KAMPUNI ZA SIMU ZATUMIA SH17 BIL KUJITANGAZA
Posted on
Mar 23, 2013
|
No Comments
Dar es Salaam. Kampuni za mitandao ya simu za mikononi nchini, zimetajwa kuongoza katika kutangaza biashara zao kwenye vyombo vya habari, katika robo ya mwisho ya mwaka uliopita.
Takwimu zilizotolewa na kampuni inayoongoza katika kusimamia na kufuatilia mwenendo wa vyombo vya habari nchini, Push Observer, Kampuni ya Airtel ndiyo inayoshika nafasi ya kwanza kwa kutangaza matangazo mengi katika vyombo hivyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Push Observer, Ruby Alcantara, alisema kampuni ya pili ni Tigo inayofuatiwa na Vodacom Tanzani hatimaye, Zantel inayoshika nafasi ya nne.
Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) inashika nafasi ya tano ikifuatiwa na Pepsi, Star Times, Coca Cola, SBL na Twaweza katika nafasi ya 10.
Alcantara alisema “takwimu hizo ni za uhakika na zimetokana na kumbukumbu zilizokusanywa kwa kutumia vifaa vya kisasa.”
Alisema fedha zilizotumiwa na kampuni zote 20 bora katika kutangaza biashara ni zaidi ya Sh17 bilioni .
Hata hivyo taarifa hiyo, haija ainisha gharama halisi ya kila kampuni zilizotumia katika kutangaza bidhaa zake.
“ Hatuwezi kuweka bayani ni kiasi gani cha fedha kimetumika katika zoezi hili, ni vigumu kufanya hivyo, lakini takwimu zetu ni sahihi kwa sababu tumetumia vifaa vya kisasa katika kuzikusanya,” alisema.
Alisema kuwa vyombo vya habari vinavyofaidika kwa kupata matangazo mengi ni redio na televisheni.
Alisema kampuni yake itakuwa inatoa taarifa kuhusu watangazaji bora wa kwenye vyombo vya habari kila baada ya miezi mitatu.
Ripoti robo ya kwanza ya mwaka huu inatarajiwa kutolewa mwanzani mwa mwezi ujao.