NYUMBA, KUTA ZA MABILIONI ZILIZOJENGWA UFUKWENI, MMOJA AKIMBILIA KORTINI KUZUIA JUMBA LAKE LA SH1.5 BILIONI
Posted on
Jul 10, 2012
|
No Comments
SERIKALI jana ilikunjua makucha yake kwa vigogo waliojenga nyumba za kifahari kando ya Mito ya Mbezi Beach, Mndumbwe na eneo la Hifadhi ya Mikoko, Dar es Salaam baada ya kuzibomoa katika operesheni iliyosimamiwa na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha Jeshi la Polisi.
Hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa tamko la Makamu wa Rais la mwaka 2004 ambalo lilitaja maeneo tengefu ambayo yalipaswa kuhifadhiwa zikiwamo fukwe za bahari ambazo zina mikoko ambayo ni mazalia ya samaki baharini. Licha ya tamko hilo na sheria mbalimbali, bado maeneo ya fukwe za bahari yamekuwa yakivamiwa.
Katika kusimamia sheria na tamko hilo, Wizara ya Maliasili na Utalii, Kitengo cha Hifadhi ya Misitu, Baraza la Taifa la Kuhifadhi Mazingira (NEMC) na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, ziliamua kuratibu bomoabomoa hiyo ya nyumba za kifahari zilizojengwa maeneo tengefu ya bahari
Hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa tamko la Makamu wa Rais la mwaka 2004 ambalo lilitaja maeneo tengefu ambayo yalipaswa kuhifadhiwa zikiwamo fukwe za bahari ambazo zina mikoko ambayo ni mazalia ya samaki baharini. Licha ya tamko hilo na sheria mbalimbali, bado maeneo ya fukwe za bahari yamekuwa yakivamiwa.
Katika kusimamia sheria na tamko hilo, Wizara ya Maliasili na Utalii, Kitengo cha Hifadhi ya Misitu, Baraza la Taifa la Kuhifadhi Mazingira (NEMC) na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, ziliamua kuratibu bomoabomoa hiyo ya nyumba za kifahari zilizojengwa maeneo tengefu ya bahari
Bomoabomoa hiyo ambayo iliendeshwa chini ya ulinzi mkali wa polisi wa FFU chini ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela na kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa NEMC, Dk Robert Ntakamulenga, jumla ya nyumba 27 kati ya hizo 15 zikiwa zimekamilika ujenzi, nane uzio (fence) na nyingine katika hatua za awali za ujenzi, zilibomolewa.
Kazi ya kubomoa nyumba hizo iliyofanywa na kampuni ya Majembe Auction Mart, ilianza huku wakazi wa nyumba hizo wakiwekwa chini ya ulinzi mkali wa FFU na polisi wengine waliokuwa wamesheheni mabomu ya machozi, bunduki na gari la kumwaga maji ya kuwasha.
Bomoabomoa hiyo ilianzia katika eneo la Hifadhi ya Mikoko, Mbezi Beach mnamo saa 2:00 asubuhi na watu waliokuwa wakiishi katika nyumba hizo walilazimika kutoa vitu vyao nje huku kububujikwa machozi.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo na Mchungaji wa Kanisa la Dar es Salaam Christian, George Makala alisema kitendo hicho kinasikitisha kwa kuwa muda uliotolewa kwao ni mdogo na wasingeweza kujiandaa kuhama.
Akizungumzia tukio hilo muda mfupi baada ya kubomolewa nyumba yake na kanisa hilo, Mchungaji huyo alisema kitendo hicho hakikufuata taratibu na kimesababisha hasara ya mali nyingi kwa wakazi wa eneo hilo akisema kama wangeachwa wahame zingeokolewa.
“Ninasikitika sana kwani kitendo hiki hakikufuata taratibu, alikuja Waziri wa Nyumba, Ardhi na Makazi Profesa Anna Tibaijuka, Mbunge wetu, Halima Mdee na Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuf Mwenda wakatuambia eneo hilo siyo la hifadhi, bali ni hatarishi, sisi tuliwaambia tuna uwezo wa kukabiliana nalo ndipo waziri aliposema atatoa tamko,” alisema Mchungaji Makala na kuongeza:
“Tukiwa tunasubiri tamko kutoka kwa waziri na vibali tunavyo, tumeshangaa (juzi) Jumapili tunaamka na kukutana alama za X. Hatukujua nani ameweka, leo (jana) ghafla tunashangaa tingatinga zimekuja na kubomoa.”
