Madaktari waibana serikali, watangaza kugoma
Posted on
Jun 9, 2012
|
No Comments
CHAMA Cha Madaktari Tanzania (MAT) kimetangaza mgogoro na Serikali na kuipa wiki mbili kuyapatia ufumbuzi matatizo yao la sivyo watafanya mgomo wa nchi nzima. Wametoa msimamo huo walipokutana jana jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku chache baada ya ujumbe wao uliokuwa kwenye mazungumzo na Serikali kugoma kusaini makubaliano kwa kile walichoeleza mpaka wapate ruksa ya wanachama. Jana ilikuwa ni siku ya ujumbe huo kuwasilisha taarifa ya makubaliano ambayo Serikali ilitaka waisaini na hivyo wanachama hao hawakuyaridhia hivyo kuamua kutangaza mgogoro.
Habari zilizoifikia Mwananchi Jumapili kutoka ndani ya kikao hicho cha ndani zilieleza kuwa madai ambayo Serikali imeshindwa kuyatekeleza ni nyongeza ya mishahara, mazingira mazuri ya kazi, marupurupu, nyongeza ya posho ya wito wa dharura, posho za nyumba na chanjo.
