photo NAAZ_zpsd0bbd510copy_zps37715af5.jpg
 photo NAAZ_zpsd0bbd510.jpg
Nafasi Ya Matangazo
> > MKURUGENZI TANESCO AINGIA MTAANI KUSAKA VISHOKA

MKURUGENZI TANESCO AINGIA MTAANI KUSAKA VISHOKA

Posted on Jul 9, 2012 | No Comments


WIZI wa umeme kwa njia ya mtandao umemfanya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Injinia William Mhando, kuingia mitaani kushiriki zoezi la ukaguzi wa mita za wateja.
 Akiwa kwenye zoezi hilo katika eneo la Keko Kanda ya Temeke jijini Dar es Salaam,  ambapo kwa wananchi lilionekana si la kawaida kutokana na kufuatana na baadhi ya mameneja na wataalamu Mhando alisema wamepokea taarifa ambazo siyo nzuri kuhusu wizi wa umeme kwa njia ya mtandao hali iliyomlazimu kufuatilia kwa makini tangu ngazi ya chini kabisa.
 Mhando alisema tangu kuanza kuzifanyia kazi taarifa hizo wameweza kumata watu wawili mkoani Dodoma na wengine watatu jijini  Dar es Salaam ambao kesi zao zimefikishwa mahakamani wakituhumiwa kutumia umeme ambao haujulikani umenunuliwa wapi.
 “Utakuta mteja amenunua umeme wa Sh10’000/ kwetu lakini unapokwenda kukagua utakuta anaumeme wa zaidi ya pesa hizo, nahii inamaanisha kuna sehemu zingine wananunua tofauti na Tanesco ambapo kwenye mfumo haupo,” Alifafanua Mhando.
 Alipoulizwa kuhusu sababu za kuwepo kwa tatizo hilo Mhando alisema wana  wasiwasi kuwa mtaalamu aliyekuja kuingiza mfumo huo, aliacha program mtaani na kufanya watu wenye nia mbaya kutumia nafasi hiyo.
 Hata hivyo, Mhando alisema tatizo hilo limegundulika haraka kutokana na mita maalum (Automatic Meter Reader), zilizofungwa ambazo husomwa moja kwa moja na Tanesco bila ya kwenda kwa mteja ndiyo maana tatizo hilo limegundulika haraka.
 Aidha alisema wameanza kufunga mfumo mwengine wa kudhibiti wizi, kwa kufunga kifaa hicho maalum (Supply Group hold), ambacho hadi sasa kimefungwa kwa wateja wakubwa 3000 jijini Dar es Salaam, zoezi hilo litaendelea kwa wateja wakawaida.
 Mbali na wizi wa mtandao Mkurugenzi huyo alishuhudia wateja waliojiunganishia umeme bila kupitia kwenye mita za shirika hilo.
Alisema baada ya kubaini hali hiyo aliwaamuru watendaji wake kukata umeme huo, huku akiamrisha jeshi la polisi kuwachukua na kuwafungulia mashitaka ya wizi, Meneja wa Baa ya King Paris alichukuliwa na polisi.
 Katika eneo la Keko mbali na nyumba za kawaida umeme ulikatwa kwenye nyumba za wageni pamoja na Baa mbalimbali zikiwemo baa ya Miami Shambwe  na Baa ya King Paris zilizopo kwenye eneo hilo.
 Naye Meneja wa kanda hiyo ya Temeke Richard Mallamia alisema hasara inayotokana na wizi wa umeme ni zaidi ya Sh milioni 80 ambapo tangu kuanza kwa zoezi hilo wamefanikiwa kukusanya sh milioni 40 kutokana na faini pamoja na ukusanyaji wa madeni.
  Zoezi hilo ambalo ni endelevu linatarajia kukamata watu zaidi ili kuweza kufidia hasara ambayo shirika limepata  kutokana na wizi huo.Tanesco hukusanya mapato mengi zaidi ya 80% kutoka kwa watumiaji wakubwa waumeme ambao ni 20% ya wateja wote ambako ndiko walikoazia kufanya udhibiti wa ufungaji wa vifaa hivyo maalum vya kuzuia wizi huo.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru