NDOLANGA: WAMBURA NENDA MAHAKAMANI.
Posted on
Feb 16, 2013
|
No Comments
Ndolanga aliyasema hayo alipozungumza na Mwanaspoti kuhusu mustakabali wa soka la Tanzania na mchakato mzima wa uchaguzi wa TFF ambao amedai kuwa umevurugwa na Kamati ya Rufaa ambayo alisema inapaswa kuomba radhi. "Mchakato wa uchaguzi umejaa matatizo mengi, inapotokea watu wenye nguvu sawa au mmoja ana nguvu zaidi ya mwenzake halafu akaenguliwa kinachofuata ni mgombea bandia kwa kuwa anataka wenzake wakatwe ili apite kirahisi, alisema. Mmoja wa wagombea walioenguliwa, Michael Wambura aliyekuwa akiwania nafasi ya Makamu wa Rais amenukuliwa akielezea nia yake ya kupeleka suala hilo mahakamani kupinga kuenguliwa kwa Jamal Malinzi anayewania nafasi ya urais. "Kamati ya rufaa ni kiina macho, waliitengeneza kwa maslahi yao binafsi, mimi nasema mchakato si shwari hata kidogo, unamkata mtu lazima uwe na sababu za kutosha, mwaka 2008 huyo waliyemkata alishindana na Tenga mmoja akashinda mmoja akashindwa na hali ilikuwa shwari alisema. "Hivi wanachohofia nini mpaka wanakata kata watu hovyo, haki itapatikana mahakamani, uchaguzi utasimama na sisi tutaendelea kucheza mpira, alisema. Alipoulizwa kuhusu agizo la FIFA kutotaka masuala ya soka kupelekwa mahakamani Ndolanga alisema: FIFA sasa hivi msimamo wao suala la uchaguzi ni la ndani turekebishe kwanza ujinga wetu humu ndani sisi wenyewe, tuondoe uozo, wajumbe wa mkutano mkuu wanajua wanamtaka nani na kwa sababu zipi sasa hii kukatakata majina inanipa mashaka sana. "Kamati inalinda watu wachache, mahakamani pekee ndio haki inapatikana, binafsi nilishawahi kwenda mahakamani ila kwanza niliitaarifu FIFA nakwenda mahakamani nimenyimwa haki yangu, wakaniambia usiende, nikawaambia naenda kwa vile nadai haki, wakaniambia kama unaenda tuhakikishie kuwa utashinda, nikawajibu suala la kushinda au kutokushinda ni mambo ya sheria. "Bahati nzuri nilishinda na nikarudishwa kugombea nikashinda nikaongoza mwaka mmoja, ninachotaka kusema hapa kufungiwa sio issue, issue ni kutoa haki, usichukue suala la fifa kama ngao ya kuwanyima watu wengine haki, alisema Ndolanga ambaye mwaka 1996 alikwenda mahakamani kupinga kuenguliwa na Baraza la Michezo la Taifa kuwania uongozi wa FAT. "Fifa wawepo wasiwepo mahakamani ni lazima watu waende, hizi kamati kamati ambazo zimeundwa kwa ajili ya kunyima watu haki zao, mchakato umechafuka, tunachafua sifa ya nchi kwa sababu ya ubinafsi lazima Kamati ya Rufaa irejeshe heshima yake kwa kuwarejesha kwenye kinyang'anyiro walioenguliwa. "Wamekosea wawe wajasiri kuomba samahani uchaguzi uendelee, kwani hata hao waliokaa miaka zaidi ya mitano hatujacheza AFCON, wala Kombe la Dunia na wana uzoefu,alisema. Kauli ya Ndolanga imekuja siku chache baada ya kamati ya rufaa chini ya Mwenyekiti wake, Idd Mtiginjola kumuengua Malinzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Kagera (KRFA), Jamal Malinzi kwa madai ya kukosa uzoefu wa miaka mitano. Hata hivyo tayari Malinzi alishaweka wazi msimamo wake kuwa hakubaliani na kuenguliwa kwake na kumtaka Rais wa TFF, Leodegar Tenga kuingilia kati suala hilo kwa kumrejeshea haki yake ya kugombea. |