DK. MWAKYEMBE AZINDUA USAFIRI WA TRENI JIJINI DAR LEO.
Posted on
Oct 29, 2012
|
No Comments
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe (katikati) akiwasili kupanda treni kituo cha Tazara kuelekea mjini kufanya uzinduzi.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ndani ya treni.
Ukaguzi wa tiketi ndani ya treni
Tiketi zikikatwa ndani ya treni.
hapa ndipo wanapotangaza na kutoa burudani ndani ya treni.
Chombo kikichanja mbuga kuelekea mjini.
Ujenzi wa vituo maalumu vya treni unaendelea.
Na Joachim Mushi, Thehabari.com
Usafiri
wa kutumia treni jijini Dar es Salaam kutokea eneo la Ubungo Maziwa
kuelekea katikati ya Jiji la Dar es Salaam (Stesheni ya Treni) umeanza
leo. Treni ya kwanza imeondoka Ubungo majira ya saa 12:00 asubuhi
kuelekea katikati ya jiji, ambapo kwa mujibu wa maofisa wa Shirika la
Reli Tanzania (TRC) imetumia wastani wa dakika 30 kufika katikati ya
jiji.
Treni
ilioanza kazi leo iliyokuwa na injini mbili (vichwa vya traini) moja
ikiwa imefungwa nyuma na nyingine mbele huku ikiwa na mabehewa sita,
yaani matano ya abiria wa kawaida (watu wazima) na moja likiwa ni
maalumu kwa ajili ya kubeba wanafunzi. Abiria mmoja ni sh. 400 kwa tripu
huku wanafunzi wakitakiwa kulipa sh. 100 kwa kila mmoja.
Waziri
wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ndiye aliyezindua usafiri wa leo
ambao ni wamajaribio, akiwa pamoja na viongozi waandamizi kutoka TRC,
Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), TAZARA pamoja na
Polisi Kitengo cha Reli. Treni hiyo pia imezinduliwa pamoja na treni ya
TAZARA ambayo itafanya kazi kama ya Ubungo, lakini yenyewe ikianzia eneo
la TAZARA kuelekea Mwakanga.
Akizungumza
mara baada ya ufunguzi huo Waziri Mwakyembe alisema atahakikisha treni
hiyo inaendelea kufanya kazi ili kuwasaidia kiusafiri wananchi wa Dar es
Salaam ambao wamekuwa wakisumbuliwa na kero ya usafiri hasa kwa foleni,
ambapo utumia muda mrefu njiani kuingia na kutoka jijini.
Alisema
jumla ya mabehewa ya treni 14 pamoja na injini mbili zimekarabatiwa na
mafundi wazalendo nchini, ambayo ndiyo yatakayokuwa yakifanya kazi ya
kusafirisha abiria kuingia na kutoka jijini kila asubuhi na jioni.
Alisema kwa sasa inafanya treni moja kwa majaribio lakini baada ya
uzinduzi mkubwa zitafanya kazi treni mbili, na zitakuwa zikipishana
njiani moja ikirudi na nyingine ikienda.
Akifafanua
zaidi alisema kitendo cha mafundi wazalendo kufanya ukarabati kwa
mabehewa na injini kimeokoa kiasi kikubwa cha fedha za umma kwani
ukarabati wote umetumia sh. bilioni 2.1 tu, ilhali kama Serikali
ingelazimika kukodi injini gharama ingekuwa kubwa zaidi kwani bei ya
kukodi injini moja ya treni ni sh. milioni moja kwa siku.
Hata
hivyoDk. Mwakyembe amewataka Watanzania hasa abiria kuwa wavumilivu kwa
upungufu utakaojitokeza kwa safari za mwanzo kwani bado wanaendelea
kufanya marekebisho kadhaa, lakini baada ya muda mambo yatakaa sawa.
Mwandishi wa habari hizi alikuwa ni mmoja wa wasafiri walioizindua treni
hiyo leo.
Awali
akizungumza mmoja wa viongozi waandamizi wa TRC, alisema treni hiyo
itafanya kazi kila siku isipokuwa kwa siku za jumapili na siku kuu na
itaanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa sita mchana na kupumzika hadi saa
9:00 za jioni, itakapoendelea tena na safari zake hadi majira ya saa nne
usiku.
Uchunguzi
uliofanywa na muandishi wa habari hizi umebaini kuwa behewa moja la
treni linauwezo wa kuchukua abiria 66 wakiwa wamekaa, lina milango
minne, feni, taa, muziki/redio, pamoja na mikanda maalumu ya kujishikia
kwa abiria ambao watakuwa wamesimama.
Aidha
mabehewa yote yana madirisha ya kutosha kuingiza na kutoa hewa ya
kutosha. Treni ilioanza kazi leo, ikitokea Ubungo ilikuwa ikisimama
vituo vya eneo la Mwananchi (relini), Tabata Relini, Buguruni Miamani,
Tazara, Kariakoo Gerezani (Kamata), na mwisho Kituo Kikuu cha Treni
kilichopo jirani na Kituo cha Polisi Kati (Katikati ya Jiji).
*Imeandaliwa na mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com)