JENGO LA ATCL HATARINI KUPIGWA MNADA
Posted on
Feb 19, 2013
|
No Comments
JENGO la Makao Makuu ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) liko hatarini kupigwa mnada kwa amri ya Mahakama kutokana na kushindwa kulipa deni inalodaiwa na Kampuni ya Huduma za Utalii ya Leisure Tours and Holidays.
Tayari Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara imeamuru kampuni hiyo ifanye uthamini wa jengo hilo na kuwasilisha mahakamani taarifa hiyo leo.
Hatua hiyo inatokana na mao mbi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na kampuni hiyo ambayo ni mshindi wa tuzo katika kesi ya madai namba 56 ya mwaka 2009 iliyotokana na mgogoro wa kibiashara baina yake na ATCL.
Kampuni hiyo inaidai ATCL Dola za Marekani, 716,259.25 (Sh1.1 bilioni) baada ya kushindwa kulipia huduma za ukodishaji wa magari ambazo kampuni hiyo ilitoa kwa ATCL.
Mbali na kiasi hicho ambacho ni deni la msingi pamoja na riba ya asilimia 10 kwa kipindi cha miaka miwili, pia ATCL inapaswa kuilipa kampuni hiyo gharama za uendeshaji wa kesi hiyo.
Katika amri ya Mahakama hiyo iliyotolewa na Jaji Mfawidhi Robert Makaramba Februari 11, 2013, kabla ya kutoa amri ya jengo hilo kupigwa mnada, ilimwamuru mshinda tuzo kufanya uthamini wake.
Taarifa ya amri hiyo inasomeka: “Amri: Muombaji/mshinda tuzo anatakiwa kuwasilisha katika Mahakama hii taarifa ya uthamini wa jengo la ATCL, lililoko katika Mtaa wa Ohio, (Dar es Salaam) saa 3.00 asubuhi, Februari 20, 2013. Shauri litakuja kwa amri zaidi saa 3.00 asubuhi, Februari 25, 2013,” inasomeka amri hiyo.
Hata hivyo, Wakili wa mshinda tuzo, Jerome Msemwa wa Kampuni ya Msemwa & Company Advocates, alisema licha ya amri ya Mahakama kufanya uthamini wa jengo hilo, lakini maofisa wa mshindwa tuzo wamezuia kufanyika uthamini.
Wakili Msemwa alisema maofisa hao wa mshindwa tuzo walizuia uthamini huo kufanyika kwa madai kuwa watalipa.
Alisema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakiahidi hivyo bila utekelezaji na kwamba leo anawasilisha mahakamani taarifa hiyo ya kuzuiwa na kisha kusubiri amri ya Mahakama.
Awali, Novemba 20, 2012, Mahakama hiyo ilimwamuru mshindwa tuzo kuwasilisha mahakamani hapo jedwali la malipo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tangu tarehe ya amri hiyo.
Hata hivyo, mshindwa tuzo hakutekeleza amri hiyo ndipo mshinda tuzo alipowasilisha maombi ya kukamata na kuuza jengo hilo.
Katika kesi ya msingi pande zote zilikubaliana kuzungumza na kufikia mwafaka nje ya Mahakama, makubaliano ambayo kila upande ulisaini ikiwa ni ishara ya kukubali kutekeleza.
Waliwasilisha mahakamani makubaliano hayo, Aprili 8, 2011 ili yaidhinishwe na kuwa uamuzi halali.
Katika makubaliano hayo, mshindwa tuzo anapaswa kumlipa mshinda tuzo kiasi cha Dola 596,882.97(Sh952 bilioni) kwa awamu tatu za kiasi cha Dola 198,960.99 (Sh317 bilioni) kwa kadri anavyopata fungu kutoka Hazina.
Pia, walikubaliana mshindwa tuzo amlipe mshinda tuzo kiasi cha Dola 119, 376.97(Sh190 bilioni) kikiwa ni riba ya asilimia 10 kwa mwaka ya malipo ya msingi, kwa kipindi cha mwaka wa 2009 na 2010, kwa awamu tatu kadri anavyopata fungu kutoka Hazina.
Hata hivyo, ATCL haikutekeleza ulipaji wa fidia hiyo kama walivyokubaliana na jinsi Mahakama ilivyoamuru.