WANANCHI WA ARUSHA WAGOMEA MRADI WA BENKI YA DUNIA
Posted on
Jul 17, 2012
|
No Comments
MRADI wa ujenzi dampo la kisasa wenye thamani ya shilingi bilioni 3 unofadhiliwa na benki ya dunia katika jiji la Arusha, upo hatari kuyeyuka kufuatia wananchi wa kata ya Muriet manispaa ya Arusha kugoma kupisha eneo la mradi huo licha ya kulipwa stahili zao
Aidha mradi huo ambao ulikuwa uanze tangu april mwaka jana umeshindwa kuendelea kutokana na mvutano mkali ulipo kati ya wananchi zaidi ya 200 na manispaa ya jiji la Arusha ,ambapo wananchi hao wameilalamikia manispaa hiyo kwa kushindwa kuwalipa fidia ya maeneo yao waliyoyaendeleza ,huku manispaa hiyo ikidai imeshawalipa.
Akizungumzia swala hilo , Mkurugenzi wa manispaa ya Arusha, Bw Estomih Changa’h alikiri wananchi hao kuwa kikwazo cha kuanza kwa mradi huo huku akidai kuwa wafadhili wa mradi huo ambao tayari walionyesha nia na kuja na kupima katika eneo hilo wameanza kukata tamaa.
Alifafanua kuwa , baada ya kufanya tathmini ya awali mwaka jana walibaini kuwa wananchi 42 ndio waliopo ndani ya eneo husika la mradi ,hivyo manispaa ya Arusha ilifanya tathimin na kukubali kuwalipa kiasi cha shilingi milioni 252 kama fidia ya makazi yao.
‘’tulipofanya tathimini ya makazi yao tulikubaliana kuwalipa wakazi hao 42,na kila mtu alipigwa picha akiwa amesimama mbele ya eneo ama nyumba yake,sasa tunasikitika sana kuona wakiendelea kunga’ng’ania huku kundi lingine la watu zaidi ya 200 wakiibuka kutaka nao walipwe fidia’’alisema Bw Chang’ah
Alisisitiza kuwa,tayari manispaa imeshawalipa wananchi 33 kati ya 42 kwa kiwango tofauti na kubaki wananchi tisa tu ambao walikuja kurubuniwa na kugomea malipo hayo.
Aliongeza kuwa, wananchi hao wamekuwa wakifika katika ofisi ya manispaa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha kudai fidia zao ambapo wamekuwa wakijaribu kuwaelewesha na uendesha vikao kadhaa, lakini wamekuwa wagumu kuelewa .
Mwenyekiti wa kamati ya waathirika hao ,Jackson Japhet alisema kuwa, wao wanachotaka ni kutaka kulipwa fidia stahili ya makazi yao kwani wengi wa wananchi wamekuwa wakiishi hapo muda mrefu na wamekuwa na makazi ya kudumu ,hivyo ni ngumu sana wao kuondoka katika eneo hilo.
Wakizungumza katika kikao cha hadhara katika eneo hilo la Muriet mwishoni mwa wiki, wameazimia kwenda mahakamani kusimamisha uanzishaji wa mradi huo hadi manispaa hiyo itakapofanya tathimini upya kwa kuwashirikisha wananchi hao na kuwalipa fidia stahili bila kuwapunja.
