TAIFA STARS YALIEMA CAMEROON JIJINI DAR
Posted on
Feb 7, 2013
|
No Comments
Timu ya taifa ya soka ya
Tanzania, Taifa Stars, imeandikisha ushindi mwingine mkubwa, pale
ilipoilaza Indomitable Lions kutoka Cameroon, bao moja kwa bila, katika
mechi ya kimataifa ya kirafiki iliyochezwa mjini Dar es Salaam.
Mbwana Samatta, anayeichezea klabu ya TP Mazembe
ya Congo, ndiye aliyeifungia taifa stars bao hilo la pekee na la
ushindi kunako dakika ya themanini na tisa.
Hata hivyo Taifa Stars ingelikuwa na mabao mawili lakini Erasto Nyoni alikosa penalti.
Ushindi huo, unajiri wiki kadhaa baada ya
Tanzania kuilaza mabingwa wa Afrika Chipolopolo ya Zambia kwa bao moja
kwa bila katika uwanja huo huo wa taifa.
Mlinda lango wa Cameroon, Ngoula Patrick,
anayeichezea klabu ya Union Doula, aliunawa mpira, hatua iliyopelekea
refa wa mechi hiyo Munyemana Hudu kutoka Rwanda kuamuru penalti ipigwe.
Baada ya dakika za 45, timu hizo mbili, zilikuwa zikitoshana nguvu ya kutofungana bao lolote.
Hata hivyo katika kipindi cha pili, Tanzania
ilirejea huku ikifanya mashambulio makali dhidi ya wageni wao lakini
juhudi zao hazikuzaa matunda hadi kocha Kim Poulsen alipofanya
mabadiliko na kumtoa kiungo wa Simba, Kazimoto, katika dakika ya 56 na
nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji wa TP Mazembe, Thomas Ulimwengu.
Ulimwengu aliwahangaisha mabeki wa Cameroon na
timu hiyo ilionekana kukosa huduma za nyota wake Samuel Eto'o
anayeichezea klabu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi na Alex Song wa
Barcelona ya Hispania, ambao walikuwa wakiuguza majeruhi.
Mabadiliko hayo yalizaa matunda dakika ya 89 ya mechi hiyo.
Kocha wa Taifa Stars, aliwasifu wachezaji wake
kwa kuonyesha mchezo mzuri na kusema mechi hiyo imewapa motisha zaidi
wachezaji wake na wako tayari kwa michuano ya kufuzu kwa kombe la dunia.
Kocha wa Cameroon, naye Jean Paul Akono, alikiri
kuwa vijana hao wa taifa Stars, walionyesha mchezo mzuri wa walistahili
kushinda.