photo NAAZ_zpsd0bbd510copy_zps37715af5.jpg
 photo NAAZ_zpsd0bbd510.jpg
Nafasi Ya Matangazo
> > RIDHIWAN, LOWASSA WAELEZEA UTAJIRI WAO

RIDHIWAN, LOWASSA WAELEZEA UTAJIRI WAO

Posted on Nov 26, 2012 | No Comments

Ridhiwan Kikwete 
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwan wamezungumzia tuhuma ambazo zimekuwa zikielekezwa kwao kwamba wanamiliki rasilimali zenye thamani ya mabilioni ya shilingi.
Lowassa kwa upande wake amekuwa akidaiwa kuwa tajiri anayemiliki kampuni kubwa za kibiashara na kumekuwa na taarifa kwamba ana ukwasi ambao vyanzo vyake vinatia shaka na siyo rahisi kuvitolea maelezo.
Kwa upande wake Ridhiwan naye amekuwa akidaiwa kuwa na utajiri mkubwa na amekuwa akihusishwa na biashara za kampuni za kusafirisha mafuta ambayo hupelekwa kwenye migodi, umiliki wa hoteli na majengo kadhaa ya kifahari.
Wote wawili wamekuwa wakidaiwa kwamba baadhi ya mali zao wamekuwa wakiziendesha chini ya kivuli cha wafanyabiashara wengine wakubwa nchini ili kukwepa kuhojiwa walikotoa utajiri huo, taarifa ambazo hata hivyo imekuwa vigumu kuzithibitisha.
Hata hivyo jana kwa nyakati na mazingira tofauti, Lowassa na Ridhiwan walijitokeza hadharani na kukanusha madai kwamba wao ni matajiri wa kupindukia.
Lowassa kwa upande wake akiwa mjini Mbeya alisema yeye siyo tajiri kama ambavyo imekuwa ikidaiwa lakini wakati huohuo akasema “sijafilisika”.
“Wengi wanasema kuwa mimi ni tajiri siyo kweli, lakini sijafilisika kutokana na kuchangia makanisa kwani nina marafiki wengi ambao wananisaidia katika kuchangia makanisa nao pia hawajafilisika,”alisema Lowassa.
Lowasa alitoa kauli hiyo alipokuwa akiendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa hosteli ya wanachuo wanawake ambao ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Theofilo Kisanji cha mkoani Mbeya, kinachomilikiwa na Kanisa la Moraviani Tanzania, Jimbo la Kusini Magharibi.
Kiongozi huyo ambaye alichangia kaisi cha Sh25 milioni, alisema kila mtu ana wajibu wa kuchangia elimu na kwamba mwanamke anapaswa kutazamwa kwa karibu zaidi kwani ndiye anayebeba jukumu kubwa la kutunza familia.
Kwa upande wake Ridhiwan alisema: “Ikiwa mimi ni tajiri wa kiasi kinachosemwa, basi mimi ninamzidi Bakhressa (Said Salim, mfanyabiashara maarufu Afrika Mashariki), maana nimepewa kila hoteli hapa mjini, kampuni za mafuta na kila biashara kubwa inayoanzishwa hapa mjini ni ya Ridhiwan”.
Said Salim Bakhressa ni mfanyabiashara ambaye anatajwa kuwa tajiri kuliko wote nchini na anashika nafasi ya pili katika nchi za Afrika Mashariki na Kati, huku akiwa miongoni mwa wafanyabiashara 10 wanaonyemelea kuingia katika nafasi za juu za utajiri Afrika.
Hata hivyo Ridhiwan ambaye hivi karibuni alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), aliongeza: “Ninaweza kuwa nafanya biashara moja au mbili, lakini siwezi kuwa mmiliki kiasi chote hicho cha mali.
Mtoto huyo wa Rais Kikwete alikuwa akijibu tuhuma kwamba magari yake kumi ya kusafirisha mafuta yamekamatwa na kuzuiwa katika mpaka wa Kenya na Tanzania, Namanga mkoani Arusha kutokana na kukwepa kodi, taarifa ambayo aliikanusha.

Maelezo ya Ridhiwan

Maelezo ya Ridhiwan yamekua wakati kukiwa na taarifa kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inayashikilia malori mapya 10 ya kubebea mafuta yanayodaiwa kuwa ni yake, yanayodaiwa kuingizwa nchini.
Hata hivyo Ridhiwan alikanusha kuhusika na biashara ya mafuta akisema: “Ili kuwa na utajiri unaotajwa kwangu lazima niwe nimekopa benki au nimeiba, sasa wale wanaonituhumu wasema nimekopa benki gani na kama nimeiba basi wajitokeze watu kulalamika kuhusu wizi nilioufanya”.
Mtoto huyo wa Rais Kikwete, alisema kumekuwa na kile alichokiita uzushi wa ajabu na kwamba hajui wanaozusha mambo hayo wana malengo gani. “Wameanza kusema kwamba nauza dawa za kulevya jambo ambalo siyo kweli, mie sifanyi biashara za aina hiyo, kama kuna jambo jingine tuunguze lakini hilo ni uzushi tu,”alisisitiza.
Habari zilizopatikana jana, zilidai malori hayo mapya yanashikiliwa na TRA kituo cha mpakani cha Namanga kwa madai ya kuwapo “utata” wa malipo ya ushuru wa forodha.
Taarifa za kuzuiwa kwa malori hayo zilianza kuzagaa nchini wiki mbili zilizopita kupitia mitandao ya kijamii ukiwamo mtandao maarufu wa Jamii Forums (JF).
Kulingana na taarifa hizo, watu walioshuhudia magari hayo walidai yalikuwa zaidi ya 70 yakitokea Kenya kutengenezwa bodi huku wengine wakidai yalikuwa ni mapya.
Baadaye taarifa hiyo ilibadilika na kusema kwamba magari hayo yalikuwa 20 na kwamba ni malori 10 tu ndiyo yaliyolipiwa ushuru na kuingia nchini, lakini malori mengine 10 yalikuwa yakiendelea kushikiliwa kutokana na ukwepaji wa kodi.
“Ni kweli hayo magari ni ya huyo bwana mkubwa na yalikuwa 20, lakini 10 yalilipwa ushuru halali”alidai ofisa mmoja wa TRA kituo cha Namanga.
Ridhiwan alisema kuthibitisha kwamba tuhuma hizo ni za uwongo haiwezekani mtu anayetajwa kuwa tajiri kama yeye ashindwe kulipia ushuru wa malori kumi. “Uwongo mwingine huo, kama kweli ningekuwa nina utajiri wote huo, nishindwe kulipia ushuru wa malori kumi tu! Ndo maana nasema ni uwongo tena wa kutunga,”alisema.
Kaimu Meneja wa TRA Arusha, Theresia Mponeja alipulizwa na gazeti hili wiki iliyopita alikanusha kuzuiwa kwa malori hayo na kwamba hakuna taarifa hizo.
Lowassa na elimu
Katika hafla ya jana mjini Mbeya, Lowassa aliendelea kuipigia chapuo elimu akisema: “Ni vizuri vijana wetu wakazingatia elimu kwani bila elimu watashindwa kuhimili ushindani wa ajira katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.”

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru