WACHEZAJI 20 WALIOITEKA ULAYA KWA KUZISAIDIA TIMU ZAO
Posted on
Nov 19, 2012
|
1 Comment

Kabla ya kuwataja wachezaji bora 20
ambao wameiteka Ulaya, napenda kuthamini mchango wa wachezaji hawa
katika timu zao Yaya Toure, Xavi, Mario Gotze, Wayne Rooney, na Hazard.
Hawa wamekuwa kwenye viwango bora kabisa msimu huu huku wakiziwezesha
timu zao katika kupata matokeo bora.
Frank Ribery (20)
Frank Ribery (20)

Mfaransa huyu amekuwa akijitolea kila
kitu kwa ajili ya klabu yake ya Bayern Munchen. Licha ya matatizo yake
ya kugombana na winger mwenzake wa Bayern, Arjen Robben mara kwa mara,
Ribbery amekuwa bora mara zote anapoingia ndani ya uwanja. Hivi karibuni
Ribbery alikaririwa akisema kwamba anaipenda Bayern kuliko timu ya
taifa ya nchi yake, Ufaransa. Ribbery anashika nafasi ya 20 katika
viwango hivi.
Edin Dzeko (19)
Edin Dzeko (19)

Amekuwa akitokea pale anapohitajika.
Edin Dzeko amekuwa bora zaidi msimu huu hasa pale anapotokea benchi,
watu kama Edin huitwa Super Sub. Yeye ndiye mtu ambaye amekuwa akiipa
matokeo mazuri Manchester City mara kwa mara pale inapoonekana
kushindwa. Huku akiwa na kiatu cha ufungaji bora cha ligi kuu ya
Ujerumani pia mchezaji bora wa wachezaji wa ligi kuu ya Ujerumani,
Dzeko ameendelea kumuonesha Roberto Mancini yeye ni mchezaji wa aina
gani. Dzeko amekuwa wa 19.
Demba Ba (18)
Demba Ba (18)

Huu ndio ulikuwa usajili bora wa msimu
wa 2011/2012 kulingana na makocha wa timu za ligi kuu ya Uingereza.
Baada ya Papiss Cisse kusajiliwa January, 2012, Ba alifunga goli moja
tu, tangu msimu huu kuanza imekuwa kinyume chake, Cisse hafungi na Ba
amerudi kuwa roho ya timu. Kama akiendelea na kiwango hiki Ba anaweza
kuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya Uingereza. Ba anashika nafasi ya 18.
Marco Reus (17)
Marco Reus (17)

Moja ya vipaji kutoka Ujerumani
vinavyokuja kwa kasi ni huyu Marco Reus. Akisajiliwa kutoka Borussia
Monchengladbach kuja kuziba pengo la Shinji Kagawa, Marco ameweza
kushirikiana vyema na Mjerumani mwenzake, Mario Gotze pia mshambuliaji
Lewamdowski katika kuiboresha timu ya Borussia Dortmund. Marco Reus
ndiye mchezaji bora wa Ujerumani kwa mwaka huu, 2012. Reus anashika
nafasi ya 17.
Thomas Muller (16)
Thomas Muller (16)

Mchezaji bora kijana wa kombe la dunia,
2010. Baada ya kuwa akitokea benchi msimu uliopita wakati Mario Gomez
alipokuwa katika kiwango cha juu. Thomas Muller amekuwa akitengeneza
chemistry nzuri na mshambuliaji mwingine wa Bayern Munich, Claudio
Pizzaro. Mara nyingi Muller amekuwa hatajwi sana midomoni mwa wapenda
kabumbu lakini yeye amaandelea kutunza kiwango chake vyema na sasa yupo
kwenye kiwango cha hatari. Amekuwa wa 16.
Klaas-Jan Huntelaar (15)
Klaas-Jan Huntelaar (15)

Wenyewe humwita Hunter, amekuwa
akifananishwa na Ruud van Nistelrooy na Marco van Basten kutokana na
jinsi anavyouchezea mpira. Kocha wa zamani wa Barcelona Louis van Gaal
aliwahi kusema kwamba huyu ndiye mchezaji bora katika dimba la penalti.
Tangu ajiunge na Schalke 04 akitokea Milan, Huntelaar amekuwa kwenye
kiwango bora na ndiyo mhimili wa Schalke. Hivi sasa ana ushirika mzuri
kabisa na Mholanzi mwenzake aitwaye, Ibrahim Affelay. Amekuwa wa 15.
Oscar (14)
Oscar (14)

