ISRAEL YARUSHA KOMBORA SYRIA
Posted on
Nov 11, 2012
|
No Comments
Israil inasema imerusha kombora
nchini Syria, baada ya kituo chake kimoja cha jeshi katika milima ya
Golan kupigwa mzinga, ambao Israil inafikiri ni kutoka jeshi la Syria
katika mapambano yake na wapiganaji.
Tukio hilo linakuja wakati makundi
ya upinzani ya Syria, yanayokutana Qatar, yametangaza kuwa yametia saini
mkataba kimsingi kuwa na shirika moja litalokuwa na serikali ya mpito,
na kuwa ndilo linalopokea misaada kwa ajili ya maeneo yanayodhibitiwa na
wapiganaji.
Hii ni mara ya kwanza kwa Israil kushambulia jeshi la Syria, tangu vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka wa 1973.
Jeshi la Israil limesema kombora moja lilirushwa
dhidi ya Syria, baada ya kituo cha Israil kwenye milima ya Golan
kupigwa kwa mzinga.
Hakuna mtu aliyeumia.
Mizinga kadha ya Syria imeshawahi kuangukia upande wa Israil; na waIsraili walisema kuwa watajibu iwapo itatokea tena.
Ni wazi kuwa vita vya Syria vinafurika katika nchi za jirani.
Huku nyuma, upinzani umetangaza kwenye mkutano
wao mjini Doha, Qatar, kwamba umekubaliana kimsingi kuunda uongozi wa
mseto utaojumuisha makundi yote makubwa yalioko ndani ya Syria na nje.
Mataifa ya magharibi yameahidi kuwa yatatambua na kusaidia ushirika.