao kwenye mambo fulani fulani. Mimi nilikuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mianzini na nina uzoefu wa mafuta, kwa hiyo, kuingia katika kamati hiyo siyo kosa na ndiyo maana hata huyo Tundu Lissu ni Mjumbe wa Kamati ya Sheria kwa sababu ni mwanasheria,” alisema Mariam.
Naye Nasri alipozungumza na MTANZANIA kwa simu alicheka, kisha akamwambia mwandishi wetu, kwamba kata simu sina cha kusema. Watuhumiwa wengine walipotafutwa kwa simu hawakupokea simu.
Kwa upande wake, Mwijage alikanusha kuwa mtaalamu mwelekezi wa Kampuni ya Puma, badala yake akasema ni mtaalamu wa petroli anayefanya kazi ya kuishauri Serikali kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu nishati hiyo, “Siyo kweli, hawa wanadandia hoja. Mimi ni mtaalamu wa petroli ambaye mchango wangu kimsingi una faida kubwa bungeni na hata kwa jamii kwa ujumla. Sijafanya maamuzi yeyote ya kulihujumu taifa hili na hata kwenye Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini pekee, nilitoa mchango wa kurasa 10 kuhusu masuala hayo ya petroli,” alisema
Aliishauri kambi hiyo ya upinzani kuvuta subira, akieleza kuwa jambo lililoko bungeni linahusu ufisadi na uhujumu uchumi hivyo kauli zinazotolewa bila utafiti zinaweza kuvuruga mchakato mzima uliokwishaanzwa na Kamati ya Maadili ya Bunge.
Awali, Abdallah alipoulizwa kuhusu tuhuma za kumiliki vituo vya mafuta hivyo kuwa na maslahi binafsi, alicheka na kuahidi kwamba angepiga simu baadaye, lakini hakufanya hivyo na alipopigiwa baadaye alikata simu. Hata hivyo, alizungumza na waandishi wa habari na kukanusha kumiliki vituo vya mafuta.
Kamata kwa upande wake alisema: “Kuna kamati maalumu imepewa kazi ya kuchunguza mambo hayo, hivyo yote yanayoulizwa yatakuwa wazi na ukweli utajulikana tu. Nina maslahi au sina ukweli mtaujua, haraka ya nini?.
via magazeti ya MTANZANIA na MWANANCHI

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru