MSINGI DHAIFU MADARASA YA AWALI CHANZO CHA WASIOJUA KUSOMA NA KUANDIKA
Posted on
Aug 16, 2012
|
No Comments
Baadhi ya shule za msingi ndio kwanza zinajenga madarasa ya awali. Hili ni darasa la awali la shule ya msingi Kitopeni Korogwe.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lwengera Darajani, Youze Mbwambo akionesha jengo ambalo ni nyumba ya mwalimu ambayo inatumika kwa muda kama darasa la awali.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Silabu Mizeki Charahani (kulia) akimtembeza mwandishi wa Thehabari.com (hayupo pichani) kuangalia mazingira ya shule hiyo alipotembelea shule hiyo. Silabu ni moja ya shule zisozokuwa na madarasa ya awali Wilaya ya Korogwe.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lwengera Darajani, Youze Mbwambo akizungumza na mwandishi wa Thehabari.com Korogwe, Tanga. Shule hii haina darasa la awali.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Boma wilayani Korogwe Amir Nassoro akifanya mahojiano na Thehabari hivi karibuni.
Mhariri Mkuu wa Thehabari akifanya mahojiano na baadhi ya wakazi wa Lwengera Darajani wilayani Korogwe.
MSINGI mbovu na dhaifu wa elimu kwa madarasa ya awali umebainika kuwa chanzo cha baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi mkoani Kilimanjaro na Tanga kumaliza elimu hiyo huku hawajui kusoma na kuandika.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni katika Wilaya ya Moshi (Manispaa) umebaini idadi kubwa ya shule za msingi awali hazikuwa na madarasa ya awali kwa ajili ya kuwaandaa wanafunzi kujiunga na darasa la kwanza, jambo ambalo liliilazimu shule kupokea wanafunzi wa darasa la kwanza toka nje ya shule wengine wakiwa hawajaandaliwa kikamilifu.
Taarifa zimebaini vituo vingi vya shule za awali ambavyo baadhi ya shule za msingi zilikuwa zikitegemea kupokea watoto wa darasa la kwanza vilikuwa havina walimu wenye taaluma ya kuwaandaa watoto katika vituo hivyo kwa ajili ya kujiunga na darasa la kwanza.
Uchunguzi uliofanyika katika baadhi ya shule za katikati ya Mji wa Moshi (Manispaa) na pembezoni umebaini shule nyingi hivi sasa zimeanzisha madarasa ya awali ikiwa ni shinikizo la Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi la miaka ya hivi karibuni.
Shule ya Msingi Magereza ni miongoni mwa shule zinazofanya vibaya katika Manispaa ya Moshi, shule hii inashika nafasi ya 45 kiwilaya kati ya shule 46 za manispaa nzima. Kimkoa inashika nafasi ya 595 kati ya shule 638 japo ipo mjini ukilinganisha na zile za vijijini.
Akizungumza mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Magereza alisema awali haikuwa na darasa la awali bali ilikuwa ikipokea wanafunzi wa darasa la kwanza kutoka nje ya shule. Alisema ilianzisha darasa la awali rasmi linaloendeshwa na shule hiyo Machi 1, 2012.
Taarifa zaidi zimebaini licha ya madarasa mengi ya shule za awali kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambao huwa mzigo kwa mwalimu mmoja anayefundisha, mengi ya madarasa hayo yana umri kati ya miaka mitatu kushuka chini jambo ambalo linaonesha mafanikio yake hayajaanza kujitokeza.
Hata hivyo hali hiyo imejitokeza katika Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, kwani kati ya shule nne za msingi Silabu, Lwengera, Kitopeni na Boma ambazo mwandishi amezitembelea ni moja tu (Boma) ndio yenye darasa maalumu la wanafunzi wa awali. Uchunguzi umebaini kuwepo na shule zenye wanafunzi wa awali lakini hakuna vyumba vya kufundishia wala waalimu wenye sifa ya kufundisha kitengo hicho muhimu.
Akizungumza Ofisa Elimu Taaluma, Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Elius Mkwizu alisema kwa eneo lao bado suala la vyumba vya madarasa ni tatizo hivyo idara hiyo inajitahidi kulishughulikia suala hilo kwa kushirikiana na wazazi wa maeneo husika.
Kwa upande wake Kaimu Ofisa Elimu Manispaa, Leocadia Akaro alisema idara yao inajitahidi kuhimiza ujenzi wa madarasa ya awali na mafanikio ni makubwa kwani idadi kubwa ya shule za msingi zinamadarasa ya awali tofauti na ilivyokuwa hapo nyuma.
*Habari hii imeandaliwa na kuletwa hapa na Mtandao wa www.thehabari.com kwa ushirikiano na taasisi ya HakiElimu