WABUNGE WAZUIA UJENZI HOTELI NGORONGORO
Posted on
Jul 7, 2013
|
No Comments
Wabunge walipotembelea Ngorongoro
Ngorongoro. Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili
na Mazingira, imetangaza kupiga marufuku mpango wa ujenzi wa hoteli ya
kutalii eneo la Layanai jirani na Kreta ya Ngorongoro, ili kulinda
mazingira ya eneo hilo ambalo ni mapito ya Faru.
Mwenyekiti wa Kamati wa Bunge, Ardhi, Maliasili na
Mazingira, James Lembeli, alitangaza uamuzi huo jana baada ya kupokea
malalamiko kutoka kwa wataalamu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(NCAA) na wananchi wanaoishi ndani ya mamlaka hiyo, kuhusiana na
shinikizo kubwa kutoka serikalini la ujenzi wa hoteli hiyo.
“Kuanzia sasa kamati ya Bunge inatangaza rasmi
hakuna hoteli ambayo itajengwa eneo hilo la Kreta, kwani kuna maeneo
mengi ambayo yanaweza kujengwa hoteli hapa, hawa wanaotaka hilo eneo
wapelekwe pengine,” alisema Lembeli.
Hoteli hiyo, inashinikizwa kujengwa eneo hilo na
mfanyabiashara mmoja maarufu wa Arusha ambaye anamiliki hoteli ya
kitalii (jina linahifadhiwa), anayeungwa mkono na vigogo kadhaa wa
Serikali.
Kamati hiyo licha ya kupiga marufuku ujenzi wa
hoteli hiyo, imeitaka Wizara ya Maliasili na Utalii, kusitisha mara moja
mpango wake wa kutaka magari ya watalii kuruhusiwa kuingia ndani ya
hifadhi, kutoka na baadaye kurejea (double entre) kwa kulia mara moja.
“Huu ni mpango wa kifisadi unalenga kunufaisha
kampuni za utalii na utapunguza mapato zaidi ya nusu ya NCAA na hifadhi
nyingine za taifa nchini,” alisema Lembeli.
Lembeli alisema kamati hiyo, itakutana na Waziri
wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, kumweleza juu ya uamuzi
wao kwani wanaamini kuna watu wanatoaka kuipotosha Serikali kwa manufaa
yao.
Hata hivyo, wajumbe wa kamati hiyo, walielezea
kuridhishwa na hatua ya NCAA kukamilisha miradi ya ujenzi wa madarasa na
Mabweni Sekondari ya Nainokanoka kama walivyoagiza.
“Pia, tumeridhishwa kuanza vizuri mradi wa
kuboresha mifugo ya wafugaji wa Tarafa ya Ngorongoro, ila tunachoagiza
ni kuimarishwa uhusiano baina ya wakazi wa tarafa hii na watendaji wa
NCAA,” alisema Lembeli.
Alisema hatua hiyo itaongeza ushirikiano ambao
umeanza kujengwa kati ya mamlaka na wananchi na kwamba, itasaidia
kulinda wanyamapori na mazingira ya eneo hilo.
Wabunge hao walikagua baadhi ya miradi
inayoendeshwa na mamlaka kwenye kata hiyo, lengo likiwa ni kuangalia
maagizo waliyotoa kwa NCAA kama yametekelezwa.