Mbunge wa Bahi amepandishwa kizimbani leo kwa tuhuma za rushwa.
Posted on
Jun 4, 2012
|
No Comments
Mbunge wa Bahi, Omar Ahmed Badwel leo amepandishwa katika kizimba cha mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa tuhuma za kudai rushwa ya Shilngi milioni 8/= na kupokea kianzio cha Shilingi milioni 1/=.
Mbele ya Hakimu Mkazi, Faisal Kahamba, Maakili wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Janeth Machullia na Ben Lincolni kuwa, mshtakiwa anakabiliwa na makosa mawili ya rushwa, mosi ikiwa ni kosa la rushwa ambalo ni kinyume na kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya mwaka 2007
Imeelezwa kuwa, mnamo tarehe 30 Mei 2012, mtuhumiwa alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkuranga, Pwani, Sipora Liana ampe kiasi cha fedha ili aweze kupitisha ripoti ya taarifa ya fedha ya mwaka 2011/2012 ya Halmashauri hiyo.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa na maofisa wa TAKUKURU tarehe tajwa ya kosa kutendeka, majira ya saa 9 alasiri, katika hoteli ya Peacock (Dar es Salaam), wakati anapokea rushwa kutoka kwa maafisa wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga.
Wakili wa mtuhumiwa, Mpare Mpoki alikana mashitaka hayo.
Mahakama imeruhusu mtuhumiwa kupewa dhamana ya watu wawili ambapo kila mdhamini anapaswa kutoa dhamana ya fedha kiasi cha Shilingi milioni 4/= na hati za kusafiria. Masharti ya dhamana yalitimizwa na mtuhumiwa ameachwa hadi tarehe 18 Juni atakapohitajika mahakamani hapo tayari kwa kesi kutajwa na kisha kupangiwa tarehe ya kusomewa maelezo ya awali.
Bedwel ni mmoja kati ya wabunge wawili waliotajwa na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR Mageuzi) katika Bunge la Bajeti mwaka jana kwamba waliomba rushwa katika halmashauri ambayo hakuitaja.
Akichangia Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano, Kafulila aliwataja bungeni Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi na Mbunge wa Bahi, Omary Badwel wote wa CCM akidai kwamba aliwakuta wakiomba rushwa kwa viongozi wa halmashauri.
Wakati akitaja majina hayo, Kafulila nusura aingie katika mgogoro na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge, George Simbachawene ambaye alikuwa akimwamuru kukaa chini kutokana na muda wake wa kuchangia kumalizika. Hivi sasa Simbachawene ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini.
Wakati Simbachawene akimwamuru akae chini, Kafulila alikuwa akiendelea kuzungumza bila kujali kengele ya pili iliyopigwa kuashiria kwamba muda wake ulikuwa umekwisha.
"Mheshimiwa Mwenyekiti kwa wakati wa sasa ni vigumu kusimamia matumizi kwani mfumo wetu wa uongozi unaruhusu ufisadi, wapo viongozi, mawaziri, wabunge wanaomba rushwa...." alisema Kafulila na kuamsha zogo ambalo liliambatana na sauti zisizo rasmi katika ukumbi wa Bunge zikiuliza ".....wapo humu humu?" Kafulila alijibu "Ndiyo..."
Sauti moja ilisema wataje, hapo ndipo aliposema "....Wapo kina Zambi, Badwel, niliwakamata na nilichukua hatua, hatuwezi kuendelea namna hii," kisha akaketi.
Baada ya dakika chache tangu alipoketi, Kafulila alionekana akiteta jambo na Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali na Augustine Mrema wa Vunjo na baadaye Mkosamali aliomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge, akitaka waliotuhumiwa watajwe ili wafahamike vizuri.
Zambi na Badwel ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa pamoja na Kafulila chini ya Mwenyekiti wao, Mrema.
Mwenyekiti wa Bunge, Simbachawene akijibu hoja hiyo alisema atatoa mwongozo wake baadaye, katika muda ambao ataona unafaa. Hata hivyo, hadi sasa hakuna mwongozo ambao umetolewa na bunge kuhusiana na kauli ya Kafulila.
