Rais Xi Jinping amepokelewa kwa shangwe na mizinga 21 alipowasili Dar-es-salaam Tanzania kuanza ziara ya nchi tatu za Afrika.
Rais Xi aliingia Dar-es-salaam akitokea Moscow ambako ndiko alikoanza safari yake ya kwanza katika nchi za nje tangu kutawazwa rasmi kuwa rais hivi karibuni.
Safari yake barani Afrika inaonesha umuhimu wa Afrika kwa Uchina, kuwa ni chanzo cha madini na nishati na piya soko kwa bidhaa za Uchina.
Rais wa Uchina anatarajiwa kutoa hotuba muhimu Jumatatu kuhusu uhusiano baina ya Uchina na Afrika, na anatarajiwa kutia saini mikataba karibu 20 ya maendeleo na utamaduni baina ya Uchina na Tanzania.
Anatarajiwa kupooza maoni kwamba Uchina inaingia Afrika ili kunufaika na madini tu ya bara hilo.
Uchina ni ya pili katika uwekezaji nchini Tanzania, baada ya Uingereza.
Bwana Xi piya anapanga kuzuru Afrika Kusini ambako viongozi wa mataifa ya uchumi unaochipukia, BRICS, watakutana Jumaane mjini Durban.
Baada ya hapo anapanga kuzuru Congo.