photo NAAZ_zpsd0bbd510copy_zps37715af5.jpg
 photo NAAZ_zpsd0bbd510.jpg
Nafasi Ya Matangazo
> > HII NDIYO SHULE ILIYOSHIKA NAFASI YA MWISHO KIDATO CHA NNE KITAIFA

HII NDIYO SHULE ILIYOSHIKA NAFASI YA MWISHO KIDATO CHA NNE KITAIFA

Posted on Feb 24, 2013 | No Comments


 
MATOKEO ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 yaliyotangazwa mwanzoni mwa juma, yanaendelea kutawala mijadala mbalimbali kila kona.
Sababu kubwa ya mijadala hiyo kutawala yaweza kuwa ni takriban kila familia kuguswa kwa njia moja ama nyingine na matokeo hayo.
Katika matokeo hayo karibu shule zote za umma zimefanya vibaya, zile za kata zikiongoza katika kufelisha, huku ile ya  Mibuyuni iliyopo Kilwa mkoani Lindi ikiwa ya mwisho kabisa katika kundi la shule zenye zaidi ya wanafunzi 40.
Mkuu  msaidizi wa shule hiyo Robart Mzumbi, alisema  kuwa matokeo hayo yalitarajiwa kwa kuwa tangu wanafunzi hao walipoandikishwa kidato cha kwanza, hawakuwa wamefaulu.
Alibainisha kuwa, matokeo ya kidato cha pili ya wanafunzi hao walipofanya mtihani wa taifa mwaka 2010, yalikuwa kiashiria kingine kwamba, hata kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wanafunzi hao hawatafanya vizuri.
Pamoja na hayo, Mzumbi anaeleza kwamba kwa kuwa lengo lao lilikuwa ni kuhakikisha wanafundisha watoto hao na mwisho wafanye vyema, matokeo hayo yamewasikitisha kwa kiasi kikubwa.
Alitaja upungufu wa walimu na umaskini wa kipato kwa jamii  inayozunguka shule hiyo kuwa ni moja ya sababu kubwa zilizosababisha matokeo hayo mabaya.
Mwalimu huyo alibainisha kwamba idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo hujishughulisha zaidi na biashara ndogo ndogo, badala ya kusoma.
Aliweka wazi kuwa, shule hiyo ilikuwa ya mwisho kati ya shule  3,392 zenye watahiniwa 40 na kuendelea, wakati watahiniwa hao wa mwaka 2012 walipochaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka 2009, ambapo walikuwa na alama za chini.
Aliongeza kuwa wanafunzi hao walichaguliwa kuanza kidato cha kwanza wakati tayari wengi wao walishaanza kufanya biashara ndogondogo, hivyo walikusanywa kutoka huko mitaani na kupelekwa shule.
“Ndugu yangu shule yetu huwa inafanya vizuri kidogo, angalia matokeo ya kidato cha pili mwaka huu Sekondari ya Mibuyuni imekuwa ya 115 kati ya shule 242 za Kanda ya Kusini, wanafunzi wanane wamefaulu kati ya 25 waliofanya mtihani. Lakini kwa matokeo ya kidato cha nne, kwa kweli wanafunzi waliochaguliwa mwaka 2009, hawakuwa na sifa bali waliokotwa tu ili kujaza darasa,”  alisema na kuongeza:
“Hata mtihani wa kidato cha pili  mwaka 2010, walifanya vibaya sana na shule hii ilikuwa ya  pili kutoka mwisho.”
Mzumbi alisema kwamba shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kukosa maabara, upungufu wa walimu wa sayansi, usafiri na umeme wa uhakika.
Pia ina ukosefu wa maji, nyumba za walimu, mabweni kwa ajili ya watoto wa kike, pamoja na shule kujengwa mbali na makazi ya wananchi.

Alieleza kuwa wanafunzi wengi wanaosoma katika shule mbalimbali za Mkoa wa Lindi, hulazimika kutembea umbali mrefu kutoka nyumbani kwenda shuleni.
Mohamedi Bori, mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo anasema kuwa wakati shule hiyo ilipofunguliwa mwaka 2008, ilikuwa na walimu wawili, kwa kipindi cha  zaidi ya miaka mitatu mfululizo.
Bori alisema kuwa wakati wao walipoingia kidato cha kwanza mwaka 2010,  kulikuwa na walimu watatu, huku shule hiyo  ikiwa na wanafunzi  140 wa  kidato cha kwanza hadi cha nne, hali ambayo ilisababisha walimu kuelemewa na majukumu ya kufundisha.
Sababu nyingine za kufanya vibaya zinatajwa kuwa ni walimu wachache waliopo kuondoka mara kwa mara na kukatisha mitalaa hivyo wanafunzi kutoshika vizuri wanayofundishwa hali iliyochangia pia wanafunzi kukata tamaa na kuangukia kwenye utoro.
Wanafunzi wengine walisema kuwa hali hiyo ilichangia wengi wao kuamua kujihusisha na biashara ndogondogo ikiwamo ya kuuza  samaki, migahawa, maji, biskuti na juisi katika stendi kuu ya mabasi Nangurukuru.
Naye  Saidi Mwichande, mkazi wa Kijiji cha Mkwajuni Nangurukuru, alisema kuwa wamepokea matokeo ya watoto wao kwa huzuni na kwamba wanatarajia kufanya kikao cha pamoja na walimu na wanafunzi wa shule ili kubaini tatizo lililopo.
Mwichande alisema jukumu la kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya shule hiyo lipo mikononi mwa wazazi na wadau wengine wanaoishi katika kata hiyo ili kuiletea maendeleo ya shule hiyo.
Wakati huohuo, Mawaziri wa zamani wa Serikali, Profesa Simon Mbilinyi aliyekuwa Waziri wa Fedha na Gaudence  Kayombo aliyekuwa Naibu Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwekezaji,  wameelezea kusikitishwa kwao na idadi kubwa ya wanafunzi waliohitimu kidato cha nne 2012 kufeli mitihani yao.
Akizungumza katika mahojiano na gazeti hili, Mbilinyi  alisema kuwa matokeo hayo yamechangiwa na kushuka kwa nidhamu kwa walimu na wanafunzi huku akiitaka Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia wahitimu waliofeli.
“Mafanikio yoyote ya elimu yanachangiwa na nidhamu, naweza kusema tatizo la matokeo mabaya limechangiwa na kushuka kwa nidhamu. Angalia, shule za misheni mara nyingi zimekuwa zikifanya vyema kuliko shule za kata, au za Serikali. Hii ni kutokana na wao kujali nidhamu hata mwanafunzi akiwa na akili za kutisha akifanya utovu wa nidhamu hufukuzwa,”alisema Profesa Mbilinyi.
Alitoa ushauri kwa wazazi, walimu na jumuia zinazowazunguka wanafunzi kuwajengea nidhamu ya kuheshimu masomo na kupenda kujisomea ili kuweza kutatua tatizo la wanafunzi kufeli.
Kwa upande wake  Gaudence  Kayombo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mashariki alisema taifa linahitaji kufanya utafiti ili kujua kilichochangia wanafunzi hao kufeli kwa kiwango kikubwa.
Alisema kuwa ili tatizo hilo lipatiwe ufumbuzi, wakaguzi wa elimu wana wajibu wa kuwakagua walimu kama wanatimiza wajibu wao ipasavyo kwa kuwafundisha  wanafunzi, lakini pia Serikali itoe vifaa vya kufundishia ili kuhakikisha wanafunzi wanapewa haki yao ya msingi ya  kufundishwa na kuelewa.
Aliwataka wazazi kutimiza wajibu wao kwa kuwabana na kukagua madaftari ya watoto wao wanaporudi nyumbani ili kuwajengea moyo wa kupenda kujisomea.
Imeandaliwa na Mwanja Ibadi, Kilwa  na Joyce Joliga, Songea

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru