JUKWAA LA SANAA LAMKUMBUKA MWANDISHI ALIYEUAWA IRINGA
Posted on
Sep 3, 2012
|
No Comments
Na Mwandishi Wetu
Kongamano la Jukwaa la Sanaa ambalo huendeshwa kila wiki, jana lilianza kwa kumkumbuka Mwandishi wa Habari na mwakilishi wa Kituo cha Channel Ten, Daud Mwangosi aliyefariki dunia juzi katika vurugu zilizotokea katika kijiji cha Nyololo mkoani Iringa.
Kabla ya kuanza kwa kongamano hilo jana, Mwendeshaji wa kongamano hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni nchini, (CAJAtz) Hassan Bumbuli aliwataka washiriki kusimama kwa dakika moja kumkumbuka mwandishi huyo ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa.
Katika kongamano hilo ambalo jana lilijadili mada ya Sanaa za jukwaani na guvu yake katika kufikisha ujumbe kwa hadhira, mwasilishaji wa mada hiyo Chediel Senzighe kutoka kundi la Jakaya Theatre, aliwakata wasanii kuandaa kazi kwa kuzingatia maadili na kanuni ili kuepusha kuipotosha jamii.
“Sanaa ina nguvu sana katika kufikisha ujumbe, kama ni muuaji basi sanaa inauwezo wa kuua watu wengi kwa wakati mmoja, daktari akikosea katika upasuaji ataua mgonjwa mmoja, lakini maudhui ya kazi ya sanaa yakikosewa yanaathari kwa watu wengi na kwa wakati mmoja. Sasa ni vyema wasanii tukawa makini katika kuandaa kazi zetu na zaidi tufanye utafiti kabla hatujaamua kuandaa maudhui ya kazi zetu,” amesema Senzighe.
Wakichangia mada hiyo, washiriki wa kongamano hilo wamesema tatizo kubwa linalowakabili wasanii siku hizi ni uvivu wa kusoma na kujifunza na ndiyo maana wanaandaa kazi za kulipua huku akili zao zikiwaza fedha zaidi kuliko kufikiria wanachokipeleka kwa jamii kinaweza kuleta athari gani.
“Wasanii wetu lazima wabadilike sasa, wafanye utafiti kabla ya kuandaa sanaa hasa sanaa za jukwaani au filamu hii itasaidia sana kuandaa maudhui mazuri ambayo pia yataisaidia jamii,” amesema Godfrey Lebejo Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, mafunzo na habari wa BASATA.
Awali wakati akifungua kongamano hilo, Katibu Mkuu wa CAJAtz, bwana Bumbuli, alieleza kusikitishwa na kifo cha kinyama kilichomtokea Mwandishi wa Channel Ten na kusema matumizi ya nguvu kupita kiasi ya jeshi la Polisi yanahitaji kukomeshwa mara moja hasa kwa kuwa yanagharimu maisha ya watu bila sababu za msingi.
“Inatusikitisha kama wanatsnia ya habari na kama Watanzania, nguvu za polisi zinaacha majereha makubwa kwa watu na sasa zinagharimu maisha ya watu, nguvu hizi hazina sababu na lazima zikemewe na kulaaniwa kwa nguvu zote,” amesema Bumbuli.
SINZIGHE: Mwasilishaji wa mada katika jukwaa la Sanaa bwana Chediel Senzighe akisisitiza jambo wakati akitoa mada kwenye kongamano la Jukwaa la sanaa, jijini Dar es Salaam jana.
JUKWAA: Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni Tanzania (CAJAtz) Hassan Bumbuli akizungumza katika Kongamano la Jukwaa la Sanaa hapo jana.kulia ni msanii Chediel Senzighe aliyekuwa muwasilishaji mada katika kongamano hilo.
JUKWAA: Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni Tanzania (CAJAtz) Hassan Bumbuli akizungumza katika Kongamano la Jukwaa la Sanaa hapo jana.kulia ni msanii Chediel Senzighe aliyekuwa muwasilishaji mada katika kongamano hilo.