TAMKO LA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) KUHUSIANA NA MAUAJI YA IRINGA.
                              Posted on 
                              Sep 5, 2012
                            |
                            
                                  No Comments
                                  
| Nape Nnauye | 
- 
CCM imevitaka vyombo na tume zilizoundwa kuhusiana na kifo cha mwandishi wa habari Daudi Mwangosi, vichunguze kwa umakini na weledi mkubwa ili kubaini kila kitu ikiwemo chanzo cha vurugu zilizotokea na mazingira yaliyosabaisha kipigo hadi kufa mwandishi huyo.
Aidha imetaka uchunguzi usichukue muda mrefu ili ukweli kuhusiana na kadhia hiyo ujulikane mapema na hatua zichukuliwe kwa kila atakayebainika kuwa sababu au chanzo cha vurugu na kifo cha mwandishi huyo.
Aidha imesema imepokea kwa masikitiko makubwa sana taarifa za kifo hicho na kujeruhiwa kwa askari watatu wa Polisi wakati wa vurugu hizo na kimetoa pole kwa wafiwa, wanahabari wote nchini na wote walioguswa na msiba huo kwa namna moja au nyingine.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye katika taarifa ya CCM kwa vyombo vya habari, leo jijini hapa, kuhusiana na sakata la vurugu hadi kifo cha mwandishi huyo, juzi mkoani Iringa.
"Itakumbukwa tarehe Septemba 2, 2012 katika operesheni za CHADEMA mkoani Iringa kulitokea vurugu zilizosababisha kuuawa kwa mwandishi wa habari mzoefu, Daudi Mwangosi na kujeruhiwa vibaya kwa polisi watatu wa kikosi cha kutuliza ghasia.
Chama  Cha Mapinduzi kimepokea kwa masikitiko makubwa sana taarifa za kifo  hicho na kujeruhiwa kwa askari hao", Nape alisema katika taarifa hiyo,  na kuongeza:
"CCM  inachukua nafasi hii kutoa pole kwa wafiwa, wanahabari nchini na wote  walioguswa na msiba huu kwa namna moja au nyingine na tunatoa mwito kwa  vyombo na tume mbalimbali zilizoundwa kuchunguza swala hili, vichunguze  kwa umakini na weledi mkubwa ili kubaini yote - ikiwemo chanzo cha  vurugu zilizotokea na mazingira ya kifo cha ndugu yetu".
Alisema  CCM  inasikitishwa na mfululizo wa matukio ya watu kupoteza maisha au  kujeruhiwa katika mikutano na operesheni mbalimbali zinazoendeshwa na  CHADEMA nchini hasa zile zilizofanyika kwa kukaidi amri halali za vyombo  vya ulinzi na usalama.
Alikumbusha  baadhi ya matukio hayo kuwa ni pamoja na lile la kuuawa kwa kada wa CCM  Mkoani Singida, kuuawa kwa Ally Hassan mjini Morogoro na la juzi la  kuuawa kwa Mwangosi Mjini Iringa, kujeruhiwa kwa askari polisi Iringa na  matukio mengine mengi ambayo yametokea wakati CHADEMA wakiendesha  operesheni zao mbalimbali nchini.
"Matukio  haya si mazuri kutokea kwenye shughuli za Chama cha siasa. Kwakweli ni  aibu, inayohitaji uwajibikaji,hata kama ni wa kisiasa. Inapotokea  shughuli za chama chako zinasababisha kupotea kwa maisha ya watu kila  unapozifanya na bado usitake kuwajibika, inahitaji roho ngumu na ujasiri  wa aina yake" alisema Nape katika taarifa hiyo na kuongeza;
"Inakuwa  mbaya zaidi pale vifo hivi vinaposababishwa na Chama hicho kutotii amri  halali zilizotolewa kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi inayovipa  pia uhalali  vyama vya siasa kuwepo na kuendesha shughuli zake kwa  mujibu wa sheria".
"Laiti  Chama hicho kingesubiri siku chache zilizobakia kabla ya Sensa kuisha  kabla ya kuendelea na mikutano yake ni dhahiri mauaji haya yasingetokea.  Lakini kauli za kukebehi na uamuzi wa kukaidi amri ya Jeshi la Polisi  na kusema "tupo tayari kwa lolote" ni ishara kwamba Chama hiki kiliandaa  na kujiandaa na fujo zilizotokea", alisema Nape.
CCM  imetoa mwito kwa vyama vya siasa na wanasiasa kwa ujumla kujenga  utamaduni wa kuheshimu utawala wa sheria na kusema kwamba amani na  utulivu vilivyopo nchini ni kazi nzuri iliyojengwa kwa muda mrefu na  waasisi wa taifa la Tanzania kwa kujenga utamaduni wa kuzingatia utawala  wa sheria.
