JE OBAMA ATAPUUZA AFRIKA TENA?.
Posted on
Nov 28, 2012
|
No Comments
Kuna baadhi ya
wenyeji wa bara hili waliotegemea mengi zaidi kutoka kwa mwanawe mtu
aliyekuwa akichunga mbuzi huko Magharibi mwa Kenya
Lakini Rais Barack Obama, katika muhula wake wa
kwanza, alizuru Afrika mara moja tu, tena kama mpita njia, na kusema
wazi kwamba hangekuwa anajihusisha kupita kiasi na maswala ya Afrika.
“Hatima ya Afrika iko mikononi mwa
Waafrika wenyewe,” alisema huko Ghana, katika hotuba iliyodhihirisha
wazi kwamba ushawishi wa Marekani unapungua katika bara ambalo sasa
linafanya biashara zaidi na Uchina kuliko Marekani.
Kwa hivyo, ni mabadiliko yapi yatakayokuwepo katika muhula wa pili?
“Kama Kenya itafanya uchaguzi huru, basi Obama ataitembelea nchi hiyo.''
Swala hili la yeye kutokuwa na muda na Afrika,
kwa sababu ya matukio mengine, halikutiwa mkazo katika uchaguzi
ulioangazia maswala nyeti nchini Marekani na harakati za mapinduzi
katika nchi za Kiarabu.
Akitoa hotuba yake baada ya kushinda, Bwana
Obama aligusia tu “,muongo wa vita” na “watu walioko katika nchi za
mbali… wanaoweka maisha yao hatarini ili tu kujadili masuala muhimu, na
kupata nafasi, kama sisi, kupiga kura kama sisi tulivyopiga leo”
Hakuna “Kanuni za Obama”
Katika muhula wa kwanza, maswala yalilenga
mizozo mikubwa iliyokuwa Ivory Coast, Somalia, Sudan and Sudan Kusini,
na hata uchaguzi uliofanywa Zambia.
Kuna uwezekano kwamba mwanzo wa muhula wa pili
atajishughulisha na masuala kama hayo: mikakati ya kimataifa kuwaondoa
waasi wenye uhusiano na Al-Qaeda kutoka Mali kaskazini – kwa kutumia
nguvu au mazungumzo, au yote mawili – na juhudi kuhakikisha kuwa
Zimbabwe na Kenya hawatakuwa tena na michafuko baada ya uchaguzi,
iliyoharibu chaguzi zao zilizopita.
Hadi sasa, hakujawa na ishara yoyote ya kuwepo
kwa “Sera Kabambe ya Obama” kwa ajili ya Afrika. Labda hilo siyo jambo
baya ukitilia maanani tofauti na masuala mengine kuhusu Afrika.
Bwana Obama kawaachia wengine watoe tahadhari kuhusu Uchina, nchi ambayo haijitoshelezi kirasilimali.
Lakini kuna uwezekano kwamba muhula wake wa pili
utampa nafasi ya kujiondoa kutoka kwa mkakati wake wa “vita dhidi ya
ugaidi” huko Mali na Somalia, na kuangazia maswala mapana zaidi –
hususan biashara – jambo aliloligusia miaka mitatu iliyopita nchini
Ghana.