MANDAMANO YATIKISA JIJINI DAR ES SALAAM, ZAIDI YA WATU 90 KUTIWA MBARONI.
Posted on
Feb 16, 2013
|
No Comments
SHUGHULI katika Jiji la Dar es Salaam jana
zilisimama kwa muda baada ya wafuasi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Issa Ponda, kuandamana huku
wakipambana na askari polisi waliotanda katika maeneo mengi ya mji.
Wafuasi hao waliotawanywa mara kwa mara na kwa
mabomu ya machozi na askari polisi, walitumia stali mpya kuandamana hadi
kwenye Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kufikisha ujumbe
wao.
Vurugu hizo za polisi kupambana na waandamanaji
hao zilianza mchana baada ya swala ya Ijumaa hadi saa 9:00 alasiri huku
mitaa mingi katika jiji la Dar es Salaam ikiwa wazi kutokana na watu
wengi kuondoka maeneo hayo.
Watu hao waliandamana kushinikiza Ponda ambaye yupo ndanmi akikabiliwa kesi ya wizi na uvunjifu wa amani ashiwe kwa dhamana.
Watu hao walitokea katika misikiti mbalimbali ya
Jiji la Dar es Salaam baada ya swala ya Ijumaa ikiwemo, Kwamtoro,
Magomeni na Buguruni kuelekea ofisi za DPP zilizopo barabara ya Ohio na
Sokoine eneo la posta wakiwa katika vikundi vidogovidogo, tofuati na
mandamano ambayo yamezoeleka kufanyika.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar
es Salaam inawashikilia zaidi ya watu 90 ambao walishiriki kuhamasisha
na kufanya maandamano.
Kaimu wa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Mohamed Msangi alisema kati ya watu hao watawahoji ili kuwabaini
wahusika wakuu na kufikishwa mahakamani.
“Kama inavyofahamika wazi kwenye msafara wa mamba
kenge hawakosekani sasa tutawahoji ili tuweze kuwapata wahusika wakuu
na tuweze kuwachukulia hatua za kisheria kwani hao ni wavunjifu wa
amani,”alisema.
Msangi alisema jeshi hilo lilipiga marufuku
maandamano hayo lakini watu hao wamekaidi amri hiyo na kwamba sasa
watachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema kulikuwa na vikundi vya watu katika maeneo
ya Buguruni, Mnazi Mmoja na Kariakoo ambao walikuwa katika makundi huku
wengine wakiandamana katika makundi
“Tumeweza kuchukua hatua kwa watu waliyokuwa
wanataka kujaribu kuvunja amani kwa kufanya maandamano kwani
tumedhibiti hali hiyo na kuweza kuwakamata watu 80 ambao wapo katika
kituo cha Polisi Kati na Msimbazi,”alisema Msangi.
Alisema hali sasa ni shwali na kwamba vurugu ambazo zilitaka kujitokeza zimedhibitiowa.