PICHA ZA USHAHIDI ZAWAUMBUA MAPOLISI AFRIKA KUSINI.
Posted on
Nov 7, 2012
|
No Comments
Picha
zilizowasilishwa mbele ya tume inayochunguza mauaji ya wachimba migodi
waliouawa karibu na mgodi wa palatinum wa Marikana zinaonekana
kudhibitisha tuhuma kuwa maafisa wa polisi nchini Afrika kusini
waliweka silaha karibu na miili.
Picha ya kwanza inaonyesha mwili wa mwanamume aliyefariki katika sehemu iliyo karibu na mgodi wa Marikana.
Picha
ya pili iliyopigwa baadaye lakini siku hiyo hiyo, ni sawa na picha ya
kwanza lakini hii inaonyesha mwanamume huyo huyo akiwa na panga lenye
mkono wa rangi ya njano lililo chini ya mkono wake wa kulia.
Picha
zote zilipigwa na maafisa wa polisi wa Afrika kusini muda mfupi tu
baada ya kuuawa kwa wachimba mgodi thelathini na wanne na polisi mnamo
mwezi Agosti.
Ipo
mifano mingine zaidi na inamaanisha kuwa huenda eneo la tukio la
uhalifu lilibadilishwa na maafisa hao wa polisi ili waweze kujitetea
kuwa waliwashambulia wachimba mgodi hao ili kujikinga.
Wakili
George Bizos ambaye kwa wakati mmoja alimtetea Nelson Mandela, anasema
kuna ushahidi mzito wa kujaribu kuzuia haki kutendeka na hivyo ametoa
wito kwa maafisa wakuu wa polisi kueleza ni nini kilichotokea.