Kipaji cha ajabu kutoka Brazil. Uwezo wa
kumiliki mpira, nguvu, pasi na jinsi anavyojitoa uwanjani haipingiki
kwamba Oscar atakuja kuwa moja ya wachezaji hatari sana katika timu ya
taifa ya Brazil. Oscar ndiye mchezaji wa Chelsea anayeng’ara zaidi
katika ligi ya mabingwa Ulaya msimu huu kuliko mchezaji yeyote mwingine
ndani ya klabu. Goli la pili aliloifunga Juventus katika mechi yake ya
kwanza ya ligi ya mabingwa Ulaya halitafutika kirahisi katika vichwa vya
wapenzi wengi wa soka. Alipoulizwa atoe maoni yake kuhusiana na goli
lile, kipa wa Juventus, Gigi Buffon alisema hivi, “Siwezi kusema ni
vizuri kufungwa goli lakini ni vizuri kuwa sehemu ya goli bora kama
lile. Hongera kwake”. Oscar ni wa 14.
Maroune Fellaini (13)
Maroune Fellaini (13)

Mchezaji ghali zaidi wa klabu ya
Everton. Huyu ndiye alikuwa gumzo zaidi wakati ligi ya Uingereza
ilipokuwa katika wiki za mwanzo mpaka sasa. Akiwa ni mzaliwa Ubelgiji na
asili ya Morocco, Maroune Abdellatif Fellaini amekuwa kiwango bora
zaidi msimu huu kuliko msimu mwingine wowote katika maisha yake. Watu
wengi wamekuwa wakiifuatilia Everton kwa sababu ya huyu mtu na yeye
ndiye ubongo nyuma ya mafanikio ya Everton kwa msimu huu. Anazivutia
klabu kubwa nyingi huku Chelsea ikiongoza mbio za kumnyakua, si ajabu
kuona akihamia kwenye timu inayoendana na kiwango chake. Amekuwa wa 13.
Gonzalo Higuain (12)
Gonzalo Higuain (12)

Mtambo wa magoli kutoka mzaliwa wa
Ufaransa. Huyu ndiye patna wa Cristiano Ronaldo katika kupasia mipira
nyavuni pale Real Madrid kwa sasa. Mafanikio ya Gonzalo msimu huu
yamechangiwa zaidi na kuumia na kiwango cha Karim Benzema kushuka.
Katika siku za hivi karibuni Higuain amekuwa akishirikiana vyema na
Lionel Messi katika kutengeza nafasi za magoli katika timu ya taifa ya
Argentina. Amekuwa wa 12.
Luis Suarez (11)
Luis Suarez (11)

Mchezaji ambaye amekuwa akiandamwa na
mikasa ya kutosha tangu adake mpira uliokuwa ukiingia nyavuni katika
mechi ya robo fainali ya kombe la Dunia pale Afrika Kusini dhidi ya timu
ya Ghana. Pamoja na mikasa mingi kuwa upande wake Luis Suarez hajashuka
kiwango na msimu huu tofauti na misimu mingine amekuwa akifunga magoli
mengi ingawa timu yake ya Liverpool bado mambo hayajawa mazuri. Ndiye
mchezaji anayeng’ara zaidi kwa majogoo wa jiji. Amekuwa wa 11.
Andrea Pirlo (10)
Andrea Pirlo (10)

Ule usemi wa ng’ombe hazeeki maini
uhalisia wake huonekana hapa. Watumiaji wa mvinyo humfananisha Andrea
Pirlo na kinywaji hicho, kadri kinywaji kinavyozidi kukaa ndivyo ubora
wake unavyoongezeka. Kadri umri wa Pirlo unavyoongezeka ndivyo kiwango
chake kinavyoongezeka. Huyu ndiye chachu hasa ya mafanikio ya Juventus
katika kumaliza msimu uliopita bila kufungwa na Italia kufika kwenye
fainali ya kombe la Ulaya. Amefunga 10 bora.
Juan Mata (9)
Juan Mata (9)

Pamoja na kwamba Didier Drogba ndiye
aliyeiwezesha Chelsea kushinda kombe la FA na lile la ligi ya mabingwa
Ulaya kwa kiasi kikubwa katika mechi za fainali, Mata ndiye aliyekuwa
mchezaji bora wa Chelsea kwa msimu uliopita. Msimu uliopita Mata alikuwa
kwenye kiwango bora lakini sasa hivi amekuwa zaidi ya alivyokuwa msimu
uliopita. Juan Manuel Mata Garcia anaendelea kuwa mchezaji bora wa
Chelsea mpaka sasa. Huyu ndiye mchezaji bora wa ligi ya Uingereza kwa
mwezi wa 10, mwaka 2012. Amekuwa wa 9.
Bastian Schweinsteiger (8)
Bastian Schweinsteiger (8)

Roho ya timu ya Bayern Munchen, akifunga
magoli na kutoa pasi za mwisho za kutosha. Basti kama marafiki zake
wanavyomwita ametengeneza chemistry katika timu ya Bayern hasa katika
sehemu ya kiungo ya timu. Uwezo mkubwa wa kukota aliokuwa nao, pasi kali
‘zenye macho’ , uwezo mkubwa wa kukaba, uwezo mkubwa wa kumiliki mpira,
na mwisho wa yote ni uwezo wake mkubwa wa kupiga mipira iliyokufa
unamfanya awe mchezaji wa kipekee. Schweinsteiger ana nafasi kubwa ya
kuingia kwenye FIFA FIFPro World XI ya mwaka huu. Amekuwa wa 8.
Andres Iniesta (7)
Andres Iniesta (7)

Mchezaji bora wa Ulaya kwa mwaka 2012,
siku zote amekuwa kwenye kiwango bora. Iniesta kwa sasa yupo kwenye
kiwango cha juu cha soka katika maisha yake. Yeye ndio mtu anayeng’aa
zaidi kwenye timu yenye vipaji lukuki ya Spain. Sababu ya Iniesta
kushika namba 7 katika listi hii ni kutokana na makali kupungua kidogo
tangu mashindano ya Ulaya kuisha pia ni kutokana na watu waliopo juu
yake viwango vyao kuongezeka kwa kiasi kikubwa. Kitu ninachoamini ni
kuwa lazima Iniesta atajwe kugombania FIFA Ballon d’Or katika wale watu
watatu wa mwisho.
Stephan El Shaarawy (6)
Stephan El Shaarawy (6)

Mashabiki wake humwita ‘The Pharaoh’ kwa
sababu amezaliwa na wazazi wenye asili ya Misri pale Savona, Italia.
Huyu ndio nguzo ya Milan kwa sasa katika upachikaji mabao baada ya
Zlatan Ibrahimovic kuondoka. Akivaa jezi yenye namba ya mwaka
aliozaliwa, # 92 (1992), na ikiwa ndio kwanza katimiza miaka 20 juzi tu
mwezi October, Firauni huyu amekuwa tishio sana kwa mabeki wa timu
pinzani zinazopambana aidha na Italia ama A.C Milan. Nimempa namba 6 kwa
sababu anastahili.
Zlatan Ibrahimovic (5)
Zlatan Ibrahimovic (5)

Mtaalamu huyu mwenye mkanda mweusi wa
mchezo wa karate amekuwa mkubwa kuliko ligi ambayo anacheza ndani yake.
Tangu kuhama kutoka AC Milan na kutua PSG mambo yamekuwa rahisi sana kwa
Ibracadabra. Kutokana na aina yake ya mchezo na kipaji chake watoto wa
mjini wanakwambia, Ibra sio wa leo wala kesho wakimaanisha, Zlatan
ataendelea kung’aa kwenye medani nzima ya soka kwa kipindi kirefu kidogo
mpaka pale atakapoamua kustaafu. Huyu ndiye mfungaji anayeongoza katika
ligi kuu ya Ufaransa kwa sasa. Tarehe 14 mwezi huu wa 11, 2012, goli la
4 aliloifunga Uingereza linasemekana kuwa goli la karne. Zlatan Sefik
Ibrahimovic ni namba 5.
Radamel Falcao (4)
Radamel Falcao (4)

Ukiwa ni msimu wake wa pili katika ligi
kuu ya Spain, Radamel Falcao ameibuka ghafla na kuwa gumzo katika bara
lote la Ulaya. Falcao ndio mpinzani mwenye nguvu wa Ronaldo na Messi
ambaye alikuwa akinghojewa katika kugombania kiatu cha dhahabu cha ligi
kuu ya Spain. Akiwa tayari ameshinda kombe La UEFA akiwa na Porto ya
Ureno pamoja Athletico Madrid aliko sasa ambako pia majuzi alishinda
UEFA Super Cup pale alipoichabanga Chelsea goli 3 peke yake katika
ushindi wa 4-1, Falcao ameendelea kuwa mchezaji wa kutumainiwa katika
kila timu anayoitumikia. Falcao anastahili nafasi ya 4.
Robin van Persie (3)
Robin van Persie (3)

Huyu ndiye mchezaji bora wa ligi kuu ya
Uingereza kwa msimu uliopita, 2011/12, huku akiwa hana muda mrefu tangu
ajiunge na mashetani wekundu akitokea kwa mahasimu wao wakubwa, Arsenal,
RvP amekuwa ndio nguzo katika mashambulizi ya United msimu huu akiwa
ameifungia goli 8 tayari na pasi za magoli 3 kwenye ligi kuu, van Persie
ameendelea kuwa moja ya nembo za ligi kuu ya Uingereza kwa wakati huu.
Hivi karibuni wakati Sir Alex Ferguson alipochaguliwa kuwa kocha bora wa
mwezi October alimshukuru Robin kwa kutoa mchango mkubwa sana katika
tuzo yake hiyo. Robin van Persie anakuwa wa 3 nyuma ya Ronaldo na Messi.
Cristiano Ronaldo (1)
Cristiano Ronaldo (1)

CR7 kama anavyopenda kujiita. Yeye
kaiteka dunia ndani ya uwanja na nje ya uwanja. Cristiano Ronaldo ni
moja ya wachezaji adimu sana katika kizazi hiki cha leo. Uwezo wake wa
kupasia ‘kamba’ umekua ukiongezeka siku baada ya siku. Ronaldo ndiye
mchezaji anayetawala vichwa vya habari vya magazeti kila kukicha pamoja
na ‘fundi’ mwingine kutoka Italia aitwaye Super Mario Balotelli. Mtupia
mabao huyu ambaye ndio anaongoza magoli katika ligi ya mabingwa Ulaya
msimu huu akiwa na goli 5 katika mechi 4 alizocheza amekuwa akisifika
kwa bidii yake ya kujituma mazoezini na kwenye mechi. Kutokana na yote
haya Cristiano pia anashikilia namba moja pamoja na Leo Messi. Ronaldo
ndiye mchezaji bora wa mwaka huu, 2012 wa Goal.com, mtandao wa soka
wenye heshima kubwa zaidi.
LIONEL Messi (1)
LIONEL Messi (1)

Ameendeelea kuiteka dunia kutokana na
kipaji chake ambacho kinawashangaza wadau wengi wa soka. Huku
akishikilia rekodi ya kufunga magoli mengi duniani katika msimu mmoja,
magoli 73 katika msimu wa 2011/12 na magoli 76 mpaka sasa kwa mwaka huu
akiwa nyuma ya Gerd Muller, urafiki wa Messi na nyavu umezidi
kudumishwa siku baada ya siku ikumbukwe kwamba kila goli analofunga
Messi kwa hivi sasa ni rekodi katika klabu ya Barcelona kwa sababu yeye
ndiye mfungaji bora wa klabu kwa wakati huu. Kwa sasa mchezaji huyu bora
wa dunia yuko katika kiwango sawa na mshindani wake wa karibu wa siku
zote, Cristiano Ronaldo ndio maana wote wamekuwa vinara kwa kushikilia
namba moja.
Oya! Badilisha hiyo picha yako hapo unatutisha.
ReplyDelete