Sehemu ya Mabango yakiwa yamebebwa na Vijana wa UVCCM Wakati wa Mapokezi ya Viongozi wapya wa UVCCM Jijini Dar es Salaam Jana
Picha juu ni jinsi UVCCM walivyowapokea viongozi wao wapya - kwa mabango na kichapo katika ofisi za Makao Makuu ya Umoja huo jana.
Wanachama wa Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM), wanaomuunga mkono
Mwenyekiti mpya wa Taifa wa Umoja huo, Khamis Sadifa Juma na viongozi
wenzake, wakimtwanga mmoja wa wanachama waliojitokeza kumpinga
mwenyekiti huyo kwa mabango (wa pili kushoto), wakati alipowasili makao
makuu ya umoja huo Dar es Salaam jana, akitokea mkoani Dodoma
alipochaguliwa kushika nyadhifa hiyo. Picha na Rafael Lubava -
----
SHAMRASHAMRA za kumpokea Mwenyekiti mpya
wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) , Khamis Sadifa Juma
jijini Dar es Salaam jana ziligeuka uwanja wa vita baada ya makundi
yanayopingana kuchapana makonde.
Tafrani hiyo ilianza baada ya
kundi moja la vijana waliokuwa wanane kutokea likiwa na mabango
yaliyokuwa na ujumbe wa kupinga ushindi wa mwenyekiti huyo, wakati
utambulisho wa ugeni huo ukiendelea katika ofisi za makao makuu ya
UVCCM, zilizopo jijini Dar es Salaam.
Baada ya kundi hilo
kujitokeza na mabango yao, ndipo vijana wa upande wa Mwenyekiti (Juma),
walipoanza kuwakimbiza na kufanikiwa kuwakamata
Kukiwa hakuna msaada wa Polisi, vijana hao walilishambulia kundi hilo
kwa muda, huku baadhi yao wakitiwa nguvuni na vijana hao na kuingizwa
katika ofisi ya UVCCM huku waandishi wa habari wakizuiwa kuwahoji
watuhumiwa wala kuingia ndani ya ofisi hiyo.
‘’Hatutaki waandishi
humu ndani, tokeni na asiingie mtu, hawa tutashughulika nao wenyewe,
wanatusumbua mno hawa kwa siku nyingi,” alisikika mmoja wa vijana hao
akiongea kwa sauti ya juu.
Baada ya purukushani hizo zilizodumu kwa
zaidi ya nusu saa, hali ya hewa ilitulia na ratiba iliendelea huku
vijana wengine wanaomuunga mkono mwenyekiti wao wakichukua jukumu la
kulinda usalama wa eneo hilo na kuwapeleka Kituo cha Polisi Mnazi Mmoja
vijana wawili waliowakamata kwa mahojiano.
Mwenyekiti mpya wa UVCCM alitamba kuwa atapambana na watu wanaotaka kuvuruga umoja huo.
Alisema: “Mimi ni mwanajeshi nimekaa kwenye kambi nyingi za jeshi, hivyo naelewa nitakavyopambana nao.”
Viongozi wa Kitaifa
Hata hivyo, sherehe hizo hazikuhudhuriwa na kiongozi yeyote wa kitaifa wa CCM.
Akizungumza
baada ya mapokezi hayo, Mwenyekiti wa UVCCM Taifa aliwataka vijana
kuwa na umoja akisema kuwa uchaguzi umekwisha na kilichobaki ni kujenga
chama na kuhakikisha CCM inashinda katika chaguzi zote.
‘’Kilichobaki
sasa ni kujenga chama, haipendezi kuendeleza uhasama ndani ya chama,
sisi sote ni wamoja na tuache makundi kwani nayachukia na kuwachukia
wale wanaoanzisha na kuendeleza makundi,’’ alisema Khamis Sadifa Juma.
Wiki
iliyopita, baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa UVCCM mjini
Dodoma, kundi la vijana kutoka mikoa mbalimbali walikutana na waandishi
wa habari na kulalamika kwamba rushwa ilitawala uchaguzi huo, huku
wakiwatuhumu viongozi wa UVCCM na baadhi makada wa chama hicho kwa
kuhusika na vitendo hivyo.
Waliotajwa ni pamoja aliyekuwa makamu mwenyekiti wa umoja huo, Beno
Malisa, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela, Bashe na mtoto wa Lowassa,
Fredy.
“Kama Rais Jakaya Kikwete kweli yuko makini na kauli zake
ni za dhati, basi atengue matokeo ya uchaguzi huu maana kanuni
zimekiukwa na kusema kweli rushwa ilitawala. Atumie nafasi yake
kurejesha hadhi ya chama kwani huu uchaguzi ni batili,” alisema Mjumbe
wa Mkutano Mkuu wa CCM kutoka Morogoro, Augustine Matefu.
Walidai
kuwa Bashe, ndiye aliyekuwa mratibu wa uingizaji wa fedha katika eneo
la mkutano ambazo zilitumika kugawanywa kwa wajumbe na kwamba Malisa na
Shigela waligawa Sh1 milioni kwa viongozi wa mikoa kama hatua ya
kumpigia kampeni mmoja wa wagombea walioshinda.
Hata hivyo, Bashe
alikanusha tuhuma hizo akisema siyo kweli na kuongeza: “Mimi sijatumwa
na Lowassa, wala sifanyi kazi na Lowassa. Nafanya kazi ya CCM, lakini
nampenda sana Lowassa kwa sababu ni mmoja wa viongozi na makada wa
chama, ambao wameonyesha mapenzi ya dhati kwa CCM na uvumilivu wa hali
ya juu.”
Kada mwingine, Livamba Adinan Selemani alisema: “Vijana
kweli tumempuuza Rais, kweli mtu ambaye hana hela hawezi kupata uongozi
UVCCM, kwa maana nyingine nchi yetu inakwenda pabaya. Watu wachache
wenye fedha wanaweza kuamua kufanya wanachotaka, hivyo ndivyo uchaguzi
wetu wa vijana ulivyokuwa.”
Mjumbe mwingine, Kichanta Selemani
alisema malalamiko ya viongozi wa UVCCM kuwapendelea baadhi ya wagombea
yalifikishwa kwa Lukuvi lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.
Wakati makada hao wa CCM wakizungumza na waandishi wa habari,
lilitokea kundi jingine la makada wa chama hicho ambao walianza kuzozana
na wenzao wakisema kuwa malalamiko yao yanatokana na kushindwa na
kwamba walitaka kutumia “Viongozi wa ngazi za juu za CCM” kuwachagulia
vijana viongozi.