LWAKATARE KUSOTA RUMANDE HADI MEI 27
Posted on
May 14, 2013
|
No Comments
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Wilfred Lwakatare akipelekwa kizimbani katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana,
Dar es Salaaam. Jitihada za mawakili wa
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Wilfred Lwakatare, kumchomoa mahabusu, jana ziligonga mwamba
na sasa atalazimika kuendelea kusota mahabusu hadi Mei 27 mwaka huu.
Mawakili hao wa Lwakatare jana waliiomba Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, impatie dhamana, Lwakatare baada ya Mahakama Kuu
Kanda ya Dar es Salaam, kumfutia, mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa
yakimkabili yeye na mwenzake Joseph Ludovick Rwezaura, ambayo hayana
dhamana.
Juzi mmoja wa mawakili hao, Peter Kibatala
aliliambia gazeti hili kuwa walikuwa wamejiandaa kikamilifu kuhakikisha
kuwa wangeweza kumtoa kwa dhamana kwa kuwa walikuwa tayari wamekamilisha
masharti ya dhamana.
Hata hivyo, jitihada zao ziligonga mwamba kufuatia
kitendo cha hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Aloyce Katemana, kutokuwapo
mahakamani na hivyo kusababisha kesi hiyo kuahirishwa hadi Mei 27.
Mapema, Wakili Mkuu wa Serikali, Prudence
Rweyongeza aliieleza mahakama kuwa kesi hiyo ilikuwa imepangwa kwa ajili
ya kutajwa na kuomba ipangiwe siku nyingine ya kutajwa.
Hata hivyo, Wakili Kibatala aliiomba mahakama impe
dhamana Lwakatare huku akirejea uamuzi wa Mahakama Kuu, kuwafutia
mashtaka ya ugaidi na kubakiwa na shtaka la kula njama ambalo kisheria
linadhaminika.
“Pamoja na kwamba hakimu mhusika hayupo, lakini
tunaomba dhamana kwa kuwa tunaamini kuwa mahakama yako inaweza kutoa
dhamana kwa kuzingatia kuwa dhamana ni haki na hasa kwa kuzingatia kuwa
amekaa mahabusu kwa muda mrefu na afya yake (Lwakatare) si nzuri,”alidai
Wakili Kibatala.
Hata hivyo, Wakili Rweyongeza alipinga maombi hayo ya dhamana akidai kuwa yametolewa nje ya muda kwa mujibu wa taratibu.
Pia alidai kuwa uamuzi wa mahakama unaanza baada ya mkurugenzi wa mashtaka, kuwasilisha maelezo ya kesi.
Wakili Kibatala alipangua hoja hizo akidai kuwa
hoja za Wakili Rweyongeza zinalenga katika kuondoa haki ya dhamana na
kwamba hakuna pingamizi lolote la kisheria.
Huku akitoa mifano ya kesi kadhaa wakili huyo
alisisitiza kuwa hata katika hatua hiyo mahakama inaweza kutoa dhamana
wakati taratibu nyingine zikiendelea.
Hata hivyo, Hakimu Sundi Fimbo alisema kwa kuwa
yeye si hakimu anayesikiliza kesi hiyo hawezi kuamua lolote na kwamba
anachokifanya ni kurekodi hoja za pande zote kwenye jalada la kesi.
Aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 27, mwaka huu.
Juzi Wakili Rweyongeza aliliambia gazeti hili kuwa
wanasubiri kupata nakala ya uamuzi wa Mahakama Kuu, kuhusu kuwafutia
mashtaka ya ugaidi ili waweze kuona hatua ambazo wanaweza kuzichukua,
kama ni kukata rufaa au la.
Katika hatua nyingine, mahakama jana iliwaacha
solemba wafuasi wa Chadema baada ya kusikiliza na kuahirisha kesi hiyo
bila wao kujua.
Wafuasi hao wa Chadema walikuwa wamefurika katika
ukumbi wa mahakama namba mbili wakisubiri kesi hiyo, lakini wakati
wakisubiri katika ukumbi huo, kesi hiyo ilikuwa ikiendelea katika
‘chamber’ ya Hakimu Fimbo hadi ilipomalizika.
Lwakatare na Rwezaura walikuwa wakikabiliwa na mashtaka manne, matatu kati yake yakiwa ya ugaidi na moja la jinai ya kawaida.
Mashtaka hayo yalikuwa ni kula njama, kupanga
kumteka Dennis Msacky na kisha kumdhuru kwa kutumia sumu na kufanya
mkutano wa vitendo vya kigaidi.
Hata hivyo Mei 8, mwaka huu, Mahakama Kuu
iliwafutia mashtaka hayo matatu ya ugaidi na kubakiwa na shtaka moja tu
la kula njama za kutenda kosa la kumdhuru Msacky kwa kutumia sumu.
Uamuzi huo wa Mahakama Kuu ulitokana na maombi ya
jopo la mawakili wa Lwakatare waliyoyawasilisha mahakamani hapo
wakiiomba ipitie uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka, kuwafutia kesi ya
awali na kisha kuwakamata na kuwafungulia tena kesi ya mashtaka
hayohayo.