TUZO YA MO IBRAHIM IMEKOSA MSHINDI
Posted on
Oct 15, 2012
|
No Comments

Mo Ibrahim
Mwaka huu hakuna mshindi wa tuzo ya Mo Ibrahim ambayo hutolewa kwa viongozi wa Afrika walioonyesha uongozi bora
Tuzo hiyo ya dola milioni tatu nukta mbili,
hutolewa kwa kiongozi wa Afrika aliyechaguliwa kwa njia ya demokrasia na
ambaye aliimarisha hali ya maisha ya wananchi wake na kisha kuondoka
ofisini kwa khiari.
Kamati iliyokutana kumteua mshindi
iliafikiana kuwa hakuna kiongozi aliyetimiza matakwa yote yaliyohitajika
kuweza kuwa mshindi wa tuzo hiyo.
Mwaka jana Rais wa Cape Verde Pedro Verona Pires ndiye alishinda tuzo hiyo.
Aliongoza vita dhidi ya watawala wa kikoloni wa
Ureno , aliongoza siasa za vyama vingi na kusifiwa kwa kuimarisha maisha
ya wananchi wake.
Tuzo hiyo hutolewa katika kipindi cha miaka kumi na mshindi hupokea dola laki mbili kila mwaka maishani mwake.

Rais wa Cape Verde Pedro Pires
Akitangaza uamuzi huo, Ibrahim alisema "mtu
hutandika anapotaka kulala. Ikiwa lengo letu ni kutoa tuzo kwa uongozi
bora, lazima tutii vigezo vyetu wenyewe. Hatuwezi kujihujumu wenyewe''
''Sisi hatupo kwenye biashara ya kutoa ujumbe
mzuri usio na manufaa, ikiwa tutafanya kinyume na kazi yetu, basi
tutapoteza ushawishi wetu. Kamati ya tuzo hiyo ilitizama baadhi ya
washidani lakini hakuna aliyetimiza matakwa yetu yote. '' alisema
mwanachama wa kamati ya tuzo hiyo, Salim Ahmed Salim.
Washindi wengine wawili, katika miaka sita tangu
kuzinduliwa kwa tuzo hiyo, walikuwa marais wa Botswana Festus Mogae na
aliyekuwa Rais wa Msumbiji Joaquim Chissano.
Mapema mwezi huu wakfu wa Mo Ibrahim ulimtuza
tuzo maalum ya dola milioni moja, Askofu mstaafu wa Afrika Kusini
Desmond Tutu kwa kupigania haki za wananchi wa Afrika Kusini.
