JANUARI MAKAMBA AWATAKA WANABUMBULI KUHUDHURIA MKUTANO WA MAENDELEO YA BUMBULI
Posted on
Jul 8, 2012
|
No Comments
MBUNGE wa Bumbuli Januari Makamba (CCM). amewataka Wanabumbuli kuhudhuria mkutano wa kujadili maendeleo ya Jimbo hilo utakaofanyika Augasti 4 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Kauli hiyo aliitoa jijini leo, wakati alipokuwa akizungumzia na wandishi wa habari kuhusu mpango wa mageuzi ya uchumi katika jimbo hilo.
Alisema lengo la mkutano huo ni kuzindua Shirika la maendeleo lisilotengeneza faida, likiwa la kukuza uchumi na kuchochea maendeleo ya Jimbo hilo.
Makamba alisema shabaha ya mkutano huo ni kuunganisha jitihada za wenyeji wa Bumbuli, wafanyabiashara na taasisi za hapa nchini, wawekezaji kutoka nje katika kufanikisha mageuzi ya kijamii na kiuchumi.
Aidha,ukiachilia mbali mkutano huo, makamba alisema kuna mpango wa kuikwamua Bumbuli kupitia uwekezaji katika jamii ambapo miradi mitano imekwishaanzishwa.
Makamba alisema mpango wa kwanza ni kuongeza pato la wakulima wa jimbo hilo kutokana na mazao wanayovuna kwa kuboresha mbinu za kuhifadhi mazao hayo ili yapate thamani zaidi.
Vilevile kuwavutia wawekezaji kujenga taasis au shule itakayokuwa na wanafunzi, waalimu na wafanyakazi wengine watakaotumia bidhaa zinazozalishwa katika jimbo hilo, hivyo kutengeneza ajira na fursa za kujiongezea kipato kwa wananchi.
Akizungumzia elimu, Makamba alisema wamebuni mpango utakaosaidia kunyanyua ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne ambao unaanza mwaka huu.
“Tutaanzisha makambi ya kuwatayarisha vijana hao wa kidato cha nne kwa kuwapa mazoezi ya kujibu mitihani ya tangu mwaka 1984”alisema Makamba
Alisema mpango huo, utajikita katika kutoa motisha kwa walimu watakaofanya vizuri huku wanafunzi nao halkadhalika watakaofanya vizuri watapatiwa zawadi.
