photo NAAZ_zpsd0bbd510copy_zps37715af5.jpg
 photo NAAZ_zpsd0bbd510.jpg
Nafasi Ya Matangazo
> > SERIKALI YALIPA SH 400M WATUMISHI HEWA

SERIKALI YALIPA SH 400M WATUMISHI HEWA

Posted on Feb 20, 2013 | No Comments



SERIKALI imelipa mishahara hewa zaidi ya Sh400 milioni kwa watumishi ambao hawapo kazini Hospitali ya Enduleni, Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka huu.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi kwenye hospitali hiyo inayomilikiwa na Kanisa la Katoliki Jimbo la Arusha, umebaini takribani tangu mwaka 2009 hadi sasa, serikali imekuwa ikituma Sh8.2 milioni kila mwezi kulipa watumishi 13 ambao wameacha kazi.
Watumishi hao majina yanahifadhiwa, wanadaiwa kuacha kazi hospitalini hapo kutokana na kuzorota kwa huduma, kulikochangiwa na upungufu wa dawa na kushindwa kulipwa stahiki nyingine.
Hospitali hiyo ambayo ipo ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, imekuwa ikihudumia zaidi ya wakazi 70,000 wa Tarafa ya Ngorongoro kutokana na eneo hilo kutokuwa na hospitali nyingine.
Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dk Fransis Mwasangi alikiri hospitali hiyo kupokea kiwango hicho tangu mwaka 2009 kwa watumishi wasiokuwapo kazini.
Hata hivyo, Dk Mwasangi alisema tayari ofisi yake imepeleka taarifa serikalini kuhusu hali hiyo na kuomba majina ya watumishi hao, kuondolewa na kuingizwa mengine 13 lakini suala hilo halijafanyika.
“Ingawa siyo msemaji wa hospitali, lakini ni kweli tatizo hili lipo binafsi na wenzangu tumepeleka majina serikalini mara kadhaa ya watumishi wapya na vyeti vyao, lakini hawajaingizwa kwenye orodha ya malipo,” alisema Dk Mwasangi.
Alisema tatizo la kuendelea kupelekwa mishahara ya watumishi ambao hawapo, linazikabili hospitali nyingi nchini hasa kutokana na kutokufanyika kwa mapitio ya mishahara.
“Tuliamua fedha hizi zinazokuja hapa tuzitumie kuwalipa watumishi tulionao kwani wana sifa,” alisema.
Licha ya kuondoka watumishi hao, hospitali hiyo inakabiliwa na ukata na kushindwa kuwalipa mishahara watumishi wengine wanaodai Sh20 milioni kwa miezi sita sasa.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Afya (Tughe) hospitalini hapo, Christopha Bajuta alithibitisha kutolipwa wafanyakazi kadhaa na kwamba, tayari wametoa malalamiko kwa bodi ya hospitali.
Awali, Mhasibu mkuu wa hospitali hiyo, Damas Mapunda alikiri kupokea Sh8.2 milioni kila mwezi kwa watumishi ambao hawapo.
“Kweli tunapokea hizo fedha lakini tunazitumia kulipa wengine, tatizo ni serikali siyo sisi,” alisema Mapunda.
Mapunda alisema tayari wametoa taarifa Serikalini kuhusu kuondoka kwa watumishi hao na wengine ambao wamepatika, lakini serikali imekaa kimya.     

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru