RAIS WA KENYA KUWASILI LEO NCHINI
Posted on
Feb 20, 2013
|
No Comments
RAIS Mwai Kibaki
RAIS Mwai Kibaki wa Kenya, leo anaanza ziara ya siku mbili nchini ikiwa ni wiki mbili tu kabla ya taifa lake kufanya Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Marchi 4. Hii itakuwa ni ziara ya kwanza ya Rais Kibaki nchini tangu taifa hilo lizundue jengo lake la Ubalozi mwaka 2009 jijini Dar es Salaam.
Tanzania ilitoa sehemu ya ardhi yake kwa Serikali ya Kenya kwa ajili ya kujenga Ubalozi huo hatua ambayo ni sehemu ya kudumisha uhusiano mwema baina ya mataifa haya mawili.
Tanzania kwa sasa iko kwenye mchakato wa ujenzi wa ofisi za balozi wake baada ya kuahidiwa kupatiwa ardhi mjini Nairobi. Katika miaka ya hivi karibu Tanzania ilizindua jengo la Ubalozi wake nchini India katika hatua iliyoelezwa ni kupunguza gharama za ukodishaji wa majengo.
Katika ziara iliyopita hapa nchini, Rais Kibaki alitembelea na kuzindua Kiwanda cha Bidco Oil and Soap Limited (BOSL) kilichoko katika eneo la Mikocheni na kuahidi kukipiga jeki.
Ziara ya Mwai Kibaki inakuja katika wakati ambapo wagombea wa nafasi ya urais nchini mwake wakianza kampeni za lala salama kabla ya Uchaguzi Mkuu ambapo wachunguzi wa mambo wanasema kuwa huenda ukawa na mchuano mkali.
Wagombea wote wanatarajiwa kuwa na mdahalo mwingine mwishoni mwa wiki ijayo kabla kuwaachia fursa wapigakura kuamua kupitia sanduku la kura.
Rais Mwai Kibaki anatarajiwa kuhitimisha muhula wake wa pili na kwa mujibu wa Katiba na haruhusiwi kugombea tena.
Jumuiya za kimataifa zinafuatilia kwa karibu uchaguzi huo kutokana wasiwasi wa kujirudia tena yale yaliyoshuhudiwa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2007.
Kumekuwa na idadi kubwa ya waangalizi wa kimataifa wanaoanza kumiminika nchini Kenya.