NENO LA LEO NA MAGGID MJENGWA: MWALIMU NYERERE NA MRADI WA UJENZI WA UMOJA WA KITAIFA.
Posted on
Oct 14, 2012
|
No Comments

Ndugu zangu,
Leo
ni siku ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere. Asubuhi hii hapa Iringa
najiandaa kwenda kwenye mjadala ulioandaliwa na Kigoda Cha Mwalimu pale
Chuo Kikuu cha Mkwawa. Hapo kuna mada yenye kuhusisha suala la Muungano
kwenye uandikaji wa Katiba Mpya. Nimeambiwa, kuwa kutakuwa na
wazungumzaji mahiri, akina Zitto Kabwe, January Makamba na wengine.
Hawa
ni vijana pia. Nitapenda sana kwenda kuwasikiliza na kujifunza. Lakini,
tunapozungumzia Muungano kwenye kuandika Katiba mpya inahusu pia mradi
mkubwa wa Ujenzi wa Umoja wa Kitaifa ambao Mwalimu Nyerere aliuanzisha,
aliusimamia, hata hivyo, tunaona sasa unavyoporomoka na kuliacha taifa
letu mashakani. Inahusu Mradi wa Ujenzi wa Umoja wa Kitaifa. Mwalimu
alijenga misingi imara ya Ujenzi wa Umoja Wa Kitaifa ( Nation Building).
Kuijenga
jamii ya Watanzania yenye kuamini kwenye ukweli kuwa sisi sote ni
ndugu. Kwamba Nchi yetu haina dini. Yenye kupiga vita ubaguzi wa aina
zote, iwe wa rangi, kabila au dini. Ilimchukua Mwalimu na taifa letu
miaka mingi sana kuijenga misingi hiyo iliyowawezesha pia Watanzania
kuwa na mioyo ya uzalendo kwa Taifa lao.
Tunaona
sasa, kazi hiyo iliyochukua miaka mingi, kutokana na ubinafsi na uroho
wa madaraka ya baadhi ya wanasiasa wetu, wanapelekea kubomoka kwa
misingi hiyo na kuliacha taifa letu kwenye hatari ya kuangamia. Ndio,
msingi wake ni ubaguzi wa kisiasa unaotokana na ubinafsi na tamaa ya
mali kwa baadhi ya tuliowapa dhamana za kufanya maamuzi makubwa kwa
niaba yetu.
Ni
hali ya baadhi ya tuliowapa dhamana za uongozi kuishiwa chembe chembe
za uzalendo; mapenzi kwa nchi yao.Ni watu wenye kulinda maslahi yao na
ya wanaowazunguka. Wako tayari hata kutumia mbinu za Umafia kutimiza
malengo yao. Watanzania wengi sasa wanaopoteza moyo wa uzalendo kwa nchi
yao.
Kuna
hata wenye kufikia kutamka; ‘Nchi hii ina wenyewe’. Kuna anayetamka
hilo kwa lengo la kumtishia mwenzake au kulazimisha kitu fulani
kifanyike. Lakini, kuna wenye kutamka hivyo kuashiria kukata tamaa. Kuwa
hata wafanye nini, hakuna anayewasikiliza ama kuwajali.
Hizi
si dalili njema kwa taifa. Kuna wanaoiba mali ya umma mchana wa jua
kali. Hakuna anayewagusa. Ukiuliza utajibiwa; “Ah! Nchi ina wenyewe!”.
Kwamba kuna baadhi yetu hawajisikii kuguswa na nchi hii, hawajisikii
kuwa na nguvu ya kupiga vita maovu yanayotusumbua. Baadhi yetu wameanza
kupungukiwa na mapenzi na nchi yao.
Ni
hatari. Tuna lazima ya kuwa na ujasiri wa kupigania maslahi ya nchi
yetu. Ni heri kufa kwa kupigwa risasi kuliko fedheha ya kufa kwa kuumwa
na mbu wa Malaria katika nchi ambayo ina rasilimali za kutuwezesha
kujenga uwezo wa kuangamiza malaria.
Lakini,
tunakubali wachache miongoni mwetu wahujumu rasilimali zetu. Juni 16,
2004 nilipata kuandika hili kwenye gazeti la Majira; kuwa Tanzania ina
vyote, kasoro Watanzania. Niliandika; kuwa Tanzania ni nchi nzuri sana.
Ni nchi ya kujivunia. Kwamba Tanzania ni nchi kubwa sana kwa eneo.
Ni
nchi yenye rasilimali nyingi; ardhi yenye rutuba, mito, maziwa, milima,
mabonde, bahari na vivutio vingi vya asili. Hata hivyo, Tanzania ni moja
ya nchi masikini sana duniani. Kwa nini? Ndio, kikubwa kinachokosekana
Tanzania ni Watanzania.
Tanzania
tunayoijenga sasa ni mkusanyiko tu wa watu wa makundi mbali mbali wenye
kwenda kwa staili ya ‘kila mtu na lwake’. idadi ya Watanzania wenye
uzalendo na mapenzi kwa nchi yao inazidi kupungua. Ubinafsi umekithiri,
na ubinafsi mbaya zaidi ni ule wenye kufanywa na viongozi.
Na hilo ni Neno la Leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa,
0788 111 765
