UVCCM YAAHIDI KUDHIBITI VITENDO VYA UBABE NA RUSHWA KATIKA UCHAGUZI MKUU HAPO KESHO.
                              Posted on 
                              Oct 22, 2012
                            |
                            
                                  No Comments
                                  

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Martine Shigela akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Dodoma kuhusu maandalizi ya Mkutano Mkuu wa UVCCM. Kulia ni  Mwenyekiti wa Kamati ya habari na mapambo wa maandalizi ya Mkutano huo Cosmas Hinju.  
Na Bashir Nkoromo-Dodoma. 
Wakati Uchaguzi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) umemalizika juzi, huku ukidaiwa kugubikwa na ubabe na rushwa, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) umejitapa kwamba, utahakikisha vitendo hivyo havitokei katika uchaguzi wake mkuu utakaofanyika kesho mjini Dodoma.
UVCCM imeapa kwamba
 mgombea au hata mpambe atakayebainika kujihusisha na kampeni zilizo nje
 ya utaratibu na kanuni za UVCCM au kujihusisha na vitendo vya rushwa, atashughulikiwa mara moja ikiwemo kuchukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Martine Shigela amesema, wameweka mtandao mpana wa kutosha kukabiliana na aina yoyote ya ukiukwaji wa tararibu, kanuni na sheria za uchaguzi wa UVCCM.
Shigela amesema, taratibu za mkutano mkuu utakao ambatana na uchaguzi huo, zimekamilika na utafanyika kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere, uliopo Chuo Cha Mipango ambako ndiko ulikofanyika pia ule wa UWT.
Amesema, mkutano unaanza kesho, Oktoba 23, na utafunguliwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
Katika nafasi ya Mwenyekiti wanachuana wagombea watatu, Lulu Mushamu Abdallah,  Sadifu Juma Khamis na Rashid Simai Msaraka wakati katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Ally Salum Hapi, Paul Christian Makonda na Mboni Mohamed Mhita.
Nafasi zingine ni, Halmashauri Kuu ya Taifa Viti sita (Bara) wagombea 40, Viti Vinne (Zanzibar) wagombea 22, Nafasi ya Baraza Kuu la Vijana Taifa Viti vitano Bara wagombea 39 na viti vitano Zanzibar wagombea 14,  Uwakilishi Wazazi Taifa na Jumuia ya Wanawake Tanzania (UWT) wagombea 16 kila nafasi.
 
 
 
 
 
 
 
 
