photo NAAZ_zpsd0bbd510copy_zps37715af5.jpg
 photo NAAZ_zpsd0bbd510.jpg
Nafasi Ya Matangazo
> Breaking News: Ajali ya Coaster yautikisa mji wa Mbeya…..wengi wahofiwa kupoteza maisha

Breaking News: Ajali ya Coaster yautikisa mji wa Mbeya…..wengi wahofiwa kupoteza maisha

Posted on Jun 5, 2012 | No Comments


Basi la abiria likiwa nyang'anyang'a baada ya ajali hiyo

Mji wa Mbeya na vitongoji vyake ungali ukizizima kufuatia taarifa za ajali mbaya iliyotokea katika eneo la Mzalendo, kilomita kadhaa tu toka mjini kati, na kuhusisha basi dogo la abiria na lori la mizigo.
Taarifa za awali ambazo zilitua kutoka eneo la tukio, zimeeleza kuwa ajali hiyo ilitokana na lori lililokuwa likitokea Tukuyu, kufeli breki zake wakati likiwa linashuka katika kilima cha Igawilo, na kwenda kuligonga basi hilo la abiria ambalo lilikuwa likielekea Tukuyu na Kyela.
Bado taarifa kuhusu idadi ya waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni za kutatanisha. Ingawa taarifa za awali zilidai kuwa ni watu wanne tu ambao walitoka wakiwa wazima katika eneo la tukio, daktari mmoja ambaye tumeongea naye kutoka hospitali ya rufaa ambako majeruhi na miili ya marehemu imepelekwa, ameeleza kuwa wamepokea idadi ya majeruhi ambao ni zaidi ya wanne.
“Sio wanne, tumepokea watu zaidi ya wanne ingawa kwa sasa siwezi kutoa taarifa rasmi kuhusu idadi kamili ya watu ambao tumewapokea kama majeruhi au waliofariki, lakini inaonyesha ilikuwa ajali mbaya maana wapo ambao wamekatika vibaya mno miongoni mwa marehemu. Kwa sasa ni kama shughuli zote za kawaida zimesimama upande wa X-Ray ili kuwasaidia hawa ndugu zetu” alisema daktari huyo ambaye aliomba asitajwe jina.
Daktari huyo ameliambia Jukwaa Huru kuwa, miongoni mwa majeruhi ambao wamekuwa wakipokelewa hapo, wapo ambao wamekuwa wanafariki wakiwa wanapatiwa huduma za dharura, na kuahidi kutoa taarifa rasmi baadae.
Mungu awape mapumziko mema wote waliopoteza maisha katika ajali hiyo na kuwapa ahueni wale waliosalimika lakini wakapata majeraha

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru