photo NAAZ_zpsd0bbd510copy_zps37715af5.jpg
 photo NAAZ_zpsd0bbd510.jpg
Nafasi Ya Matangazo
> MAELFU WANZIKA NGWAIR

MAELFU WANZIKA NGWAIR

Posted on Jun 7, 2013 | No Comments


Mama mzazi wa marehemu Albert Mangwea, Denisia Mangwea akisali mbele ya mwili wa mwanawe kabla ya kuanza msafara kuelekea makaburi ya Mtakatifu Monica kwa ajili ya mazishi yaliyofanyika Kihonda, Morogoro jana. Picha na Juma Mtanda. 
Morogoro. Msanii wa muziki, Albert Mwangea, maarufu kama Ngwair amezikwa jana kwenye makaburi ya Kanisa Katoliki la Mtakatifu Monica eneo la Kihonda, nje kidogo ya Morogoro.
Kabla ya safari ya mwisho ya Ngwair aliyefariki zaidi ya wiki moja iliyopita nchini Afrika Kusini kuhitimishwa, maelfu ya wakazi wa
Morogoro, walipata fursa ya kutoa heshima za mwisho kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Juzi jioni, mamia ya watu walijitokeza kuupokea mwili wa msanii huyo kutoka Dar es Salaam, ambako nako watu walishiriki katika zoezi la kuuaga Jumatano kabla ya kusafirishwa.
Miongoni wa walioshiriki katika ibada ya kumwombea marehemu kwenye Uwanja wa Jamhuri na kisha kwenye mazishi, ni pamoja na wasanii mbalimbali wa muziki, filamu na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Pia alikuwapo Waziri Kivuli wa Habari Utamaduni na Michezo kutoka Kambi ya Upinzani Bungeni, Joseph Mbilinyi, wawakilishi wa wizara mbalimbali ikiwamo Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo na viongozi wa serikali.
Awali, akiongea katika ibada ya kumwombea marehemu, Paroko Msaidizi wa Kanisa la Mtakatifu Monica, Petter Luanda aliwataka wananchi kutokuhuzunika sana na kifo hicho, kwani bado kuna nafasi nyingine ya kufurahi kiroho mbinguni.
“Lakini pia hii ni fursa yetu kujiweka tayari kwa kifo wakati wowote. Kifo hakina miaka, muda wowote unaweza kufa, huwezi kusema mpaka uwe mzee ndipo kifo kikukute. Hatujui siku wala saa,” alisema Luanda.
Joel Bendera, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ndiye aliyeongoza mazishi hayo, ambapo alisema, umati uliojitokeza kumzika marehemu, unatoa taswira halisi ya namna alivyokubalika mbele ya jamii.
Marehemu Ngwair alizaliwa mwaka 1982, Mkoa wa Mbeya akiwa ni mtoto wa 10 wa mzee Kenneth Mangwea. Alisoma shule ya msingi Bungo kati ya mwaka 1990 na 1994, na kisha sekondari ya Mazengo na kuhitimu mwaka 2000.
Alijiunga na Chuo cha Sanaa Bagamoyo mwaka 2000, ambapo pia alikuwa mhamasishaji wa vikundi mbalimbali vya wasanii likiwamo kundi la ChembaSquard akiwa kama mwasisi.
Mungu amlaze mahali pema peponi.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru