CCM YAMTAJA ATAKAYEWANIA UBUNGE JIMBO LA CHAMBANI
Posted on
May 15, 2013
|
No Comments
Dodoma. Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeteua na kupitisha jina la Mattar Sarahan Said kuwa mgombea Ubunge katika Jimbo la Chambani, Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba.
Uchaguzi wa jimbo hilo unafanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge, Salim Hemed Khamis (CUF) aliyefariki Machi 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati akihudhuria moja ya vikao vya Kamati za Bunge.
Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Zanzibar, Waride Bakari Jabu alisema Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Zanzibar ilikutana mwishoni mwa wiki na ilipendekeza majina mawili likiwamo hilo la Mattar na kuwasilisha kwa Kamati Kuu ya CCM.
Kamati hiyo ilipitisha uteuzi huo katika kikao chake cha siku moja kilichofanyika mjini Dodoma jana chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
Katika kikao hicho, pia imemteua Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Balozi Seif Idd kuzindua kampeni hizo,
Mei 18 mwaka huu wakati naye Mwenyekiti mstaafu wa CCM na Rais Mstaafu wa Awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi atafunga kampeni hizo kabla ya uchaguzi Juni 6.