VIONGOZI WA AU WANAIHOFIA NINI ICC?
Posted on
May 29, 2013
|
No Comments
Wiki iliyopita Umoja wa Afrika (AU), ulitimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1963 mjini Addis Ababa, Ethiopia. Hivyo, viongozi wa nchi 54 wanachama wa umoja huo waliwasili nchini humo kusherehekea umoja huo kutimiza miaka 50 ya uhai wake. Tulitazamia kwamba mkutano huo ungekuwa fursa kwa viongozi hao kujitathmini katika nyanja za uchumi, demokrasia na utawala bora katika nchi zao.
Tulitarajia pia kwamba AU ingetumia fursa hiyo kutengeneza mazingira ya viongozi hao kujadili na kuweka dira ya maendeleo ya umoja huo angalao kwa miaka 25 ijayo, ili Bara la Afrika libadilike kutoka bara la nchi zinazoandamwa na njaa, umaskini, vita, ujinga na maradhi na kuwa bara lenye amani na uchumi mkubwa utokanao na viwanda.
Kwa maneno mengine, hiyo ilikuwa fursa kwa viongozi hao sio tu kujitathmini mmojammoja, bali pia kwa pamoja kutafakari kwa kina na kupata mikakati ya kutambua wapi umoja huo unapaswa kuelekea baada ya miaka 50 ya mateso ya raia wa nchi zao yaliyotokana na adha nyingi, zikiwamo udikteta na utawala wa mabavu wa viongozi hao. Ajenda ya viongozi hao ingekuwa namna ya kuimarisha umoja huo kwa kuunganisha nchi hizo na kuunda bunge moja, sarafu moja, jeshi moja, benki moja, rais mmoja, serikali moja na kadhalika.
Lakini kwa mshangao wa wengi, viongozi hao walisuka ajenda ya kuishambulia Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), wakidai kwamba mahakama hiyo inaendesha kesi zake kwa kuwang’ang’ania viongozi wa Afrika pekee. Kama hiyo haitoshi waliituhumu ICC kwamba inaelekeza mashtaka kwa viongozi wa Afrika kwa sababu ya rangi yao, huku wakijikita katika mashtaka yanayowakabili watuhumiwa wa vurugu za baada ya Uchaguzi Mkuu nchini Kenya mwaka 2007, Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake, William Ruto.
Badala ya kuweka mbele ajenda za kuinua maisha ya raia wa nchi zao, viongozi hao waligeuka na kuwa genge la kuteteana, kulindana na kupongezana kwa mafanikio yasiyokuwapo. Muda mwingi ulipotea katika kuelekeza mashambulizi kwa ICC ambayo iliundwa mwaka 2002 na jumuiya ya kimataifa, zikiwamo nchi nyingi wanachama wa AU, chini ya Mkataba wa Roma na kuipa mamlaka ya kushughulika na kesi za uhalifu dhidi ya binadamu.
Inatia kichefuchefu kuwasikia viongozi hao wakiituhumu ICC, ambayo imefanya kazi nzuri ya kuwawajibisha viongozi madikteta na wauaji wa raia katika mabara mengi, yakiwamo Afrika, Asia, Amerika ya Kusini na Ulaya. Ni kweli wengi wa viongozi madikteta na wauaji wa raia wao waliofunguliwa mashtaka katika ICC wanatoka Afrika. Hii ni kwa sababu Bara la Afrika ndilo linaloongoza kwa ukiukaji wa haki za binadamu, sio kwamba viongozi wake wanalengwa tu na ICC kwa sababu ni Waafrika.
AU imetoa tamko ikiitaka ICC iache kesi dhidi ya Kenyatta na Ruto isikilizwe na mahakama za Afrika. Ombi hilo lilikataliwa awali na Baraza la Usalama la UN na pia limekataliwa na ICC, kutokana na ukweli kwamba kesi ya nyani haiwezi kupelekwa kwa ngedere. Kufanya hivyo kungewanyima haki waathirika wa vurugu hizo za mwaka 2007 ambao ndugu na jamaa zao watatoa ushahidi dhidi ya Kenyatta na Ruto katika kesi hiyo iliyo ICC.