photo NAAZ_zpsd0bbd510copy_zps37715af5.jpg
 photo NAAZ_zpsd0bbd510.jpg
Nafasi Ya Matangazo
> > RUFAA YA SERIKALI DHIDI YA ACP ZOMBE KUANZA KUSIKILIZWA

RUFAA YA SERIKALI DHIDI YA ACP ZOMBE KUANZA KUSIKILIZWA

Posted on Nov 19, 2012 | No Comments



JOPO la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani nchini litasikiliza rufaa ya Serikali dhidi ya hukumu iliyompa ushindi aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoa wa Dar es Salaam, ACP Abdallah Zombe pamoja na wenzake, Jamiipress imebaini.
Zombe na wenzake waliachiwa huru Agosti 17, 2009 na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, dhidi ya ya makosa ya mauaji ya kukusudia yaliyokuwa yakiwakabili.
Watuhumiwa hao wanarejea tena mahakamani, ikiwa imepita miaka 3 na miezi 3 tangu hukumu hiyo ya kuwaachia huru ilipotolewa na aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu wakati huo, Salum Massati. Hivi sasa Massati ni Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Habari ambazo gazeti hili limezipata kutoka Mahakama ya Rufaa na kuthibitishwa na baadhi ya maofisa ndani ya mahakama hiyo zinasema rufaa hiyo itaanza kusikilizwa mwezi ujao.
Mwananchi limefanikiwa kuiona ratiba ya vikao vya Mahakama ya Rufani ambayo inaonyesha kuwa rufaa dhidi ya Zombe na wenzake itaanza kusikilizwa tarehe 11Desemba mwaka huu saa 3:00 asubuhi na Majaji William Mandia, Nathalia Kimaro na Katherine Oriyo.
Watuhumiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kukusudia ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro na dereva wa teksi wa Manzese jijini Dar es Salaam.
Siku chache baada ya kuachiwa huru, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alikata rufaa Mahakama ya Rufani, akipinga hukumu ya Mahakama Kuu, akidai kuwa Jaji Salum Massati aliyesikiliza kesi hiyuo alikosea kuwaachia huru washtakiwa hao.
Katika hukumu yake, Jaji Massati alisema kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa hapo bila kuacha mashaka.
Pia Jaji Massati alisema kuwa amebaini kuwa wauaji halisi hawajafikishwa mahakamani na kwamba kutokana na kutokuwepo kwao mahakami, mashtaka dhidi ya washtakwa waliokuwapo mahakamani hayawezi kutengenezeka, hivyo akaiagiza Jamhuri kuwasaka na kuwafikisha mahakamani wauaji halisi.

Hoja za DPP
DPP katika rufaa yake namba 254/2009, iliyofunguliwa Oktoba 6, 2009, amebainisha sababu 11 ambazo zimemfanya apinge hukumu hiyo, akidai kwamba kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, washtakiwa wote walikuwa na hatia.
Katika hoja hizo, DPP amedokeza kile anachokiita upungufu katika hukumu hiyo, kwa kila mshtakiwa.
DPP anadai kuwa jaji Massati alipotoka, alishindwa kutafsiri sheria na kanuni mbalimbali zinazohusu mashtaka ya jinai na kwamba alijichanganya sana katika hukumu hiyo.
Anadai na kueleza kushangaa Jaji kushindwa kuwatia hatia washtakiwa wote licha ya kwamba kulikuwa na ushahidi wa dhahiri na wa kimazingira wa kutosha kuwatia hatiani.

DPP anadai kuwa Jaji alikosea kisheria na alipotoka kwa kiwango kikubwa katika kujenga na kutafsiri ushirika katika kutenda kosa na kwamba katika mazingira ya kesi hiyo jaji alijipotosha katika kutafsiri na kutumia kanuni zinazoongoza nia ya pamoja.
Pia DPP anadai kuwa Jaji alikosea sana kisheria na kiukweli, katika kujenga na kutafsiri maana ya maelezo ya kukiri, jambo ambalo lilimfanya afikie hitimisho potofu.
DPP anaendelea kudai kuwa Jaji pia alishindwa kutafsiri na kutumia kanuni ya kumtia hatiani mtu anayepatikana na kitu kilichoibiwa karibuni (doctrine of recent possession) dhidi ya mshtakiwa wa tatu (ASP Makelle).
Kwa mujibu wa ushahidi ulitolewa mahakamani na upande wa mashtaka, Makelle ndiye aliyekuwa na mkoba wa pesa wa marehemu walipofika katika kituo cha polisi Urafiki.
DPP anaendelea kudai kuwa alikosea kumwachia mshtakiwa wa tano (WP Jane Andrew) na mshtakiwa wa 10 Abineth Saro, ambao walishindwa kueleza mahalai walikokuwa wakati wa tukio.
Anadai kuwa alikosea kuwatokuwatia hatiani washtakiwa hao licha ya kuwepo kwa ushahidi wa kimazingira, pamoja na mshtakiwa wa saba na wa tisa.
Pia DPP anadai kuwa Jaji alikosea kuchambua ushahidi na hivyo  alijichanganya katika hukumu yake.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru