photo NAAZ_zpsd0bbd510copy_zps37715af5.jpg
 photo NAAZ_zpsd0bbd510.jpg
Nafasi Ya Matangazo
> > POLISI WARUKA UKUTA KUMKAMATA LEMA.

POLISI WARUKA UKUTA KUMKAMATA LEMA.

Posted on Apr 27, 2013 | No Comments

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema akiwa polisi siku za hivi karibuni 

Arusha. Maofisa wa Jeshi la Polisi, waliokuwa na mbwa, mabomu ya machozi na silaha nyingine za moto, usiku wa kuamkia jana waliruka ukuta na kuingia katika eneo la makazi ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ambako walizingira nyumba yake kwa zaidi ya saa nne.
Operesheni ya kutiwa mbaroni Lema iliogozwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha (OCD), Gillel Muroto ambaye alifuatana na askari zaidi ya 25 waliokuwa na silaha hizo.
Walifika nyumbani kwa Lema saa 5:00 usiku lakini walilazimika kusubiri hadi saa 9:10 walipomkamata Mbunge huyo baada ya yeye mwenyewe kujisalimisha. Habari zinasema Lema aliyekuwa akihojiwa na polisi hadi jana jioni, alinyimwa dhamana kwa maelezo kwamba “anaweza kuhatarisha amani”.
Mashuhuda waliokuwa karibu na anakoishi Lema, eneo la Njiro Mwisho wa Lami, walisema polisi hao walifika wakiwa kwenye magari manne na kwamba ili kuchunguza ndani ya uzio wa nyumba yake, walipanda juu ya mabega ya wenzao huku wakielekeza mitutu ya bunduki tayari kukabiliana na lolote ambalo lingejitokeza.
Baada ya kuchungulia baadhi yao walitumbukia ndani ya uzio na kwenda kusimama mbele ya milango na madirisha ya nyumba ya Lema na huku nyuma wengine walipanda tena kwenye mabega ya wenzao kuendelea kuweka ulinzi kwa walioingia ndani.
Askari hao wanadaiwa kwamba waliwataka walinzi wa nyumba hiyo iliyopo karibu na Chuo cha Ufundi Veta, kuwafungulia mlango, lakini walinzi hao walikataa hivyo kuzua mabishano makali.
Kutokana na mabishano hayo, Lema aliyekuwa ndani amelala alishtuka na kuanza kufuatilia na kubaini kuwapo kwa polisi nje ya nyumba yake hiyo. Mke wa Lema, Neema alimpigia simu Katibu wa Wilaya wa Chadema, Aman Golugwa kumwarifu kuhusu uwepo wa watu walioruka ukuta.
Golugwa jana alithibitisha kupokea simu ya mke wa Lema na kwamba alipopata taarifa hizo alimwarifu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) wa Mkoa wa Arusha, Camillius Wambura ambaye baadaye alimuahidi kwamba angefuatilia suala hilo.
“Baadaye alithibitisha kuwapo kwa polisi waliotumwa kwa ajili ya kumkamata Lema lakini akasema amewapa maelekezo ya kufuata taratibu za kawaida,”alisema Golugwa na kuongeza:“Baada ya hapo, wale askari waliokuwa wameruka ukuta walitoka nje ya uzio”.
Habari zinasema wakati baadhi ya askari wanaruka ukuta, wengine walibaki nje wakizingira uzio wa nyumba ya Lema huku wakiwazuia viongozi wa Chadema waliokuwa eneo hilo kusogea.
Kukamatwa kwa Lema katika mtindo wa aina yake kumefanywa saa chache tangu alipotoa kauli ya kukataa kujisalimisha polisi, kutokana na agizo la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo. Mulongo aliagiza Lema akamatwe kwa tuhuma kwamba alichochea vurugu katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).
Katika vurugu hizo, wanafunzi hao walimzomea Mulongo na kurushia mawe msafara wake wakati alipokwenda kusikiliza malalamiko yao yaliyotokana na kuuawa kwa mwanafunzi mwenzao, Henry Kago (22) ambaye alichomwa kisu na watu wasiofahamika wakati anatoka kujisomea saa 4:00 usiku.
“Kuna taratibu za kumwita mbunge polisi, wanaweza kunipigia simu au kuwasiliana na Spika, lakini siyo kutumia utaratibu huu wa kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa mimi natakiwa kukamatwa wakati najua sina kosa,”alisema Lema.
Kauli ya Lema
Akizungumza na Mwananchi kabla ya kujisalimisha kwa askari hao juzi usiku, Lema alisema alishangaa polisi kuvamia nyumba yake usiku wakati walikuwa na uwezo wa kumpigia simu na kumwita.
“Wapo nje ya nyumba yangu, wanatishia kupiga mabomu kama nisipotoka nje, lakini wanajadiliana na walinzi wangu na mimi nimewataka wanipe hati ya kunikamata,” alisema Lema. Hata hivyo, baada ya muda idadi kubwa ya wafuasi wa Chadema, walijitokeza na kuzingira nyumba ya Lema, hali ambayo ilianza kutishia uvunjifu wa amani.
Golugwa ndiye aliyefanya majadiliano na OCD Muroto kuhusu namna ya kufanikisha mbunge huyo kujisamilisha baada ya kuwa amewasiliana na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na ilipotimu saa 9:10 usiku Lema alijisamilisha baada ya kuhakikishiwa usalama wake.
Mmoja wa viongozi wa Chadema, Calist Lazaro alisema walikubali Lema aende polisi, baada ya majadiliano na viongozi wa juu ya chama hicho.
“Tulitaka Polisi watuhakikishie usalama wake na pia tulitaka suala hili lifanyike kwa uwazi kwani siyo jambo la kawaida mbunge kuvamiwa na polisi usiku kama jambazi,”alisema Lazaro.
Polisi wanena
Kamanda wa polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas jana, alikiri maofisa wa jeshi hilo kumkamata mbunge huyo juzi usiku na hadi jana mchana alikuwa bado yupo rumande.
“Ni kweli tupo naye hapa polisi, anasubiri kuhojiwa kutokana na tuhuma za uchochezi katika Chuo cha Uhasibu Arusha,”alisema Kamanda Sabas. Alisema uamuzi wa kuendelea kumshikilia au kumwachia, utatolewa baada ya kukamilika mahojiano.
Mapema wakili wa Lema, Hamphrey Mtui akizungumza na Mwananchi nje ya kituo kikuu cha polisi, alisema bado alikuwa hajaruhusiwa kuonana na mteja wake .
“Bado tunasubiri polisi wamtoe na wakati wa kuchukua maelezo yake ndiyo wameniambia wataniita,” alisema Mtui. Baadaye Lema alihojiwa lakini alikataliwa kupewa dhamana.
Taarifa za kukamatwa kwa Lema zilianza kusambaa juzi saa sita kasorobo usiku na ilipofika jana asubuhi tayari tukio hilo lilikuwa limeishateka mijadala ya mitandao ya kijamii.
Mijadala hiyo iliambatana na mkanda wa Video wa Lema wakati akizungumza na wananfunzi wa IAA.
Hali hiyo pia iliuweka mjia wa Arusha katika hali tete na kulikuwa na wasiwasi mkubwa kwamba wafusai wa Chadema wangeandamana kushinikiza kuachiwa kwa mbunge huyo. Katika kituo kikuu cha polisi kulikuwa na kundi kubwa la wafuasi wa Chadema waliokusanyika kufuatilia hatma ya mbunge wao na kusababisha ulinzi uongezwe maradufu ili kukabiliana na lolote ambalo lingeweza kutokea.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru