photo NAAZ_zpsd0bbd510copy_zps37715af5.jpg
 photo NAAZ_zpsd0bbd510.jpg
Nafasi Ya Matangazo
> > HIVI NDIVYO MABILIONI HUTOROSHWA NJE YA NCHI KIPINDI CHA UCHANGUZI

HIVI NDIVYO MABILIONI HUTOROSHWA NJE YA NCHI KIPINDI CHA UCHANGUZI

Posted on Sep 2, 2012 | No Comments



KIASI kikubwa cha fedha hutoroshwa na kufichwa nje ya nchi wakati taifa linapokuwa katika uchaguzi, vita na matatizo ya kiuchumi.
Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umebaini kuwa katika mazingira hayo, kuanzia mwaka 1970 hadi 2004, jumla ya Dola 3,899.6 milioni za Marekani, sawa na takriban Sh6.2 trilioni zimebainika kutoroshwa na kufichwa kwenye benki za nje ya nchi ikiwamo Uswisi.
Kiwango hicho cha fedha kimezingatia ubadilishaji wa fedha wa Dola moja ya Marekani kwa Sh1,600.
Ripoti ya utafiti uliofanywa na Shirika la Global Financial Integrity,  inaonyesha kuwa kiasi kikubwa cha fedha hizo kilitoroshwa katika kipindi cha mwaka 1977, 1978, 1985 na 2004.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mwaka 1977 ndipo Jumuiya ya Afrika Mashariki ilipovunjika, mwaka 1978 Tanzania iliingia katika vita vya Kagera dhidi ya majeshi ya Uganda, wakati huo yakiongozwa na  Idd Amin.
Mwaka 1985 ulikuwa mwaka wa uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge ambapo Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliondoka madarakani na nafasi yake kuchukuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi.
Mwaka 2004 pia kilikuwa kipindi cha uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge ambapo Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alikuwa akimalizia ngwe yake ya miaka 10 kukaa madarakani.
Uchaguzi huo uliofanyika Oktoba mwaka 2005 ndiyo uliomwigiza madarakani Rais Jakaya Kikwete, ambaye kipindi cha miaka 10 ya utawala wake kitamalizika mwaka 2015.
Katika taarifa hiyo ya Global Financial Integrity, mwaka 1977 Tanzania ilipoteza Dola 539.9 milioni sawa na Sh863.8 bilioni.
Imebainisha kuwa mwaka 1978, ambapo taifa lilikuwa katika wakati mgumu wa vita na Uganda, wajanja wachache walifanikiwa kutorosha Dola 635.8 milioni sawa na Sh1.01 trilioni.
Wakati vita hivyo vikitumiwa kama mwanya wa kuiba kiasi hicho cha fedha, mwaka 1985 ambapo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliamua kustaafu na Mwinyi kuchukua madaraka, kiasi cha Dola 1,577.9 milioni sawa na Sh2.5 trilioni kilitoroshwa.
Taarifa hiyo pia inaonyesha kuwa mwaka 2004 kipindi ambacho mbio za kuwania urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 zilianza, Tanzania ilipoteza Dola 1,146 milioni (Sh1.8 trilioni) zilizofichwa katika benki za nje ya nchi.

Fedha zinavyotoroshwa
Kwa mujibu wa Shirika la Global Financial Integrity, kuna njia nyingi zinazotumiwa na watu hao kuiba fedha hizo.
Limetaja njia moja kuwa ni kuingiza rekodi mbalimbali kwenye vitabu husika na maelezo mengine, kutoingizwa kwenye vitabu vya hesabu za Serikali au mashirika.
Kiasi hicho ambacho huachwa kwa makusudi baada ya kufanyika ujanja wa hesabu, ndicho hufichwa kwenye akaunti za nje ya nchi.
Limetaja pia biashara za kimataifa kuwa njia nyingine, ambapo, watu hao wasio waaminifu huongeza bei ya bidhaa au huduma husika na kurekodi hesabu za bei inayofahamika, huku kiasi kingine kikitoroshwa nje.
Taarifa hiyo inabainisha kuwa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF), hushindwa kugundua ujanja huo mapema kutokana na taarifa zinazowasilishwa katika benki hizo kuwa ni zile zilizo kwenye vitabu na zilizorekodiwa.
Inaongeza kuwa fedha nyingi pia zilitoroshwa baada ya kukosekana kwa taarifa muhimu za masuala mbalimbali ya kifedha.
Katika ripoti hiyo, imebainika pia kwamba awamu ya nne ya uongozi wa Tanzania ndipo fedha nyingi zilitoroshwa kwenda nje ya nchi.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa katika kipindi cha utawala wa kwanza ulioisha mwaka 1985, fedha zilizofichwa nje zilikuwa Dola 3,498.3 milioni (sawa na Sh5.5 trilioni).
Katika Awamu ya Tatu  ya Rais Benjamin Mkapa zilizotoroshwa Dola 2,108.8 milioni (Sh3.3 trilioni), wakati katika Awamu ya Pili ya Mzee Mwinyi zilitoroshwa Dola 529.1 milioni (Sh846 bilioni).
Utafiti huo pia unaonyesha pia nchi 20 za Afrika zinazoongoza kuficha fedha nje huku Nigeria ikiwa kinara.
Jumla ya Dola za Marekani 1.8 trilioni zimefichwa katika benki mbalimbali nje ya nchi kutoka nchi za Kiafrika katika kipindi cha mwaka 1970 hadi 2009.
Akizungumzia suala hilo, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya alisema Serikali inatambua uwepo wa tatizo hilo na tayari imeanzisha mikakati ya kukabiliana nalo.
Alisema kuwa Wizara ya Fedha imeanzisha kitengo maalumu kiitwacho Financial Intelligence Unit, ambacho pamoja na mambo mengine kitashughulikia utoroshwaji wa fedha nje ya nchi.
“Suala hilo tumeliwekea mikakati na tayari tumeshaanzisha kitengo kinachoshughulikia suala hilo, tunachohitaji ni kuongeza nguvu kazi kwa sababu inahitajika watu wenye uzoefu mkubwa,” alisema naibu waziri huyo.
Alifafanua kuwa kitengo hicho kitafanya kazi Tanzania Bara na Visiwani na kuongeza kuwa sheria ya kuzuia fedha haramu itaanza kutekelezwa hivi karibuni, akisema kuwa anaamini itasaidia kukabiliana na tatizo hilo.
Akizungumza kwa njia ya simu, Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Delfin Rwegasira alisema kuwa chanzo kikubwa cha watu kutorosha fedha nje ya nchi ni kukosekana kwa uwazi na ufisadi.
Alifafanua kuwa tangu kuanza kwa mfumo huru wa kiuchumi, kumekuwa na wafanyabiashara waliotumia mianya ya uhuru wa kiuchumi kukimbiza fedha hizo.
“Sidhani kama nchi kuwa katika misukosuko kunaweza kuwa chanzo cha utoroshwaji wa fedha, chanzo kikubwa ni kukosekana kwa uwazi na rushwa,” alisema Dk Rwegasira.
Aliongeza kuwa kutoroshwa kwa fedha nje ya nchi kunaweza kutokea pale wafanyabiashara wanapokuwa na shaka na biashara zao au mustakabali wao katika nchi, hivyo ili kuhakikisha hawapati matatizo kiuchumi huanza kukimbiza fedha zao nje ya nch

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru