photo NAAZ_zpsd0bbd510copy_zps37715af5.jpg
 photo NAAZ_zpsd0bbd510.jpg
Nafasi Ya Matangazo
> > MJUE MISS TANZANIA HAPPYNESS WATIMANYWA

MJUE MISS TANZANIA HAPPYNESS WATIMANYWA

Posted on Sep 23, 2013 | No Comments




Mrembo kutoka Dodoma, Happyness Watimanywa amechaguliwa kuwa mshindi mpya wa Miss Tanzania 2013 usiku wa kuamkia jana kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam na kukabidhiwa zawadi ya gari aina ya IST na kitita cha Sh8 milioni.
Taji hilo la Miss Tanzania lilikuwa linashikiliwa na Brigitte Alfred na mwaka huu lilikuwa likigombewa na warembo 30, lakini Happyness aliwabwaga warembo wenzake 29 na kushinda taji hilo.
Nafasi ya pili ilikwenda kwa Latifa Mohamed huku nafasi ya tatu ikienda kwa Clara Bayo. Nafasi ya nne na tano zilikwenda kwa Isabel Petty na Lucy Tomeka.  
Tunampongeza Happyness kwa ushindi alioupata na tunaamini Kamati ya Miss Tanzania inayosimamia mashindano hayo itakuwa makini na kumwandalia mazingira mazuri Happyness ili afanye kile Watanzania wanachohitaji kuona kinatendeka katika mashindano ya dunia.Kwa miaka mingi sasa tumekuwa tukifanya vibaya kwenye mashindano ya dunia, ambapo moja ya sababu kubwa ya Tanzania kufanya vibaya ni warembo wetu kupewa maandalizi ya rasharasha.
Katika mashindano mengi ya dunia yaliyopita warembo wa Tanzania walikuwa wakienda kushiriki mashindano hayo wakiwa wamepata maandalizi ya mwezi mmoja hivyo kushiriki katika mashindano hayo makubwa wakiwa hawajapata mbinu mbalimbali za urembo.
Hata hivyo, hivi sasa nafasi ya kufanya maandalizi ya kutosha ipo ambayo ikitumiwa vizuri ni dhahiri mrembo wa Tanzania ataweza kushindana katika kiwango cha juu badala ya kushiriki tu.
Tunasema hivyo kwa sababu tunafahamu mashindano yajayo ya kumtafuta mrembo wa dunia yatafanyika mwezi 2014 hivyo Happyness ana muda mrefu wa kujiandaa kabla hajaiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo ya dunia.
Ni wazi Happyness hatakiwi kulewa umaarufu katika kipindi hiki ambacho macho ya Watanzania zaidi ya milioni 40 yanamwangalia yeye kama mwakilishi wa Tanzania katika mashindano ya dunia.
Anachopaswa kutambua ni kujiepusha na makundi yasiyofaa, ajitunze na kufanya kazi nyingi za kusaidia jamii, ambapo anaweza kurekodi kazi zote za kusaidia jamii anazozifanya na kwenda nazo katika mashindano ya dunia kwa ajili ya kuonyesha kile alichokuwa akifanya nchini mwake baada ya kuchaguliwa kuwa Miss Tanzania.
Tunaamini Happyness ni mrembo mzuri na ndiyo maana amechaguliwa kuwa Miss Tanzania hivyo atanyemelewa na wanaume mbalimbali ambao watataka kumharibia maisha yake kwa hiyo ajichunge asije kuharibikiwa hata kabla hajakanyaga mashindano ya dunia.
Tunasema hivyo kwa sababu tunaona muda alionao Happyness ni mzuri katika kujiandaa na mashindano ya dunia na kusaidia jamii, lakini kama hatajali hayo basi ataona muda uliopo ni mbaya sana na atashindwa kufanya vizuri katika mashindano ya dunia.
Ikumbukwe kwamba siku zote Watanzania wanataka mshindi mwenye sifa na vigezo vya kuiwakilisha vyema Tanzania katika shindano la kumtafuta mrembo wa dunia.Kwa hiyo tunaamini kabisa Happyness analitambua hilo na atatumia vizuri muda alionao katika kujiandaa badala ya kujiingiza katika mambo ambayo hayatamsaidia katika maisha yake.

Tunampongeza Happyness kwa kushinda taji la Miss Tanzania, tunaamini atajitunza na ataisaidia jamii kabla na baada ya mashindano ya dunia, pia tunaamini ataliwakilisha vyema taifa katika mashindano ya dunia na hatajihusisha na vitendo vya kashfa kama walivyowahi kufanya baadhi ya warembo walioshinda taji la Miss Tanzania.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru