photo NAAZ_zpsd0bbd510copy_zps37715af5.jpg
 photo NAAZ_zpsd0bbd510.jpg
Nafasi Ya Matangazo
> > KESI YA EPA WALIPA FIDIA KUKWEPA KIFUNGO

KESI YA EPA WALIPA FIDIA KUKWEPA KIFUNGO

Posted on Nov 26, 2012 | No Comments


WAFANYAKAZI watatu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ester Komu, Iman Mwakosya  na Sophia Kalika wamelipa fidia ya Sh5 milioni na kuepuka kifungo cha miaka mitatu jela.
Jopo la mahakimu watatu  waliokuwa wakiisikiliza kesi ya wizi wa Sh3.8 bilioni za EPA linaloongozwa na Jaji Samuel  Kalua, Jaji Beatrice Mutungi na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Ilvin Mugeta, katika hukumu yao waliyoisoma juzi  waliwahukumu wafanyakazi hao kifungo cha miaka mitatu jela ama kulipa fidia ya Sh5 milioni.
Baada ya kumalizika kusomwa kwa hukumu hiyo, Ester Komu alifanikiwa kulipa fidia ya Sh5 milioni  na kuachiwa huru wakati wenzake Iman na Kalika walipelekwa gereza la Segerea hadi jana walipokamilisha  maamuzi ya  hukumu  hiyo kwa kulipa Sh5 milioni  na kuachiwa huru.
Mbali na watuhumiwa hao, wengine waliohukumiwa katika hukumu  hiyo iliyosomwa juzi na Hakimu Mugeta ni  Kada  wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rajabu Maranda  ambaye alihukumiwa kifungo  cha miaka miwili  jela na kuamuriwa kurejesha Sh616.4 milioni.
Binamu yake Farijala Hussein naye alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na kuamriwa kurejesha Sh81 milioni na  mfanyabiashara Ajay Soman akihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela sawa na Maranda lakini yeye akiamriwa arejeshe Sh400 milioni.
Kabla ya kusoma  hukumu hiyo iliyochukua zaidi ya saa 4,  Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Ilvin Mugeta alisema washtakiwa wote wamepatikana na hatia  katika makosa ya kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kuwasilisha nyaraka za uongo BoT na kuisababishia Serikali hasara ya Sh3.8 bilioni.
Hakimu Mugeta alisema wafanyakazi wa BoT hawatahusika katika mpango wa kurejesha fedha kwa sababu ushahidi unaonyesha hawakunufaika na chochote katika wizi huo.
Alisema Maranda, Farijala na Soman wana ushahidi ambao unaonyesha kuwa walijinufaisha na fedha hizo hivyo wanatakiwa kuzirejesha na kwamba iwapo watashindwa kutekeleza amri hiyo, mali zao zikamatwe.
Wakili wa Serikali, Shedrack Kimaro awali aliiambia mahakama kuwa Maranda na Farijala walikwisha tiwa hatiani  kwa makosa ya aina hiyo  katika kesi namba 1161/2008 na 1163/2008 na kwamba hawana kumbukumbu ya kutenda  makosa ya uhalifu kwa washtakiwa Ajay, Iman, Ester na Sophia.
Kimaro alisema kutokana na aina ya makosa  na fedha za umma aliomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho  kwa wahalifu wengine  wenye tabia kama hiyo.
Pia aliiomba mahakama itumie mamlaka yake iliyopo katika kifungu cha 348 (1) ama cha 358 (1) cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai sura ya 20, kuwaamuru washtakiwa hao kurejesha fedha wanazodaiwa kuiba BoT kama walivyojipatia.
Magafu akijibu hoja hizo, alidai kuwa Maranda na Farijala wasipewe adhabu kali kwa sababu kesi hizo zilifunguliwa wakati mmoja  na kwamba tofauti ilikuwa ni majina ya kampuni na kuwa aliyestahili kupewa onyo kama hilo ni yule aliyefanya uhalifu na akarudia tena.
Maranda na binamu yake Farijala  Hussein tayari wanatumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa Sh1.8 bilioni za Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) iliyopo BoT na kuamuriwa kurejesha kiasi hicho cha fedha.


Licha ya kutumikia kifungo hicho, pia wanatumikia kifungo kingine cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana  na hatia katika kesi ya tuhuma za kuchota Sh2.2 bilioni  za EPA.
Hukumu hiyo ya tuhuma za wizi wa Sh3.8 bilioni za Epa, ilisomwa na  jopo la mahakimu watatu lililoongozwa na Jaji Samuel Kalua, Jaji Beatrice Mutungi na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Ilvin Mugeta.
Katika kesi hiyo, washtakiwa hao kwa pamoja  wanadaiwa kuwa kati ya Januari 18 na Novemba 3,2005, kinyume na kifungu namba 384 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 ya sheria, walikula njama ya wizi wa fedha kutoka BoT.
Pia wanadaiwa kughushi hati ya usajili yenye namba 46218 na kuonyesha kuwa zimesainiwa na kutolewa na Msajili wa Biashara kwa Kampuni ya Mibale Farm wakati si kweli.
Wanaendelea kudaiwa kujipatia Sh3.8 bilioni baada ya kudanganya kuwa kampuni yao ya Mibale Farm imepewa deni na Kampuni ya Textile Mills Ltd ya nchini India.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru