photo NAAZ_zpsd0bbd510copy_zps37715af5.jpg
 photo NAAZ_zpsd0bbd510.jpg
Nafasi Ya Matangazo
> > SERIKALI YAWAFIKISHA MAHAKAMANI WATUMISHI 231 KWA UBADHIRIFU

SERIKALI YAWAFIKISHA MAHAKAMANI WATUMISHI 231 KWA UBADHIRIFU

Posted on Jul 13, 2012 | No Comments

Serikali imewafikisha mahakamani watumishi wa wake 231 kutokana na tuhuma za ubadhirifu na wizi wa fedha za Umma kati ya Desemba 2008 na mwezi Machi mwaka huu, bunge limeambiwa.
 Akijibu swali leo katika mkutano wa bunge unaoendelea mjini Dodoma, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Aggrey Mwanri ameliambia bunge kuwa serikali imekuwa ikiwachukulia hatua za kinidhamu watendaji wake ambao wamethibitika kuhusika na wizi au ubadhirifu wa fedha za Umma katika maeneo mbalimbali nchini.
Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuwasimamisha kazi watumishi hao ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za nidhamu au jinai dhidi yao, na kuwafungulia mashtaka ya jinai mahakamani watumishi wenye kutuhumiwa kwa makosa ya jinai.
Aidha, Naibu waziri huyo alisema serikali imekuwa ikirekebisha sheria zake mbalimbali ikiwemo kuzibadili sheria hizo pale inapoonekana inafaa ili kukidhi malengo yaliokusudiwa kwa manufaa ya Umma.
 Akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Esther Bulaya (Viti Maalum) aliyetaka kujua ni kwa nini serikali huwahamisha watendaji wabadhirifu badala ya kuwafukuza kazi, Naibu Waziri huyo alisema kuwa mtendaji yeyote anayebainika kufanya ubadhirifu anapaswa kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria na kumtaka mbunge kutoa taarifa sehemu husika iwapo anazo taarifa za mtumishi mbadhirifu aliyehamishwa badala ya kushtakiwa.
Alisema Wizara yake tayari imewasimamisha baadhi ya wakurugenzi wake kutokana na tuhuma za ubadhirifu na kuongeza kuwa hivi karibuni Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa George Mkuchika alitaja majina ya viongozi 33 waliosimamishwa kazi kutokana na tuhuma za wizi wa fedha za Umma.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru