>
LOCAL NEWS
>
TAARIFA KUHUSU MADAI YA WANAMTWARA KUSHINIKIZA KUCHAKATWA KWA GASI
TAARIFA KUHUSU MADAI YA WANAMTWARA KUSHINIKIZA KUCHAKATWA KWA GASI
Posted on
Jan 7, 2013
|
Ndugu waandishi wa Habari kwanza ningependa kuwashukuru sana kwa kuitikia wito
wenu kuja hapa leo kuyasikiliza yale ambayo nimekusudia kuyaongea.
Pili ningependa kuwapongeza sana kwa namna mnavyoripoti habari hizi kila wakati
bila kuchoka na kuyafuatilia matukio na kueleza hoja na hisia za wananchi wa
Mtwara kila kunapokucha.
Najua ziko shutuma zilizotolewa na viongozi wa serikali kwamba wanaozungumzia
jambo hili wanatafuta umaarufu wa kisiasa,nadhani hiyo ilikuwa mbinu ya kuziba
mdomo tusizungumze.Swala hili ni nyeti na lina sura ya kitaifa ni wajibu wa
kila mpenda maendeleo ya nchi hii kulizungumzia kwa ustawi wa watu wetu,ndicho
ninachofanya leo,uzalendo unanitaka kufanya hivyo.Nikinukuu maneno ya mpigania
haki za wanawake nchini Afghanistan Mama Malalai Joya aliyewahi kusema”The
silence of Good people is worse than the actions of Bad people ” Hivyo kukaa
kwangu kimya ni kubaya zaidi kuleta matendo mabaya ya mtu yeyote yule,ili
nisiwe kwenye kundi hilo naomba nivunje ukimya huo.
Nianze kwa kusema kuwa ningependa kutoa maoni yangu kama mwananchi wa kawaida
ninayeguswa na jambo hili na ninatumia haki yangu ya kikatiba kwa mujibu ya
ibara ya 18 kipengele (A).Ingawa ukweli utabaki kuwa mimi ni mwanachama wa
chama cha mapinduzi na historia inajieleza kuwa nimeshawahi kuwa katibu
msaidizi wa CCM wilaya na mgombea wa ubunge katika kura za maoni mwaka 2010
katika uchaguzi wa ndani ya chama kwa jimbo la Mtwara Mjini.
Tangu kuanza kwa vuguvugu la mradi wa ujenzi wa bomba la gesi nimetumia muda
mwingi kuwa Mtwara kuliko Dar es Salaam ambako hasa ndiko ninakofanya shughuli
zangu.
Kabla vuguvugu hili halijachukua sura kubwa ya kitaifa yalikuwepo manun’guniko
mengi kwa wananchi yaliyoonyesha kutoridhishwa na kufanyika kwa mradi
huu.Ikumbukwe kuwa ingawa mkataba wa kupata mkopo wa ujenzi wa bomba kutoka
benki ya Exim china(Takribani usd 1Bill) ulisainiwa nchini china tarehe 26
september 2011 na ujumbe uliiongozwa na waziri wa wakati huo wa Nishati na
Madini William ngeleja,kujulikana kwa utekelezwaji wa mradi huu kwa watu wengi
ulikuwa ni pale mheshimiwa Rais alipozindua mradi wa kujenga mtambo wa kufua
umeme kinyerezi tarehe 8/November/2012 ambao ungetokana na gesi kutoka Mtwara
ikiungana na bomba la songosongo,hapa ikiwa ni takribani mwaka mmoja kupita
tangu kusainiwa.
Kwa kulitazama jambo hili kutokea mbali na kwa kutoridhishwa na ukimya
uliotawala kwa viongozi wa serikali na wawakilishi wa wananchi,nilichukua hatua
za makusudi kufanya ufuatiliaji mbalimbali.Hatua yangu ya kwanza ilikuwa kwenda
TPDC ofisi ya mkurugenzi tarehe12 december 2012 ikiwa ndiyo mwakilishi wa
serikali anayesimamia mradi huu ili kuhoji mambo kadhaa na kutoa mtazamo wangu
wa umuhimu wa kusimamishwa kwa mradi huu ili kusikiiliza kilio cha
wananchi.Ingawa sikufanikiwa kuonana na mkurugenzi nilifanikiwa kukutanishwa na
wakuu wa kitengo cha malalamiko yanayohusu mradi huu ambao kwa ukweli ni kwamba
walisisitiza tatizo kubwa ni kutokuelewa kwa wananchi na kupuuza hoja yangu ya
msingi ya kutaka ujenzi wa bomba hili usimamishwe ili kusikiliza hoja za msingi
za wananchi.
Baada ya hapo nilichukua hatua ya kuomba msaada wakisheria kutoka kituo cha
sheria na haki za binadamu ili kusitisha mradi huu kwa kuwasiliana na
mkurugenzi wa kituo hicho Bi hellen Kijo bisimba mnamo tarehe 17dec 2012 ambaye
alinieleza kuwa alishatuma ujumbe wake Mtwara na wako katika hatua za kuandika
ripoti hivyo niisubirie.Kwa bahati mbaya sana bado sijafanikiwa kuipata ripoti
yao.
Sikuishia hapo,niliamua kuandika barua kwa ngazi za manispaa ya Mtwara mnamo
tarehe 18 dec 2012 ikiwa na madai kadhaa na mapendekezo ya nini kifanyike
kuhusiana na mradi huu.Kati ya madai yangu ilikuwa kumtaka meya wa manispaa
kuitisha kikao cha haraka cha baraza la madiwani kulijadili jambo hili kama la
dharura wakiwa ndio wawakilishi wa wananchi na kutoa msimamo wao kwa serikali
kuitaka kusitisha mradi huu na kusikiliza kilio cha wananchi.Juhudi hii nayo
haikuzaa matunda kwani sikupata jibu lolote la barua yangu wala utekelezaji
wake hadi hii leo.
Baada ya hapo nilishiriki kikamilifu katika mijadala ya sera na vipindi
mbalimbali vya redio nikihimiza kusitishwa kwa ujenzi wa bomba hili hadi pale
hoja za wananchi zitakapojibiwa kama vile nilivyonukuliwa katika gazeti la
mwananchi la tarehe 26 december 2012 ukurasa wa kumi ikiwa ni siku moja kabla
ya kufanyika maandamano makubwa siku ya tarehe 27.
Nimeeleza haya yote ili kuonyesha kuwa kwa mtu yeyote anayeona mbali ni lazima
alijua kuwa bila ya kusikilizwa kwa kilio hiki cha wananchi ni lazima tungefika
hapa tulipo na kuna uwezekano wa kwenda mbali zaidi kuliko hapa kama hatua
stahiki hazitachukuliwa.
Baada ya kusema hayo ningependa kutoa masikitiko yangu kwa kauli za
kejeli,dharau na kukatisha tamaa zilizotolewa na viongozi waandamizi wa
serikali Mh.Waziri Sospeter Muhongo na mkuu wa mkoa wa Mtwara(Joseph Simbakalia)
mara baada ya maandamano ya tarehe 27 dec.Pia napenda kueleza kusikitishwa na
Rais Jakaya Kikwete kwa kauli yake aliyoitoa kuhusu ujenzi wa bomba hili katika
salamu zake za mwaka mpya,napenda kutumia nafasi hii kumshauri Mh.Rais,Waziri
wa Nishati na Madini na Mkuu wa mkoa kupitia upya madai 9 yalisomwa siku ya
maandamano ili kutoupotosha mjadala na madai ya watu wa Mtwara.
Nimetoa rai hiyo kwasababu ukipitia hotuba za viongozi hawa wote utagundua kuwa
aidha wamepewa taarifa zisizo sahihi kuhusu madai ya wanamtwara ama wamefanya
haraka kujibu au hawajaelewa kabisa madai ya wanamtwara.Kwani kilichofanyika si
kujibu madai yao bali kuonyesha jinsi ambavyo hawako tayari
kuwasikiliza,nadhani mtazamo huu ndio unaochochea jambo hili kuwa kubwa kila
siku na kuwapa mtazamo wananchi kuwa kuna ajenda ya siri katika hili.
Naomba kuchukua nafasi hii kueleza kuwa WANANCHI WA MKOA WA MTWARA HAWAPINGI
WANANCHI WA MIKOA MINGINE KUNUFAIKA NA FAIDA ZA GESI BALI KINACHOPINGWA NI
KUSAFIRISHA GESI GAFI TOFAUTI NA AHADI YA SERIKALI YA KUJENGA MTAMBO WA
KUZALISHA UMEME MKOANI MTWARA UTAKAOVUTIA WAWEKEZAJI WA VIWANDA.UMEME HUU
UNAWEZA KUSAFIRISHWA KWENDA MAHALI POPOTE TANZANIA/NJE YA NCHI BAADA YA MTAMBO
KUJENGWA MTWARA.
Naomba kukumbusha kuwa madai haya hayajotoka hewani,bali yametokana na sababu
kadhaa:
1. Ni ahadi za mara kwa mara zilizokuwa zilizotolewa na Mh.Rais na mawaziri wa
Nishati na Madini katika nyakati tofauti.Tangu mara ya kwanza Mh.Rais
alipohojiwa clouds(kipindi cha power breakfast) tarehe 29 october katika kampeni
ya mwaka 2010,pia alipokuja kwenye kampeni Mtwara na hata alipokuja kushukuru
baada ya kuwa Rais aliendelea kuahidi kuufanya Mtwara kuwa mji wa viwanda kwa
kuupatia umeme wa uhakika kupitia ugunduzi wa gesi hii,pia alieleza katika
kipindi hicho cha radio kusudio la serikali yake kujenga mtambo wa 300MW.Hii
yote ilitengeneza matumaini makubwa kwa wananchi wa Mtwara wa kufaidika na gesi
hii.Leo tunaposikia gesi ghafi inahamishwa na bado hakuna mtambo huo wala
kiwanda sawa na ahadi zilivyotolewa,kuna kosa gani wananchi wakihoji?
2. Mpango wa Mtwara power project uliolenga kuufanya mradi huu kuwa sehemu ya
National power Development plan(3920MW) ukilenga kuwa na mtambo wa kuzalisha
300MW Mtwara zitakazoingizwa katika gridi ya Taifa na kuondoa tatizo la umeme
nchini uliokuwa umelenga kukamilika mwaka 2012.Ingawa ni wazi kuwa kampuni
iliyokuwa itekeleze mradi huu Artumas ilishindwa kutokana na mtikisiko wa
kiuchumi wa mwaka 2008,iliweka bayana kuwa ingepata dola za kimarekani milioni
7 ingeweza kuutekeleza.Kwa nini serikali haikuweka kama sharti mojawapo kwa
kampuni ya Wentworthy resource Limited iliyoinunua artumas kuutekeleza mradi
huu uliokuwa umekubalika kuingia katika mpango wa kitaifa?kwa nini
uliachwa?Hili nalo hatuna majibu kama ilivyo kwa mipango mingine kama vile
Mtwara Corridor.
3. Ikumbukwe kuwa kisiwa cha songosongo ndio eneo la kwanza kugunduliwa kwa
gesi asilia mwaka 1974 na kampuni ya AGIP kukiwa na takriban cubic feet 783
billion.Kati ya mipango mingi iliyowekwa kwa wakati huo kuhusiana na kubadilisha
maisha ya wanasongosongo na kilwa kwa ujumla ni kujenga kiwanda cha mbolea
KILWA AMMONIUM COMPANY,kilicholenga kutatua tatizo la ajira na kutosheleza
uzalishaji wa mbolea nchini.Waliambiwa wasiwe na hofu gesi kwenda Dar es Salaam
kwani viwanda vitajengwa kilwa,Ingawa eneo lilitengwa kwa ujenzi wa kiwanda
hicho na wataalamu kusomeshwa,hadi hivi leo kiwanda hakijajengwa. Hivi hali
kama hii haitoshi kuleta wasiwasi kwa wananchi?kuna tatizo gani wakihoji jambo
hili?Waswahili husema ukiona mwenzako ananyolewa,wewe tia maji.
Kama viwanda hivi vitafanikiwa vitaleta tija na ulazima wa kuifufua bandari ya
Mtwara ambayo tangu mwaka 2006/2007 imekuwa ikitumika kwa 31% ya uwezo
wake(Tani 122,862 kwa mwaka badala ya tani 400,000 kwa mwaka).Mbinu hii
itasaidia kupunguza msongamano wa bandari ya Dar kama ambavyo nchi Jirani ya
Kenya wamefanya kwa kuipanua bandari ya Lamu ili kupunguza msongamano bandari
ya mombasa.
4. Hoja nyingine ni ya kihistoria,Tangu tupate uhuru watu wa kusini wamesota
katika janga la kukosa nishati ya umeme kwa muda mrefu na hawakuunganishwa na
gridi ya taifa kwa sababu lukuki ingawa iliwezekana kuvusha umeme baharini
kwenda Zanzibar ilishindikana kuuleta Mtwara.Kama wameweza kusahauliwa kwa
miaka 51 katika swala la nishati,hofu ni kuwa gesi itakapoisha vizazi vyao
vitasahauliwa tena kwa kubaki na bomba tupu,na hakuna atakayekumbuka tena
kuunganisha mikoa hii na Gridi ya Taifa ili kuwa na umeme wa uhakika ambao ndio
hitaji kubwa mojawapo la wawekezaji.Hoja ya gesi kuwa nyingi sana na itachukua
muda mrefu kuisha haina mashiko kwani hata dhahabu tuiyokuwa tunajivunia kuwa
ni nyingi sana katika mgodi wa Nzega uliokuwa unachimbwa na kampuni ya Resolute
umefungwa mwaka jana august,dhahabu imeisha,hivyo hata gesi itaisha tu,tufanye
maamuzi ya busara.
5. Ilani ya chama cha mapinduzi(2010) katika ibara ya 63(h) na (k) ilianisha
miradi ya kinyerezi(240MW) na mradi wa Mnazi bay(300MW) kama miradi miwili
tofauti inayojitegemea.Hivyo tunashangaa leo inapoonekana kuwa ni mradi
mmoja.Tunataka kila mmoja uendelee kama ulivyopangwa na si vinginevyo.Hii ndiyo
itawezesha ahadi ya ujenzi wa kiwanda cha UREA kilichopangwa kujengwa Mtwara
kama inavyoainishwa katika Ibara ya 49(e) kufanikiwa.Lakini hii pia itawezesha
uhakika wa uanzishwaji wa kiwanda cha kubangulia korosho kama
makubaliano(Memorandam of understanding) yaliyoingiwa kati ya TIB(80% Tanzania
Investiment bank) na Tandahimba Newala Cooperative union(20%TANECU)
kukamilika.Nadhani Kuyatekeleza tuliyoahid ndio njia bora ya kutimiza ahadi na
kuboresha maisha ya watanzania.
6. Kwa kuwa kipaumbele cha watu wa Mtwara si kuwa na umeme majumbani ambao ni
ongezeko la gharama la maisha kiuchumi(na kwa kuzingatia kuwa nyumba nyingi za
mji wa Mtwara hazina sifa ya kuunganishiwa umeme kwani ni za nyasi,udongo na
makuti na kipato chao cha sasa kinawanyima uwezo wa kuipa bili za kila
mwezi)Kipaumbele kinabaki ni kupunguza makali ya maisha kwa kuwa na uhakika wa
kipato kwa njia ya ajira kwa shughuli za uzalishaji viwandani na shughuli
zitakazoambatana na hizo,Ni vema serikali ikazingatia kauli ya Mkurugenzi mkuu
wa Wentworthy resource Limited Inayochimba gesi ya Mnazi Bay Bwana Bob Mcbean
iliyoripotiwa tarehe 6 December London mwaka 2012 kuwa watapata faida kubwa kwa
kuwekeza katika kiwanda cha mbolea na kemikali nyingine,hivyo ni vyema mkazo
ukawa katika kuhimiza uwekezaji zaidi kupitia gesi hii na uhakika wa nishati ya
umeme kutokana na mtambo wa kufua umeme utakaojengwa Mtwara.
TUJIFUNZE KWA WENZETU.
Tanzania si nchi ya kwanza kuchimba gesi katika dunia wala Afrika.Katika bara
la afrika tunazo nchi kama Algeria,Misri na Nigeria ambazo husafirisha gesi nje
ya nchi.Tukiwa nchi ya 66 duniani tukizalisha 658,000,000cubic metres,jirani
zetu msumbiji ni wa 50 wakizalisha 3,600,000,000cubic metres(takwimu za mwaka
2012).
Tanzania kwa sasa inasadikika kuwa na kiasi cha 43 Trillion Cubic feet (TCF)
ukilinganisha na kiasi cha 2.8Trillioni cubic Metres(98.896Trillion cubic feet)
za msumbiji ambazo ni zaidi ya mara mbili ya kiwango tulichonacho hivyo si
vibaya tukijifunza kwao.
Kwa sababu ya mipango mizuri ya kiuchumi ya Msumbiji haikuwa lazima kujenga
kila kitu Maputo/beira ambayo ni miji ya biashara lakini mtambo wa kuzalisha
gesi ya 107.5MW umejengwa na kampuni ya Aggreko katika mji wa pembeni wa
Ressano Garcia utakaopeleka umeme Maputo na miji mingine ya Afrika kusini
ambako katika miji hii umeme huu utasafirishwa na kutumika kwani ndio miji
mikubwa ya kibiashara kama ilivyo Dar Es Salaam .Ingawa umbali wa Maputo na
Ressano Garcia ni 1/5 ya umbali wa Dar-Mtwara,tunaweza kujifunza kwao katika
hili.
Akizindua mradi huo mwezi July 2012 Rais wa msumbiji Mh.Armando Guebuza
alieleza kuwa wanakusudia kujenga mitambo ya kuweka gesi katika hali ya
kimiminika ipatayo 10(liquefied natural gas (LNG) plants) katika maeneo
mbalimbali ya msumbiji.Hii yote ni kutawanya uchumi na kutengeneza fursa
mbalimbali kwa wananchi wa kawaida wa Msumbiji.Hili nalo linaweza kufanyika
Tanzania.
NINI KIFANYIKE?
1. Kwa sababu bomba hili halisafirishi chakula cha dharura kwamba likisitishwa
watu watakufa katika jiji la Dar Es Salaam,Serikali itangaze rasmi kusitishwa
kwa mradi huu wa ujenzi wa bomba mara moja kutokana na kilio cha wananchi na
izijibu hoja 9 za wananchi zilizotolewa katika maandamano ya tarehe 27 december
2012.
2. Mkuu wa mkoa na waziri wa nishati na madini wawaombe radhi wananchi wa
Mtwara kwa maneno yao ya kuudhi kwa kuita maandamano yao kuwa ni ya
kipuuzi,wahaini na wasioelewa ili kuonyesha kuwa walikosea.Wasipofanya hivyo ni
kusema walikusudia kuyasema hayo na kwa jinsi hiyo ni kuchochea mikutano na
maandamano yanayoendelea,hivyo kwa lolote litakotokea watastahili kuwajibishwa.
3. Uwekwe mpango maalumu wa viongozi waandamizi wa serikali kuja mtwara na
kukutana na wananchi wa mtwara Haraka ndani ya siku 14 zijazo.Nia sio kuwaambia
gesi lazima itoke bali ni kuwasikiliza na kufanyia kazi hoja zao.
4. Wabunge wa mkoa wa Mtwara na Lindi waache malumbano kati yao bali wajitokeze
hadharani na kueleza msimamao wao wa pamoja kuhusiana na jambo hili.
ANGALIZO
Swala la gesi linalenga kuwafaidisha wananchi wote wa Tanzania kama vile sera
ya serikali inavyosema.Wananchi wa Mtwara ni sehemu ya Taifa hili nao wanahaki
ya kuhoji na kutathmini utekelezwaji wa yale waliyoahidiwa na viongozi
wao.Kuwanyima fursa hiyo ni kuwatenga na utajiri wa Taifa lao.
Ningependa kurudia kwa kusema kuwa,wananchi wa Mtwara hawasemi wananchi wa
maeneo mengine ya Tanzania hawapaswi kufaidika na gesi inayozalishwa
Mtwara,hoja yao ni kuhusu faida zilizozungumzwa na viongozi hapo kabla
kuhusiana na viwanda na umeme.Hili ndilo linalotakiwa kufanyiwa kazi kwa
sasa.Ingawa ni kweli kwamba sio serikali inayojenga viwanda hivi lakini ndiyo
yenye dhamana ya kufanya hivyo kama ilivyoahidi.
Ikumbukwe kuwa kufanikiwa kwa ujenzi wa mtambo wa kufua umeme Mtwara utatoa
mwongozo wa utekelezaji wa miradi kama hii katika maeneo mengine ya Nchi yetu
ambako gesi inaendelea kugundulika.
Mungu Ibariki Tanzania,
Mungu Ibariki Mtwara,
Mungu Ibariki Gesi Asilia isaidie kuinua maisha ya watanzania Maskini,
Ahsanteni Sana.
JOEL NANAUKA
0713-243 244
MDAU WA MAENDELEO.