WAFANYA BIASHARA KILIMANJARO WAKAIDI KUSHUSHA BEI YA SUKARI
Posted on
Jan 10, 2013
|
No Comments
WAFANYABIASHARA wa sukari mkoani Kilimanjaro
wameendelea kukaidi agizo la Serikali la kuuza sukari kwa bei elekezi ya
Sh1,900 kwa kilo na kuendelea kuuza Sh2,300.
Mtendaji wa Kiwanda cha Sukari cha TPC, Jaffar Ally alipoulizwa kuhusu kutokushuka kwa bei hiyo alionyesha kushangaa akisema kiwanda chake bado kina mlundikano wa sukari.
“Hata sisi hatuelewi nini kinaendelea kwa sababu sukari tunayo nyingi na imelundikana hapa, kwa mazingira haya tulitarajia ifurike kwenye soko ili bei ishuke,” alisema Ally na kuhoji.
”Kama Nakumati Supermarket inauzwa sukari ambayo ni branded kwa Sh2,000 kwa kilo, kwa nini hiyo iliyoko kwenye mifuko mitaani iuzwe Sh2,200?”.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na waandishi wa habari hizi mji wa Moshi na baadhi ya wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro umethibitisha sukari kuuzwa kwa kati ya Sh2,000 na Sh2,200.
Mkazi wa Majengo, Muhamed Athman, alivilaumu vyombo vya dola kushindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo hadi wafanyabiashara wajione wako juu ya sheria.
“Bei ya sukari iko juu sana tunanunua kwa sasa Sh2,200 na wakati mwingine Sh2,300 kwa kilo, hatuelewi ile bei elekezi ya serikali ni kiini macho au ni usanii fulani?” alihoji Athman.
Hata hivyo, wakati bei ya soko kwa kilo moja ya sukari ikiwa kati ya Sh2,000 hadi Sh2,300, viongozi wa serikali mkoani hapa walidai hawana taarifa ya suala hilo.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika, Kasya Kasya alisema binafsi hakuwa na taarifa juu ya ulanguzi huo wa sukari.
Hata hivyo, Kasya alisema waliwahi kukutana na wadau wote wa sukari Mkoa wa Kilimanjaro na kujadili bei ya sukari na kufikia mwafaka wa kuuza Sh1900 kwa kilo wauzaji wa rejareja.
Kwa upande wake, Msaidizi wa Ofisa Biashara Manispaa ya Moshi, Lucy Sewe alisena wiki iliyopita walifanya ukaguzi kwenye Super Markets na kubaini wanauza sukari kwa Sh1,900.