Alisema walichofanyiwa siyo haki kwa sababu hawakupewa muda wa kujiandaa kutafuta mahali pa kuhamia lakini pia wangebomoa nyumba zao kuokoa mali zao.
“Kwa sasa tutawasiliana na mwanasheria wetu kuona kama kuna uwezekano wa kuchukua hatua ili twende mahakamani, lakini hilo litategemea nini mwanasheria atatushauri,” alisema Makala.
Wananchi washangilia
Wakati Mchungaji Makala akielekeza kilio chake kwa waratibu wa shughuli hiyo, baadhi ya watu waliofika kushuhudia tukio hilo waliisifu Serikali wakisema sheria sasa imeanza kufanya kazi.
Mmoja wa wakazi hao, Samuel Laizer alisema kilichofanywa sasa na Serikali kinaonyesha kuwa sasa inafanya kazi na hakutakuwa na mtu atakayekuwa juu ya sheria.
“Tukio hilo limenifurahisha sana, tumezoea kuona Serikali ikituonea sisi maskini, lakini kitendo cha kubomoa nyumba hata za vigogo waliovunja sheria, sasa tunaamini watu wote tutakuwa sawa,” alisema Laiser.
Katika eneo la Mto Mbezi Beach, kikosi hicho cha ubomoaji kilivunja kuta kadhaa zilizokuwa zimezungushwa katika viwanja saba vilivyokuwa karibu na mto huo pamoja na Mto Mndumbe inayomwaga maji katika Bahari ya Hindi.
Mwanasheria wa NEMC, Manchare Heche alisema baadhi watu wanaomiliki viwanja hivyo waliendelea kujenga majumba ya kifahari licha ya zuio hilo lilitolewa zaidi ya mara tatu.
Heche pia alisema bomoabomoa hiyo ilikuwa iikumbe moja ya nyumba ya kifahari katika Mto Mbezi lakini mmiliki wake ameweka pingamizi katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi. Kwa mujibu wa watu waliokuwa katika eneo hilo, nyumba hiyo inakadiriwa kuwa na thamani ya Sh1.5 bilioni.
Akizungumzia shughuli hiyo ya jana, Kaimu Mkurugenzi Usimamizi Rasilimali na Wakala wa Huduma za Misitu, Zawadi Mbwambo alisema kazi hiyo imechelewa kutokana na kuhusisha idara, wizara na taasisi tofauti katika utendaji wake.
Alisema kazi hiyo itakuwa endelevu na itawahusu watu wote waliojenga katika maeneo ya fukwe za bahari na kusisitiza kuwa umbali unaoruhusiwa kujenga nyumba kutoka eneo la bahari ni meta 60.
Kwa upande wake, Dk Ntakamulenga alisema kazi hiyo ya kubomoa nyumba katika maeneo ya hifadhi za taifa, fukwe za bahari na kando ya mito ni endelevu na akatoa wito kwa watu wote waliojenga katika maeneo hayo kuchukuka tahadhari mapema kuondoa usumbufu.
“Tumechelewa kuchukua hatua kutokana na zoezi hili kushirikisha mamlaka zaidi ya mmoja, tulikutana kujadili na kuona umuhimu wa kuunganisha nguvu ili utekelezaji wake usiingilie mamlaka nyingine,” alisema Dk Ntakamulenga.
Alisema kazi hiyo pindi itakapomalizika katika jiji la Dar es Salaam ambako kuna viwanja zaidi ya 100, vinavyopaswa kurudishwa katika mamlaka husika, itahamia mikoani na itawahusu pia watu wote waliojenga nyumba zao kwenye hifadhi za taifa, kando ya mito na kwenye fukwe za bahari kitendo kinachosababisha uharibifu wa mazingira.
Polisi Kinondoni yatoa onyo
Kamanda Kenyela aliwataka watu wote waliojenga nyumba zao katika maeneo yanayokatazwa na Serikali, kuzibomoa wenyewe ili kukwepa mkono wa sheria.
“Tukio la leo ni kwamba tumewasha taa, sasa watu wote waliojenga nyumba zao kinyume na sheria katika jiji la Dar es Salaam na hata wenye migogoro ya ardhi ambao Mahakama ilishatoa hukumu ni vyema wakabomoa wenyewe, watii sheria pasipo shuruti,” alisema.