WANANDOA NA UKIMWI, KUCHUKUA TAHADHARI NI MUHIMU
Posted on
Nov 30, 2012
|
No Comments
Pete ya ndoa ni sehemu kubwa katika ndoa
FWANANDOA wanashauriwa kupima maambukizi ya
Ukimwi ili kuongeza tahadhari kwa kuwa bado kuna uwezekano mkubwa wa
mmoja aliyeathirika kutomwambukiza mwenzake.
Utafiti mpya juu ya maambukizi ya uganjwa huo
umebaini kuwa, asilimia 47 ya watu walio katika mahusiano ya kimapenzi
ambao mmoja anaishi na virusi vya Ukimwi, hawawaambukizi wenzi wao.
Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa na madaktari
bingwa wa nchini Uingereza na kuchapishwa katika Jarida la Magonjwa ya
Kuambukiza la Lancet, si lazima kila mwenye ukimwi amwambukize mwenzake,
ila kuchukua tahadhari ni muhimu.
Utafiti huo uliofanyika katika nchi 14 ikiwemo
Tanzania, kwa kuchukua sampuli za wenza 13,061 katika nchi 27, ulibaini
kuwa asilimia 47 ya wanawake na wanaume wenye Ukimwi walioko kwenye
mahusiano ya kudumu, walikuwa na wenza ambao hawana VVU.
Jarida hilo limeeleza kuwa zipo sababu za kibaolojia na kisayansi zinazofanya baadhi ya watu wasiwaambukize wenzao Ukimwi.
“Hii ni pamoja na aina ya seli za mwanadamu,
virusi na iwapo mmoja anatumia dawa za kufubaza makali ya Ukimwi au la,”
linaeleza Jarida hilo.
Utafiti huo unafafana na uliofanywa na Benki ya
Dunia (WB), chini ya Dk Damien de Walque katika nchi tano za Afrika,
zikiwemo Kenya na Tanzania ambao ulibaini kuwa, robo tatu ya wenzi
wanaoishi na VVU, mmoja hakuwa na maambukizi hayo.
Novemba mwaka huu, Shirika la Afya Duniani (WHO)
lilisema kuwa, karibu nusu ya watu wanaoishi na VVU walio katika
mahusiano wana wenza ambao hawana maambukizi.
Akizungumza tafiti hizo, Mganga Mkuu wa Hospitali
ya Amana, Meshack Shimwale alisema zipo sababu nyingi zinazofanya mwenzi
mmoja akawa na maaambukizi na wengine hana.
“Baadhi ya sababu hizo ni aina ya virusi, vichocheo, upekee wa maumbile, idadi ya wadudu na tabia zao,” alisemna kuendelea;
“Pia muda ambao mwenye virusi ameishi na virusi hivyo, iwapo anatumia ARV, au hatumii na majeraha katika sehemu za siri.”
Daktari huyo alibainisha kuwa kuna virusi ambavyo
vipo hai na vina kasi kubwa ya kuingia katika mwili wa mtu kwa haraka na
vingine si vikali. Virusi hivyo hufa kabla havijaingia katika majimaji
ya mwili wa binadamu, alisema.
“Tabia hizi za virusi ndizo zinazoweza kufanya mmoja kati ya wapenzi kuwa na maambukizi na mwingine asiwe navyo,” alisema.
Pia daktari huyo alibainisha kuwa, baadhi ya
wanawake maumbile yao yana kiwango kikubwa cha alkali ambacho huviua
virusi vya Ukimwi mara.
“Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa wapo watu wenye
seli ambazo zinasababisha virusi visiingie katika miili yao, ingawa
tafiti hizo hazijathibitishwa,”alisema Dk Shimwale
Hata hivyo, Dk Shimwale alisema tafiti za hakika zaidi zinaendelea kufanyika kujua sababu ya kuongezeka kwa wenza wa aina hiyo.
Dk Shimwale alishauri kuwa, wapenzi/wanandoa
wapime afya zao kabla ya kuanza kufanya ngono na kila mara inapowapasa
kufanya hivyo.
Tacaids yatahadharisha
Katika hatua nyingine vijana Tanzania
wametahadharishwa kujikinga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa vile
ndilo kundi lililo kwenye hatari zaidi.
Tahadhari hiyo ilitolewa hivi karibuni na Kaimu
Mkurugenzi wa Mwitikio wa Taifa wa Tume ya Kudhibiti Maambukizi ya
Virusi vya Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Morris Lekule.
“Vijana wanatakiwa wajue kuwa, kuna adui anawanyemelea ambaye ni Ukimwi, hivyo wanapaswa kujihadhari,” alisema Lekule
Kwa upande wake Afisa uhusiano wa TACAIDS, Glory
Mziray alisema takwimu za kasi ya maambukizi ya VVU kwa Tanzania
zinatarajiwa kutolewa mapema Machi, 2013 na Mtakwimu Mkuu wa Taifa.
Alisema takwimu zilizopo sasa zinaonyesha kuwa kasi ya maambukizi ni asilimia 5.7.