photo NAAZ_zpsd0bbd510copy_zps37715af5.jpg
 photo NAAZ_zpsd0bbd510.jpg
Nafasi Ya Matangazo
> > ZITTO KABWE; TUTAWEKA WAZI MAJINA YA WATANZANIA WENYE AKAUNTI USWISS KWA UTARATIBU NA UMAKINI.

ZITTO KABWE; TUTAWEKA WAZI MAJINA YA WATANZANIA WENYE AKAUNTI USWISS KWA UTARATIBU NA UMAKINI.

Posted on Oct 28, 2012 | No Comments

Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe
---
Kwa nchi za wenzetu magazeti ya uchunguzi yanafanya kazi hizi. Kwetu magazeti yanasubiri wanasiasa wafanye. Orodha ya Watanzania wenye akaunti Uswiss inakuja. Hoja Binafsi kuhusu suala hili imeruhusiwa na sasa naandaa maelezo ya Hoja. Sio suala la kutaja orodha tu bali pia hatua za kuchukua dhidi ya fedha hizo na wenye fedha haramu zilizofichwa huko.

Zitto Kabwe Kuna baadhi ya Watanzania wenzangu wanabeza kazi hii. Ninachowaambia sitakata tamaa. Ninaifanya kazi hii kwa umakini mkubwa kwa kuwa najua uhatari wake. Sikurupuki tu. Ninafanya kazi hii kwa niaba ya Kambi ya Upinzani nikiwa Waziri kivuli wa fedha. Hii ni kazi ya CHADEMA, sio kazi ya Zitto. Wengine wanasema mbona 'list of shame' tulitaja majina. Ni kweli. Lakini ilituchukua wiki kadhaa kutaja majina. Katika mkutano wa Jangwani wakati napokelewa kutoka Bungeni baada ya kusimamishwa ubunge kufuatia hoja ya Buzwagi, tuliahidi mbele ya umma kutaja orodha ya mafisadi. Tukataja wiki 3 baadaye mnamo Septemba 15, 2007. Tulifanya kazi ile kwa umakini sana. Tutaifanya kazi hii ya Watanzania wenye akaunti huko uswiss kwa umakini zaidi.

Tutaweka wazi majina ya Watanzania wenye akaunti Uswiss kwa utaratibu na umakini. Nitataja orodha hiyo Bungeni na kamwe sitataja nje ya Bunge. Hii ni kazi kubwa inahitaji utulivu. ” ~ Zitto Kabwe

---
Habari kamili na Rodrick Mushi, Rombo
 
  
WAKATI serikali ikishindwa kuwataja vigogo walioficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, anatarajia kuwasilisha hoja binafsi katika mkutano wa tisa unaotarajiwa kuanza wiki ijayo mjini Dodoma, kutaka serikali irejeshe fedha hizo.

Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, amesema tayari hoja hiyo imeshapata baraka za Spika wa Bunge, Anne Makinda.

Mbunge huyo wa CHADEMA alisema hayo jana wakati wa akifunga mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Nanjarareha, wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro.
Katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika leo, CHADEMA imemsimamisha, Frank Salakana. Alisema sh bilioni 349 zilizofichwa Uswisi na baadhi ya vigogo wa serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), lazima zirejeshwe nchini, huku akimtaka Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea, kueleza umma barua aliyoituma nchini humo kwa ajili ya kashfa hiyo ilikuwa na lengo gani.

Alisema barua ya Dk. Hosea imesababisha ugumu wa upatikanaji wa taarifa za mabenki ya nchini Uswisi ambayo yameshindwa kutoa ushirikiano kwa kamati inayofuatilia kashfa hiyo.
Huku akishangiliwa na maelfu ya wanachama wa CHADEMA waliofurika kusikiliza mkutano huo, Zitto alisema wizi wa mabilioni hayo umetokana na kuporomoka kwa maadili ya viongozi nchini ambao wengi wanajali zaidi masilahi binafsi badala ya umma.

Mbunge huyo machachari wa CHADEMA, alisema kuna haja kama taifa kurejesha maadili ya uongozi kama enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere ili viongozi wachague kitu kimoja, kati ya biashara na siasa.
Alisema CHADEMA imepania kuhakikisha mabilioni hayo yanarejeshwa ili yaweze kutumika kuwasaidia Watanzania katika kujenga na kuboresha miundombinu ya barabara, maji na afya.

Aliwataka viongozi walioficha mabilioni hayo kujitokeza mapema na kueleza jinsi walivyozipata badala ya kusubiri kuumbuliwa.

“Nawataka viongozi waliohusika wajitokeze wenyewe, waeleze walivyozipata na kisha wazirejeshe nchini, vinginevyo patachimbika, kwani nitahakikisha kama chama tunashirikiana na Benki ya Dunia kuhakikisha fedha hizo zinarudi nchini,” alisema Zitto.

Alisema CHADEMA inapigania fedha hizo zirejeshwe kwani zimetokana na wizi wa rasilimali za Watanzania kupitia mikataba mibovu ya mafuta na wizi wa madini na nyingine.

Katika ripoti ya Swiss Central Bank, iliyotolewa hivi karibuni, inaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 11 barani Afrika ambazo vigogo wake wa kibiashara, kitawala na kisiasa wameficha kwa siri mabilioni ya fedha katika mabenki ya Uswisi.

Nchini nyingine za Afrika zilizoficha fedha hizo ni Kenya, Uganda, Zimbabwe, Misri, Shelisheli, Afrika Kusini, Rwanda, Sierra Leone, Somalia na Sudan.

Kwa upande wa Tanzania, mapesa ambayo yamefichwa huko ni dola milioni 196.87, sawa na shilingi za Tanzania bilioni 315.5!

Hebu jiulize; mapesa haya tuliyoibiwa yangetusaidia kiasi gani kama yangerejeshwa nchini na kutumbukizwa kwenye miradi ya kuboresha huduma za jamii?

Pia jiulize swali jingine: Je, hata baada ya Benki Kuu ya Uswisi kuturahisishia mambo kwa kututobolea ukweli kwamba tumeibiwa, na kwamba wezi wetu wameficha hizo fedha nchini mwao, watawala wetu wana dhamira ya kuanzisha mchakato ili wahusika wafikishwe mahakamani na fedha hizo zirejeshwe nchini?

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru