photo NAAZ_zpsd0bbd510copy_zps37715af5.jpg
 photo NAAZ_zpsd0bbd510.jpg
Nafasi Ya Matangazo
> > HAWA NDIYO VIGOGO CCM WANAWEZA KUWANIA URAIS 2015

HAWA NDIYO VIGOGO CCM WANAWEZA KUWANIA URAIS 2015

Posted on Feb 15, 2013 | No Comments

 
UCHAGUZI wa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) uliofanywa na Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho Jumatatu wiki hii mjini Dodoma, ni kama unabadili mwelekeo wa siasa za ndani za chama hicho kikongwe nchini.
Tangu Rais Jakaya Kikwete aingie madarakani miaka saba iliyopita na kupewa kofia ya uenyekiti wa CCM, chama hicho kimekuwa kwenye minyukano ya siasa za visasi kiasi kwamba hakijawahi kuwa na utulivu wa kisiasa kama ilivyo sasa, miezi michache baada ya kufanyika mabadiliko kadhaa ya kiuongozi.
Uteuzi na baadaye uchaguzi wa wajumbe wa Kamati Kuu umeweka kando baadhi ya vigogo wa kisiasa hasa waliokuwa wakitajwa katika harakati za kuusaka urais katika uchaguzi wa 2015 na kuziingiza sura mpya ambazo huenda baadhi yao wanaweza kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ni vigogo ambao wamekuwa wakitajwa kupiga mbio hizo, lakini waliwekwa kando katika     Kamati Kuu ya sasa.
Pia majina ya mawaziri na wizara zao kwenye mabano Profesa Mark Mwandosya (Ofisi ya Rais – Kazi Maalumu), Dk John Magufuli (Ujenzi), Dk Harrison Mwakyembe (Uchukuzi) pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela, pia hayakuwa sehemu ya waliopendekezwa kuingia katika CC ambacho ni chombo cha kufanya uamuzi mkubwa ndani ya CCM.
Profesa Mwandosya licha ya kuwa na matatizo ya kiafya, amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa watu muhimu katika mustakabali wa siasa za sasa za Tanzania wakati Dk Magufuli na Dk Mwakyembe wamekuwa wakipigiwa chapuo na umma kwamba huenda wangefaa kuwania urais kutokana na kasi katika utendaji kwenye wizara wanazoziongoza.
Badala yake Kamati Kuu inawajumuisha makada ambao siyo wapya, lakini ambao wanaweza kutumika kubadili sura na mwelekeo wa siasa ndani ya CCM hasa tunapoelekea 2015, akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Dk Salim Ahmed Salim.
Hatua hiyo inaweza kuwa ni hatua ya kujaribu kujipanga kwa CCM katika kuzipa sura mpya siasa za ndani ya chama hicho. Dk Salim kama ilivyo kwa Profesa Mwandosya, alikuwa mpinzani wa Kikwete katika kinyang’anyiro cha urais wa 2005, ambaye bado anatizamwa kuwa mtu mwenye uwezo licha ya kwamba umri wake ni mkubwa.
Wengine ambao kuingia kwao katika Kamati Kuu ya CCM kunaweza kuwa na maana ya kubadili siasa za urais ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi na mwenzake kutoka Tanzania Visiwani ambaye alipata kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Shamsi Vuai Nahodha.
Dk Nchimbi anarejea Kamati Kuu ambako aliingia kwa mara ya kwanza akiwa na umri mdogo pale alipochaguliwa kuongoza Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na kuongoza jumuiya hiyo kwa miaka kumi mfululizo. Kwa mujibu wa kanuni za CCM, wenyeviti wa jumuiya za chama huwa ni wajumbe wa CC kwa mujibu wa nyadhifa zao.  Nchimbi amekuwa mjumbe wa CC kwa miaka 10.
Hali kadhalika, Dk Mwinyi ni mmoja wa makada wa CCM ambaye amekuwa ndani ya CC kwa muda mrefu, wakati Nahodha alikuwa akiingia ndani ya kamati hiyo alipokuwa Waziri Kiongozi wa SMZ (kwa wadhifa wake).
Nahodha, Dk Mwinyi na Dk Nchimbi kwa nyakati tofauti wote wamepita katika wizara nyeti ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Dk Mwinyi wakati alipokuwa waziri, naibu wake alikuwa Dk Nchimbi ambaye baadaye alihamishiwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na sasa Mambo ya Ndani.


Dk Nchimbi alichukua nafasi ya Nahodha ambaye sasa yupo ulinzi.
Mwingine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Sera na Uratibu), Steven Wassira ambaye katika siku za karibuni ametokea kuwa moja ya nguzo kuu za CCM katika kujibu hoja mbalimbali ndani na nje ya Bunge, kusuluhisha migogoro ya kichama na kupambana na wapinzani wakuu wa chama chake, ambacho ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Wassira aliongoza kwa kupata kura nyingi miongoni mwa makada wa CCM waliochaguliwa kuwa wajumbe wa NEC kupitia uchaguzi wa kitaifa, lakini amekuwa akitajwa kwamba ni mmoja wa wanaokusudia kuchukua fomu za urais katika uchaguzi wa 2015.
Katika mazingira ya kawaida hii ni CC mpya ya mwisho kuundwa na Rais Kikwete akiwa Mwenyekiti wa CCM kwani ndiyo inayotazamiwa kukivusha chama hicho katika kinyang’anyiro cha 2015 ambacho yeye hatogombea kwani atakuwa amemaliza muda wake.
Umekuwa ni utaratibu wa CCM kwamba ni vigumu kumteua mgombea urais ambaye si mjumbe wa Kamati Kuu na kitendo cha baadhi ya vigogo wa kisiasa kuwekwa kando kunaweza kutafsiriwa kwamba ni kuwaweka kando katika kuwania nafasi hiyo na kuwapa fursa makada wengine ambao wanaonekana kuwa ‘watulivu’.
Licha ya kwamba Rais Kikwete ni mwenyekiti, lakini uwapo makamu wake, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kunakipa nguvu chama hicho kuendeleza utulivu uliopo na kupitia kwao, CCM wanaweza kufanya uamuzi mgumu ambao utawashangaza wengi kwa kumteua mgombea ambaye hafikiriwi na wengi kupeperusha bendera ya chama hicho.Pia aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha-Rose Migiro ambaye ameteuliwa hivi karibuni katika sekretarieti mpya, naye amekuwa akitajwa kwamba huenda akachukua fomu ya kugombea urais katika chama hicho.
Kwa upande wa Dk Mohammed Shein naye huenda akachukua fomu ya kugombea urais wa Muungano baada ya kuweza kufanya kazi na upinzani bila ya mikwaruzo mikubwa huko Zanzibar. Hata hivyo, CCM kama itatupa karata yake kwa Dk Shein itabidi kufanya kazi ya ziada kumnadi.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru